Tuesday, August 21, 2012

Haya someni ya Dr Kafumu kuvuliwa ubunge...Na Hafidh Kido

Aliekuwa mbunge wa jimbo la Igunga Dr Peter Kafumu (CCM), leo amevuliwa ubunge na mahakama kuu kanda ya Tabora baada ya kushindwa kesi ya madai na mpinzani wake wa Chadema Joseph Kashindye.

Akisoma hukumu hiyo leo hakimu wa mahakama hiyo Mery Shangali alisema amepitia madai yote yapatayo 13 yaliyotolewa na wakili wa upande wa mlalamikaji Professa Abdallah Safari na kuona kuwa kampeni za uchaguzi huo kwa upande wa CCM zilikuwa na vitisho vingi hasa kwa wapiga kura.

Miongoni mwa malalamiko yaliyofkishwa mahakamani hapo na Professa Safari ni lugha za matusi zilizotolewa na makada wa CCM, Rais mstaaf Benjamin Mkapa nae alihusishwa na kutoa ahadi za uongo pamoja na vitisho vilivyotolewa na Waziri wa ujenzi Joseph Magufuli kuwa kama wana Igunga hawataichagua CCM basi ujenzi wa daraja la Mbutuhautafanyika.

Aidha madai mengine yaliyotolewa na wakili Safari ni kile kitendo cha Mbunge wa Tabora Ismail Aden Rage kusimama katika jukwaa akiwa na bastola kiunoni hali hiyo iliashiriwa kama dalili za uvunjifu wa amani na kuwajaza hofu wapiga kura.

Awali Dr Kafumu alimkataa hakimu Mary Shangali kwa madai hawezi kutenda haki kwani kwa kipindi kirefu alikuwa akiwadhalilisha mashahidi wake. Hata hivyo ombi lake hilo halikukubaliwa na matokeo yake siku ya leo saa sita mchana hakimu Shangali ndie alietoa hukumu na kufanya mwisho wa kesi hiyo iliyoanzwa kusikilizwa tangu tarehe 26 Machi, mwaka huu kuisha vibaya kwa upande wa CCM.

Dr Kafumu aliingia madarakani kujaza nafasi ya ubunge iliyoachwa na Rostam Aziz aliekuwa mbunge wa jimbo hilo baada ya kufuata agizo la chama chake cha CCM la kujivua gamba kwa kuachia nafasi zote za uongozi katika chama na serikali kutokana na tuhuma za rushwa.

HAFIDH KIDO
DARE ES SALAAM, TANZANIA
0713 593894/0752 593894
kidojembe@gmail.com
21 August, 2012

  

No comments:

Post a Comment