Wednesday, August 22, 2012

Ndege yaua wanne Maasai Mara Kenya...

Watu wanne wamekufa na wengine wanane kujeruhiwa baada ya ndege moja kuangukaa leo katika mbuga ya taifa ya wanyama ya Maasai Mara, nchini Kenya, moja ya mbuga iliyo kivutio kikubwa cha watalii, Afrika Mashariki.
Afisa kutoka Mamlaka ya Anga nchini Kenya, Mutia Mwandikwa amethibitisha kuanguka kwa ndege hiyo.
Mutinda amesema miongoni mwa waliokufa ni pamoja na watalii wawili kutoka Marekani na marubani wawili wa ndege hiyo, ambao ni raia wa Kenya.
Kwa mujibu wa idara ya polisi ndege hiyo iliyokuwa imebeba watalii ilianguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja mdogo wa ndege wa Ngerende ulioko katika mbuga hiyo ya wanyama ya Maasai Mara.
Miongoni mwa waliojeruhiwa ni pamoja na raia wanne wa Marekani, wawili kutoka kwa jamuhuri ya Czech na wawili kutoka Ujerumani.
Majeruhi hao walisafirishwa kwa ndege nyingine hadi Nairobi ambako wanaendelea kupata matibabu.

No comments:

Post a Comment