Na Hafidh Kido
Mradi wa mabasi yaendayo kasi
jijini Dar es Salaam unategemea kuzalisha ajira elf 80 pindi itakapokamilika
awamu ya kwanza ya mradi huo mwaka 2014 ambayo inahusisha barabara ya morogoro
kutoka Kimara mpaka Kivukoni.
Akizungumza na kidojembe
katika ziara ya kamati ya mradi huo wiki iliyopita mkurugenzi wa mradi injinia
Enock Kitandu, alisema mbali na kupunguza msongamano wa magari jijini lakini
pia wamelenga kutoa ajira kwa vijana na makampuni binafsi ya kizalendo.
“Hapa kituo cha kivukoni tu
tunategemea kutoa ajira elfu 15, na tutakuwa na vituo takriban vine kwa awamu
ya kwanza ambapo tunategemea kuzalisha ajira elfu 80, ni hatua kubwa sana hasa kwa kipindi hiki
cha matatizo ya ajira. Lakini mbali ya watu watakaoajiriwa lakini kutakuwepo na
mambo mengine ambayo yatapasa watu kujiajiri kama
kufanya biashara ya vyakula na vinywaji katika vituo na huduma nyingine ambazo
hutokea kutokana na mahitaji,” alisema.
Kwa kipindi cha miezi kadhaa
kumekuwepo na sintofahamu kwa wakazi wa jijini hasa wale wanaotumia barabara ya
morogoro kwa kuona ujenzi unaendelea lakini wengi wao hawakuwa wakijua ni nini
hasa kimekusudiwa kujengwa hasa katika kufahamu baada ya ujenzi kukamilika
mabasi hayo yataptia wapi, magari madogo yatapitia wapi na waenda kwa miguu watakuwa
na nafasi gani.
Kwa mujibu wa injinia Kitandu
anaeleza kuwa barabara itakuwa na njia nane, mabasi yaendayo kasi yatakuwa na
njia nne za katikati ambazo hazitoingiliana na magari mengine. Halafu njia nne
za pembeni (mbili kila upande) zitakuwa za magari madogo ya binafi na waenda
kwa miguu watapita pembeni kabisa, ambapo kwa mujibu wa mkurugenzi huyo baada
ya ujenzi kukamilika hakutaruhusiwa daladala kupita katika njia hiyo.
Akizungumzia kuhusu aina ya
mabasi yatakayotumika alisema kuwa kutakuwa na mabasi ya aina mbili mabasi
mlisho; ambayo ni madogo yenye uwezo wa kubeba abiria 60 waliokaa na mabasi
makubwa yenye uwezo wa kubeba abiria 140 waliokaa.
“Kutakuwa na mabasi aina
mbili mabasi mlisho na mabasi makubwa, haya mabasi mlisho au kwa lugha ya kigeni
‘feeder buses’ kazi yake ni kuchukua abiria kutoka maeneo ya ndani kama kigogo ama magomeni ambamo mabasi makubwa hayapiti
na kuwaleta barabarani kupanda mabasi ya kasi.
“Halafu kutakuwa na mabasi
makubwa yatakayopewa majina ya Chui, Simba, Duma, Pundamilia, na Twiga kutokana
na rangi ambayo yatakuwa na uwezo wa kubeba abiria 140 waliokaa au
ikisimamisha; ambapo kisheria inaruhusiwa itakuwa na uwezo wa kuchukua abiria
270 kwa safari moja. Msishangae haya mabasi ni makubwa sana yatakuwa na urefu wa mita 18.5. Na ili
kuleta usawa kutakuwa na sehemu ya mizigo na hata viti vya watu wenye mahitaji
maalum kama wazee na vilema,” alieleza
Kitandu.
Nae mtendaji mkuu wa mradi
huo Cosmas Takule, alisema mradi utakuwa na awamu sita lakini awamu ya kwanza
itakapokamilika mnamo mwaka 2014 zitakuwa zimetumika kiasi cha Tsh 470bil
ambapo pesa hizo zimetoka bank ya dunia. Na kila baada ya miaka miwili
watahakikisha wanakamilisha awamu moja hivyo kufanya mpaka kufikia mwaka 2025
jiji la Dar es Salaam litakuwa halina shida ya usafiri kwa namna yoyote ile.
“Hizi fedha Tsh 470bil
zinatoka bank ya dunia na ni mkopo usio na masharti, na kila tutakapokamilisha
awamu moja watakuwa wanatuletea pesa nyingine kwa ajili ya awamu ya pili.
Ambapo awamu ya kwanza itahusisha kilomita 20.9, awamu ya pili 19.3km, awamu ya
tatu 23.6km, awamu ya nne 16.1km, awamu ya tano 22.8km na awamu ya sita ni
27.6km.
“Awamu ya kwanza ni barabara
za morogoro, kawawa, kivukoni, sokoine na msimbazi. Awamu ya pili itahusisha
barabara ya Kawawa upande wa kusini, awamu ya tatu ni barabara ya Nyerere
ambapo itapitia mtaa wa uhuru, bibi Titi na mtaa wa Azikiwe. Awamu ya nne
barabara ya Kilwa, awamu ya tano barabara ya Mandela na awamu ya sita itakuwa
ni barabara ya Old Bagamoyo, nadhani hayo ndiyo maeneo korofi katika msongamano
wa magari jijini,” alifafanua Takule.
kidojembe ilipozungumza na
kaimu mkurugenzi wa jiji Mussa Matty, ambae ni mjumbe wa kamati ya mradi huo
iliyo chini ya uenyekiti wa Meya wa Dar
es Salaam Dk Didas Masaburi alisema “Huu mradi umeanzia
ofisi za jiji mwaka 2002 ambapo ndipo wazo la kuondoa kero ya msongamano wa
magari lilipokuja.
“Mwaka 2010 tulishinda nafasi
ya kupata msaada kutoka bank ya dunia ili kutengeneza miundombinu ya barabara
za miji mikubwa barani Afika. Kulitangazwa nafasi ya kuandika miradi ili kuweza
kuwasilisha bank ya dunia ili kupewa msaada huo, tulishiriki miji mingi lakini
baada ya mchujo tukabakia miji mitatu Accra (Ghana ), Lusaka (Zambia ) na sisi Dar es Salaam .
“Hatimae baada ya mchujo
mwingine sisi tukafanikiwa kuibuka kidedea na sasa mnaona mambo yameshaanza.
Kamati yetu imetembelea miji mingi kuenda kuangalia maendeleo ya barabara hizi
za mabasi yaendayo kasi tumejifunza mengi hasa tulipokuwa Bogota
nchini Colombia ,
naamini tutafanya kile ambacho bank ya dunia ilikusudia kukiona,” Matty.
Hata hivyo mradi wa mabasi
yaendayo kasi bado unakumbwa na changamoto nyingi sana kiasi inaweza
kuchelewesha mradi kukamilika kwa wakati, kwa mfano mpaka sasa kituo cha
gerezani palipokuwa na nyumba za bandari mpaka sasa ujenzi haujaanza kutokana
na kesi iliyofunguliwa na wananchi wa eneo hilo kwa madai kuwa hawajalipwa
fidia yao.
Mtendaji mkuu wa mradi Cosmas
Takule, alisema watu hao walishalipwa pesa zao lakini bado wanasisitiza kupewa
zaidi kwa madai kuwa kiasi walichopewa hakilingani na thamani ya ardhi yao kwa wakati huu.
Kwa mujibu wa Takule,
gerezani ndiyo itakuwa kituo kikuu cha mabasi hayo lakini mpaka sasa hakuna
kilichofanyika hata msingi haujajengwa kutokana na mgogoro huo, maana eneo hilo litajengwa vituo
‘terminal’ vitatu yaani mabasi yaendayo kasi na usafiri wa reli ambao ni mradi
mpya wa kukabiliana na msongamano jijini. Pia kutakuwa na jingo la mawasiliano
kwa vituo vyote (control centre), ambapo itakuwa ni makao makuu ya mabasi yote
kwani taarifa za wasafiri na mwenendo wa mabasi utakuwa unaendeshwa kutoka
kituo hicho.
Kuhusu nauli Takule hakutoa
majibu ya moja kwa moja juu ya viwango ingawa alisisitiza kuwa mradi huo
umedhaminiwa na bank ya dunia bila masharti yoyote maana yake Serikali wala
viongozi wa jiji hawatakuwa na maslahi yoyote katika mradi huo ila ni
kuhakikisha uendeshaji wake unakuwa mzuri ili kila mmoja aweze kumudu.
“Siwezi kusema nauli itakuwa
ni shilingi ngapi lakini nataka kukuahidi kuwa mradi huu umewalenga watu wa
hali ya chini, yaani wale wasiokuwa na magari, wasiomudu kupanda bajaji,
wasiomudu kupanda daladala tena hasa wale ambao wanatembea kwa miguu.
“Utaratibu utakuwa ni kupewa
kadi maalum ambayo utakuwa unajaza pesa kutokana na uwezo wako, ukifika katika
vituo vyetu unaingiza katika mashine maalum ambapo utakatwa nauli kutokana na
mahali unapokwenda, itakuwa ni gharama ndogo sana . Faida yake ni kuwa kama utajaza pesa
katika kazi yako kwa mwezi mzima hata kama
huna pesa mfukoni utakuwa unapanda basi kwa mwezi mzima,” alifafanua Takule.
Mji wa Dar es Salaam ni moja
ya miji inayokuwa kwa kasi sana katika Afrika hivyo kuvutia watu wengi mbali ya
wageni kutoka nchi jirani na nchi za mbali lakini hata watanzania wanaoishi
mikoa mingine nchini huvutika na shughuli za kijamii na kiuchumi zinazofanyika
Dar es Salaam, hivyo kuufanya ni mji wenye watu wengi kuliko miji yote nchini
Tanzania.
Dar es Salaam inakisiwa kuwa
na wakazi milioni nne ambapo idadi kubwa ya wakazi asubuhi huenda mjini hivyo
kuhitaji usafiri kila siku asubuhi na jioni, hali hiyo huufanya mji wa Dar es
Salaam kuwa na msongamano wa magari wakati wa asubuhi na jioni si tu kwa
wanaotumia usafiri wa umma lakini hata wanaotumia usafiri wa binafsi adha hiyo
inawakumba.
Katika miaka ya nyuma
kuliwahi kuja mabasi aina hii yakiitwa ‘icarus’ ambapo yalisaidia sana kupunguza msongamano
wa watu katika usafiri wa umma, lakini baada ya kukosa matunzo mabasi yale
yalishindwa kuendelea kuwepo barabarani.
Hata hivyo tatizo sasa si
idadi ya mabasi yanayotoa huduma bali miundombinu ya barabara kutoandaliwa
kuweza kukabiliana na ongezeko kubwa la watu namna hii, hivyo wazo la kutafuta
mabasi makubwa yatakayopita njia yake pekee na kutanua barabara kutoka mistari
mine mpaka minane inaweza kupunguza adha ya usafiri jijini.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM , TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
21 August, 2012
No comments:
Post a Comment