Na. Aron Msigwa –
MAELEZO.
26/8/2012, Lilongwe , MALAWI .
Hayo yamebainishwa
katika mkutano wa wataalam na viongozi kutoka serikali ya Malawi na Tanzania kushindwa kufikia muafaka
uliokusudiwa kuhusu eneo halali la mpaka unaotenganisha nchi hizo.
Akizungumza wakati wa
kuhitimisha kikao cha usuluhishi kilichohusisha timu za wataalam na viongozi wa
wizara husika wa nchi hizo kilichomalizika jana usiku mjini Lilongwe Waziri wa
mambo ya nje na Ushirikiano wa Kimataifa wa Tanzania Bernard Membe amesema
Tanzania bado inaamini katika mazungumzo ili kufikia muafaka wa kudumu wa
mgogoro huo.
Amesema kuwa pamoja na
sababu mbalimbali zilizotolewa na upande wa serikali ya Malawi juu ya umiliki
wa eneo lote la ziwa Nyasa ,msimamo wa Tanzania juu ya mpaka unaozitenganisha
nchi hizo uko wazi kwa kwa kuzingatia vielelezo vya historia vilivyoachwa na
wakoloni na sheria za kimataifa kuhusu mpaka kuwa katikati ya ziwa hilo.
Ameeleza kuwa licha ya
serikali ya Malawi
kuonyesha kila dalili za kukwamisha mazungumzo hayo yaliyoanza kupitia vikao
mbalimbali nchini humo viongozi wa nchi hizo kupitia mkutano wa kutafuta suluhu
uliomalizika jana usiku wameamua kuunda timu za wataalam
“Licha ya kuwasilisha
vielelezo kuonyesha uhalali wa mpaka hatukuweza kufikia muafaka tumefika mahali
pa kuhitaji msaada tuzitume tume za nchi zetu zitoe mapendekezo ya nini
kifanyike maana kuna kila dalili kwamba sisi wenyewe tutashindwa kuendelea
zaidi “
Amesema kuwa wataalam
kutoka Malawi
na Tanzana watakutana mwezi Septemba jijini Dar es salaam ili waweze kutoa
mapendekezo ya namna bora ya kuwapata wasuluhishi wa mgogoro huo pamoja na
kutoa mapendekezo ya faida na hasara ya njia watakazozipendekeza.
“ Sasa tumefika mahala
pa kuhitaji msaada,tutazituma timu zetu zikae pamoja na kutoa mapendekezo ya
nini kifanyike maana inaonyesha wazi kabisa sisi wenyewe hatutaweza kuendelea
tena sasa timu zitatoa mapendekezo juu ya kesi hii tuwaite wazee wenye busara
barani Afrika tunaowaamini watuamulie” amesema.
Amefafanua kuwa timu za
wataalamu zitakazoundwa zinatarajia kukutana mwezi Septemba jijini Dar es salaam
ili kutoa mapendekezo ambayo yatapelekwa kwa marais wa nchi hizo katika
kuelekea hatua ya pili ya utatuzi wa mgogoro huo ikiwemo kumtafuta msuluhishi
au kwenda kwenye mahakama ya Kimataifa.
Aidha , Tanzania
imeitaka Malawi kusitisha shughuli za utafiti katika eneo la Tanzania katika
ziwa Nyasa lililo na mgogoro na kukisisitiza kuwa mchakato wote wa kutafuta
suluhu utaendeshwa kwa amani na utulivu huku akiwaomba watanzania kuendelea
kuiombea nchi amani ili suala hilo limalizike kwa amani ,utulivu na undugu.
Kwa upande wake waziri
wa Mambo ya Nje na Mahusiano ya kimataifa wa Malawi Bw. Ephraimu Chiume katika
maelezo yake wakati wa kuhitimisha mkutano huo amesisitiza kuwa licha ya
mgogoro huo kuhitaji busara zaidi bado serikali yake inaamini kuwa mpaka kati
yake na Tanzania uko upande
wa mashariki mwa ziwa Nyasa na unatenganishwa na ardhi ya Tanzania .
Amesema kutokana na
unyeti wa suala lenyewe na eneo hilo
pamoja na historia ya nchi yake anapenda kuona ufumbuzi ukipatikana haraka ili
wananchi wa nchi mbili waweze kuendelea na shughuli zao bila hofu yoyote.
“Ni matumaini yangu
mkutano wa Dar es salaam
utaofanyika mwezi Septemba utazaa matunda ili suala hili lipatiwe ufumbuzi na
ikiwezekana tupate msaada wa sheria za kimataifa kwa sababu suala hili liko
kisheria zaidi” alisisitiza Bw. Chiume.
Ujumbe wa wataalam
kutoka Tanzania uliokuwa ukitafuta suluhu ya mgogoro huo uliwahusisha makatibu
wakuu Patrick Lutabanzibwa (Ardhi),John Haule(Mambo ya nje) na mawaziri wa
wizara ya Ardhi Prof. Anna Tibaijuka na Bernard Membe wa Mambo ya Nje na
ushirikiano wa Kimataifa, balozi wa Tanzania nchini Malawi Patrick Tsere pamoja
na wataalam wanaotoka eneo la ziwa Nyasa akiwemo Prof.Hemphrey Kamisama ambao
nao walitoa maelezo kueleza hisia za wananchi wa eneo hilo na uhalisia wa ziwa
hilo.
No comments:
Post a Comment