Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kimeanza kuchukua hatua za kisheria dhidi ya Nape Nnauye Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM kufuatia madai ya uzushi na uongo aliyoyatoa tarehe 12 Agosti
2012 kuwa anao ushahidi kwamba CHADEMA kimekuwa kikiwahadaa wananchi kwa
kuwachangisha fedha huku kikipokea mabilioni ya fedha kutoka kwa wafadhili
kutoka nje.
Izingatiwe kuwa matamshi yake yalitangazwa
na vyombo vya habari vya kielekroniki ikiwemo vituo vya televisheni, radio na
kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii tarehe 12 Agosti 2012 na katika kurasa za
mbele za magazeti mbalimbali tarehe 13 Agosti 2012.
Bodi ya Wadhamini wa CHADEMA iliagiza
wanasheria wamwandikie barua ya kumtaka kukiomba radhi Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo kwa kutumia njia ile ile aliyotumia kufanya propaganda chafu za
kuikashifu na kuifitisha CHADEMA kwa umma wa watanzania ikiwemo kuzusha kuwa
upo uwezekano wa CHADEMA kupewa fedha hizo kwa mikataba yenye masharti ya
kuiweka nchi rehani.
Tayari ameshaandikiwa barua ya kisheria
tarehe 24 Agosti 2012 ya kumtaka aombe radhi na kulipa fidia ya bilioni tatu
kwa matamshi hayo ya uzushi na uongo yenye maana ya kuwapotosha waliyoyasikia
na kuyasoma kuwa CHADEMA kinawalaghai wananchi, kina viongozi wasio waaminifu
na kwamba kiko tayari kuuza nchi wa uroho wa madaraka.
Kipaumbele cha CHADEMA katika suala hili ni
kuombwa radhi hata hivyo kiwango cha fidia ya fedha kwa fedheha kilichotakiwa
ni fundisho kuwa uzushi na uongo unagharimu.
Ikumbukwe kwamba tarehe 12 Agosti 2012
nilitoa kauli ya awali baada ya mkutano Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM na
waandishi wa habari ambapo pamoja na mambo mengine nilieleza kwamba tutatoa
tamko la kueleza hatua za ziada baada ya kupata taarifa kamili aliyoitoa.
Katika kauli hiyo nilitoa mwito kwa
Mwenyekiti wa CCM Rais Jakaya Kikwete kueleza watanzania iwapo propaganda hizo
chafu zina baraka zake; hivyo ukimya wake mpaka sasa kuhusu matamshi hayo
inakifanya CHADEMA kuwa na imani yenye shaka (benefit of doubt) kwamba Nape
hakutumwa na chama chake kutoa matamshi aliyoyatoa.
CHADEMA inachukua fursa hii kuutaarifu umma
kwamba asipotekeleza matakwa hayo ndani ya siku saba kuanzia tarehe hiyo
aliyopokea barua hatua nyingine ya kumfikisha mahakama kuu zitaanzishwa ili
aweze kuchukuliwa hatua zaidi.
Pamoja na kuchukua hatua za kisheria,
CHADEMA kinaendelea kutimiza dhima yake ya kuleta uongozi bora, sera sahihi,
mikakati makini na oganizesheni thabiti kwa maendeleo endelevu ya Tanzania kwa
pamoja na mikakati mingine kutekeleza operesheni ya vuguvugu la mabadiliko
nchini (M4C) na tunawashukuru wananchi kwa kuendelea kuunganisha nguvu ya umma
kwa hali na mali katika maeneo mbalimbali nchini.
Imetolewa tarehe 26 Agosti 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa
Habari na Uenezi
No comments:
Post a Comment