Tuesday, August 28, 2012

Vurugu Mombasa siku ya pili...


Hali ya taharuki ikiendelea kutanda mjini Mombasa siku moja baada ya kuuawa kwa mhubiri wa kiisilamu , ripoti zinasema kuwa shambulio la guruneti limefanywa dhidi ya gari la polisi na kusababisha kifo cha polisi mmoja.
Afisaa mkuu wa polisi mjini humo amethibitisha kifo hicho pamoja na kusema kuwa watu wengine kumi na tatu wamejeruhiwa vibaya katika shambulio hilo.
Wakati huohuo, watu 12 wamekamatwa na polisi kufuatia makabiliano kati ya polisi na vijana wanaofanya vurugu kufuatia kuuwawa kwa kiongozi wa kidini Sheikh Aboud Rogo siku ya jumatatu.
Katika siku ya pili ya vurugu hizo, wengi ya vijana hao wamekamatwa nje ya Msikiti Musa iliyo eneo la Majengo visiwani Mombasa.
Wakati wa makabiliano hayo polisi walitumia vitoa machozi kuwatawanya waandamanaji waliokuwa na ghadhabu.
Hata hivyo katika eneo moja polisi walilazimika kutumia risasi za mpira kuwatawanya vijana waliokuwa wakiwasha matairi barabarini na kufanya uporaji.
Bwana mmoja alichomwa kisu katika karakana yake na kulazimika kupewa huduma ya kwanza na wafuasi wa dhehebu la Jeshi la wokovu.

Na wakati Mombasa ikiwaka moto, wapiganaji wa Al shabaab wametuma ujumbe katika mtandao wao wakiwasihi waislamu wa Kenya "wachukuwe kila hatua zinazostahili kulinda dini yao"
" Waislamu lazima wachukue sheria mikononi mwao, na wasimame kidete dhidi ya makafiri na kuchukua kila hatua kuilinda dini yao, heshima yao ,mali yao na maisha yao kutoka kwa maadui wa waislamu" , Al shabaab wamenukuliwa wakisema hayo katika taarifa yao.
Kiongozi huyo wa kidini Sheikh Aboud Rogo ,aliyepigwa risasi na kuuwa siku ya jumatatu alikuwa ametajwa na Marekani pamoja na Umoja wa Mataifa kama mtua anayewasajili baadhi ya vijana wa Kenya wkenda kujiunga na wapiganaji wa Al Shabaab.
Sheikh Aboud Rogo pia anadaiwa kuwa alikuwa mfadhili wa kundi hilo la Al shabaab
Chanzo: BBC Swahili.

No comments:

Post a Comment