Ndugu wananchi;
Imekuwa
ni mazoea yetu kuwa Rais huzungumza na taifa kila mwisho wa mwezi.
Lakini, leo nazungumza nanyi siku saba kabla ya mwisho wa mwezi kwa sababu
maalum. Sababu yenyewe si nyingine bali ni Sensa ya Watu na Makazi
itakayofanyika kwa siku saba kuanzia kesho Jumapili tarehe 26 Agosti, 2012.
Shabaha yangu ni kutaka kuwakumbusha Watanzania wenzangu wote kuhusu wajibu wao
wa kujitokeza kuhesabiwa siku hizo. Naomba kila mmoja wetu ahakikishe
kuwa anakuwepo kuhesabiwa na kujibu maswali yote yatakayoulizwa na makarani wa
sensa kwa ufasaha.
Ndugu
wananchi;
Katika
historia ya nchi yetu, Sensa ya mwaka huu itakuwa ni ya tano tangu Uhuru wa Tanganyika mwaka 1961, Mapinduzi ya Zanzibar ya tarehe 12 Januari, 1964 na kuzaliwa kwa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
tarehe 26 Aprili, 1964. Sensa nyingine zilifanyika mwaka 1967, 1978, 1988
na 2002. Kumbukumbu zinaonesha kuwa kwa upande wa Tanzania Bara
wakati wa ukoloni zilifanyika Sensa mwaka 1910, 1931, 1948 na
1957. Kwa upande wa Zanzibar
wakati wa ukoloni na utawala wa Sultan kulifanyika Sensa mara moja mwaka 1958.
Ndugu
Wananchi;
Ndugu
wananchi;
Pamoja
na umuhimu huo wa jumla wa Sensa kwa maendeleo ya nchi yetu, Sensa ya
mwaka 2012 ina umuhimu wa aina yake. Taarifa zake zitatumika kufuatilia
na kutathmini utekelezaji wa Dira za Taifa za Maendeleo za Tanzania Bara na
Zanzibar; Mkakati wa Kukuza na Kupunguza Umaskini Tanzania Bara (MKUKUTA
II); Mkakati wa Kupunguza Umaskini Zanzibar (MKUZA II); na Mpango wa
Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2011/12 – 2015/16. Vilevile taarifa
zitakazopatikana zitatumika kupima maendeleo ya utekelezaji wa Malengo ya Milenia
(Millenium Development Goals) yaliyowekwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa
mwaka 2000. Kama tujuavyo, itakapofika mwaka
2015 ndicho kilele cha utekelezaji wa Malengo hayo hivyo kujua hatua
tuliyofikia sasa itasaidia kujipanga vizuri katika miaka mitatu iliyosalia.
Ndugu
Wananchi;
Pamoja
na faida hizo, taarifa za Sensa hii zitasaidia kufanikisha zoezi linaloendelea
sasa, la kuwapatia Watanzania vitambulisho vya taifa. Baadhi ya maswali
yatakayoulizwa kwenye Sensa ya Watu na Makazi yatasaidia katika kuhakiki
maombi ya vitambulisho vya taifa. Bila ya shaka sote tunatambua vyema manufaa
ya vitambulisho vya taifa, hivyo basi ndugu yangu, shiriki zoezi la sensa ili
kuirahisishia Serikali kazi ya utoaji wa vitambulisho kwa raia wake.
Ndugu
wananchi;
Shughuli
yoyote kukabiliwa na changamoto mbalimbali ni jambo la kawaida. Lakini,
tofauti na miaka ya nyuma, Sensa ya mwaka huu imekabiliwa na changamoto ambazo
hazijawahi kuwepo. Kuna baadhi ya wenzetu wamekuwa wanafanya jitihada za
makusudi za kutaka kulivuruga zoezi la Sensa nchini. Wamekuwa
wanawashawishi watu wasishiriki kuhesabiwa, kwa sababu ambazo baadhi yake
hazina uhusiano wo wote na Sensa. Zipo sababu nyingine ambazo hata
haziingii akilini. Kwa mfano, wapo watu wanaodai kuwa hawatashiriki Sensa mpaka
mjusi aliyeko kwenye Jumba la Makumbusho kule Berlin , Ujerumani atakaporudishwa.
Kinachozungumzwa hapa ni mabaki ya mifupa ya mnyama wa kale aliyekuwepo hapa
nchini zaidi ya miaka milioni 200 iliyopita. Mwaka 1906 wana sayansi wa
Kijerumani waliyagundua mabaki hayo kule Tendaguru, Lindi, wakayafukua na
kuyapeleka Ujerumani ambako yamehifadhiwa tangu wakati huo.
Ndugu
Wananchi;
Kudai
mifupa hiyo irejeshwe nchini si jambo baya, watu wataona wanyama wa kale
waliokuwepo wakati huo wanafananaje. Huenda pia kikawa kivutio cha
utalii. Hata hivyo, kugeuza kurejeshwa kwa mabaki hayo kuwa sharti la
kushiriki Sensa ni jambo ambalo mantiki yake siielewi. Watu wakisusia
Sensa kwa sababu hiyo itakuwa siyo tu haieleweki wala haielezeki, bali hata
watu wengine nchini na duniani watawashangaa. Lakini, jambo ambalo
ningependa wajiulize ni kuwa hivi hasa wanamsusia nani? Mjerumani au
wanajisusia wenyewe? Hivi kweli mtu uko tayari kuacha manufaa yako ya
maendeleo yapotee au yaathirike kwa sababu ya mjusi ambaye hata akirejeshwa
huna manufaa ya moja kwa moja? Hasara anapata nani sisi au wao?
Nawasihi, Watanzania wenzangu, tusiwasikilize watu wanaoeneza maneno yahusuyo
Mjusi au mambo mengine ya upotoshaji na uvurugaji wa mambo yenye maslahi
makubwa zaidi kwetu binafsi na nchi yetu. Tuachane nao hawatutakii mema
na wala hawaitakii mema nchi yetu. Nawaomba tusitumie vibaya uhuru wa
kutoa maoni.
Ndugu
Wananchi;
Wapo
ndugu zetu wengine wanaotaka liongezwe swali la dini ya mtu katika orodha ya
maswali yatakayoulizwa katika Sensa ya mwaka huu. Wahusika wakuu hasa ni
baadhi ya viongozi na wanaharakati wa Kiislamu. Wao wanasema bila ya swali hilo kuwepo, Waislamu
wasikubali kuhesabiwa. Wamekuwa wanafanya juhudi kubwa ya kuwashawishi
Waislamu wawaunge mkono katika msimamo wao huo. Nimesoma baadhi ya
nyaraka na vipeperushi vyao kuhusu madai hayo. Nilipata pia bahati ya
kukutana na kuzungumza na baadhi ya wanaharakati na viongozi wa harakati
hizo. Nia yangu katika kufanya hayo ilikuwa ni kutaka kuelewa kwa undani
hoja na madai yao .
Yako mambo kadhaa yanayotajwa kama sababu, lakini ukweli ni kwamba jambo
linaloweza kuhusishwa moja kwa moja na Sensa, ni lile la takwimu za idadi ya
Waislamu, Wakristo na Wapagani zilizotolewa na Baraza la Maaskofu Katoliki,
Shirika la Utalii na Shirika la Utangazaji Tanzania .
Hawazikubali
taarifa hizo kwa hoja kwamba, Waislamu hawajawahi kuhesabiwa na watoaji wa
takwimu hizo. Kwa sababu hiyo hawaelewi ni kwa vipi watoe idadi ya kuwa
ni asilimia fulani Watanzania. Hawana ugomvi nao kuhusu takwimu za
Wakristo na Wapagani kwani huenda waliwahesabu. Kwa maoni yao , taarifa hizo si za
kweli na ni upotoshaji unaofanywa maksudi kwa sababu wanazozijua watoaji wa
taarifa hizo. Ili kuondoa upotoshaji
huo, wanaharakati na viongozi hao wa Waislamu wakataka swali la dini liwepo
katika Sensa hii ili ukweli ujulikane.
Katika
mazungumzo yangu na baadhi ya viongozi wa Waislamu niliwaambia kuwa naelewa
sababu na hoja za wao kukasirishwa na kutokuzikubali takwimu hizo. Vile
vile, niliwaeleza kuwa takwimu hizo si za Serikali bali ni za mashirika
hayo. Nilisisitiza kuwa takwimu za Serikali kuhusu idadi ya watu hutolewa
na Ofisi Kuu ya Takwimu na si chombo kingine chochote cha Serikali.
Bahati nzuri Ofisi Kuu ya Takwimu haijatoa takwimu hizo na wala siyo chanzo cha
takwimu zilizotolewa na mashirika hayo. Walikozipata wanajua
wenyewe. Taarifa hizo hazina ithibati yo yote na ndiyo maana
zinatofautiana. Niliwasihi waachane nazo, wazipuuze na wakipenda watoe tamko la
kuzikataa.
Ndugu
Wananchi;
Niliwaambia
pia kuwa kuelekeza lawama kwa Serikali kwa ajili ya taarifa hizo ni kuionea na
kutoitendea haki. Vile vile kuibebesha dhima ya kuongeza swali la
dini ili kuyajibu mashirika hayo ni kuipa mzigo usiostahili. Napenda,
kutumia nafasi hii kuwasihi wale wote wanaotoa takwimu za namna hiyo kutambua
unyeti wake na kuepuka kufanya hivyo. Zinatuletea mifarakano isiyokuwa ya
lazima kama ilivyo sasa.
Ndugu
Wananchi;
Kwa
upande wetu, yaani Serikali, imekuwa vigumu kukubali maombi ya kuliingiza swali
la dini katika Sensa hii kwa sababu za kisera na kiutekelezaji. Wakati wa
ukoloni maswali ya rangi, dini na kabila la mtu yaliulizwa katika Sensa.
Baada ya uhuru, maswali hayo yaliulizwa katika Sensa ya kwanza ya mwaka 1967
kwa vile ilikuwa bado inafuata misingi ya kikoloni. Baada ya hapo
ulifanyika uamuzi wa kisera wa kutokuuliza maswali hayo kwani nia ya wakoloni
kuuliza maswali yale ilikuwa ni kwa sababu ya sera yao ya wagawe uwatawale. Walitoa huduma
kwa ubaguzi, sera ambayo Serikali zetu ziliachana nayo baada ya Uhuru na
Mapinduzi. Huduma hazikuwa zinatolewa kwa ubaguzi wa rangi, kabila wala
dini, bali kwa msingi wa haki ya uraia na ubinadamu wake.
Ndugu
Wananchi;
Sera
hiyo pia ilikuwa na lengo la kudumisha umoja na mshikamano wa taifa letu na
watu wake. Badala ya watu kubishana juu ya watu wa dini ipi ni wengi na
hivyo kufarakana kwa kutokubaliana na takwimu zilizotolewa, sera mpya inawataka
watu wajivunie uwingi wao kama Watanzania.
Ndugu
Wananchi;
Nionavyo
mimi Sera hii ni nzuri na kwamba ulikuwa ni uamuzi wa busara na hekima kubwa.
Tuendelee kuidumisha na kuienzi. Kufanya vinginevyo, na hasa
kuingiza sera ya kutoa huduma kwa misingi ya dini zetu ni kuliingiza
taifa letu ambalo lina sifa ya amani, upendo na utulivu, katika migogoro
isiyokuwa ya lazima. Ni migogoro inayoweza kuepukika kwa kuenzi na
kudumisha sera yetu hii nzuri na sahihi.
Ndugu
Wananchi;
Sababu
ya pili inayotupa ugumu kiserikali ni ya kiutekelezaji. Imechukua miaka
kadhaa ya maandalizi mpaka kufikia hatua hii ya sasa ya kuwa tayari kutekeleza
zoezi la Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Isitoshe Sensa ya
majaribio imeshafanyika kwa kutumia vifaa, madodoso na maswali yaliyopo na
marekebisho kufanywa baada ya hapo. Kuingiza mambo au jambo jipya sasa
itakuwa viguku kiutekelezaji. Kutachelewesha zoezi zima na kusababisha
hasara kubwa kwa taifa.
Kwa
vile watu wote hawataulizwa swali la dini na kwa kuwa dini si kigezo cha kutoa
huduma kwa wananchi, hakuna ulazima wa kusisitiza swali hilo liwepo. Napenda kuwasihi ndugu zangu
wanaokereketwa na jambo hili waache kuling’ang’ania na badala yake wajitokeze
kuhesabiwa. Tujitokeze kuhesabiwa ili na Waislamu nao wawemo katika idadi ya
wananchi wa Tanzania .
Ndugu
Wananchi;
Sioni
ulazima wa kuunda Tume Huru ya Sensa yenye uwakilishi sawa wa Wakristo na
Waislamu. Tangu mwaka 1931 kazi ya Sensa imekuwa inafanywa na Ofisi Kuu
ya Takwimu nchini na ndipo ujuzi na maarifa yote yapo. Hata ukiamua uiite
Tume bado utawatumia watu hao hao, hivyo mabadiliko hayo hayana sababu.
Vile vile, sioni haja ya kuwa na mgao wa wafanyakazi wake kwa msingi wa dini
kwa sababu Sensa siyo kwa ajili ya kujua Wakristo na Waislamu.
Huduma hazitolewi kwa misingi ya dini za watu.
Ndugu
Wananchi;
Katika
maelezo yao
kwangu, hivi karibuni Kamishna wa Sensa, Hajat Amina Mrisho Said na Mtakwimu
Mkuu wa Serikali ya Muungano, Mama Albina Chuwa walinieleza kwamba kwa kawaida
katikati ya Sensa moja na nyingine, hufanyika utafiti wa kidemografia, yaani
Demographic Survey. Huu ni utafiti wa kina unaofanywa katika ngazi ya
kaya ambapo taarifa za mambo mengi yahusuyo watu ambazo hazikusanywi, katika Sensa
hukusanywa. Mara ya mwisho utafiti huo kufanyika ilikuwa mwaka 1973,
yaani baada ya Sensa ya mwaka 1967 na kabla ya ile ya mwaka 1978. Ni
makusudio ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu kuanzisha tena utaratibu huo mwaka 2016
ambapo baadhi ya masuala yaliyoachwa yanaweza kujumuishwa. Subira yavuta
heri.
Ndugu
Wananchi;
Nimehakikishiwa
na mamlaka zinazohusika kuwa maandalizi ya sensa yamefikia hatua nzuri na zoezi
liko tayari kuanza siku ya Jumapili, tarehe 26 Agosti, 2012. Lakini, mafanikio
ya zoezi lenyewe yatategemea sana
ushiriki wa watu ambao ndiyo walengwa na wadau wengine.
Naomba nitumie fursa hii kuwataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya na Wenyeviti na
Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Wilaya na Miji na wadau wengine wa
kisiasa na kiutendaji wa ngazi mbalimbali waendelee kusimamia utekelezaji
wa shughuli zote za Sensa katika maeneo yao ya uongozi. Hawana budi
kuhakikisha kuwa zoezi linakuwa na mafanikio makubwa. Wale wote
wanaofanya vitendo vya kuvuruga zoezi hili wachukuliwe hatua stahiki za kisheria.
Nawaomba
viongozi wa kisiasa na kijamii nao waendelee kuwahamasisha na kuwaelimisha
wananchi kuhusu umuhimu wa kujitokeza kuhesabiwa na kushirikiana na Makarani wa
Sensa watakapokuwa wanafanya kazi yao .
Wakumbusheni kukataa kuwasikiliza au kuwafuata watu wanaowashawishi
wasijitokeze kuhesabiwa. Watu hao si wema wao na wala hawaitakii mema
nchi yetu.
Ndugu
wananchi;
Nitakuwa
mwizi wa fadhila kama sitawapongeza Hajat Amina Mrisho Said, Kamishna wa Sensa
wa Tanzania Bara na Ndugu Mwalim Ameir, Kamisaa wa Sensa Zanzibar kwa kazi
kubwa na nzuri wanayoendelea kuifanya ya kutoa uongozi wa kisiasa, kusimamia na
kuratibu zoezi la Sensa nchini. Nawapongeza pia Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya
Taifa ya Takwimu na Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar pamoja na
watendaji wengine wa Sensa katika ngazi mbalimbali katika Mikoa, Wilaya,
Majimbo, Tarafa, Kata, Mitaa, Vijiji na Shehia kwa kazi nzuri ya
matayarisho na uendeshaji wa Sensa ya mwaka 2012. Nawatakia mafanikio
mema katika kazi hii muhimu na adhimu kwa nchi yetu na watu wake.
Ndugu
zangu, Watanzania wenzangu, nawaomba sote tuwaunge mkono ndugu zetu hawa kwa
kushiriki katika zoezi la Sensa kuanzia siku ya Jumapili tarehe 26 Agosti,
2012. Haya shime sote tujitokeze kuhesabiwa kwani kujitokeza kwetu ndiyo
ukamilifu na mafanikio ya Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012. Ewe
Mtanzania mwenzangu shiriki Sensa kwa maendeleo yako na ya taifa
letu.
Mungu
Ibariki Tanzania !
Mungu
Ibariki Afrika!
Asanteni
kwa kunisikiliza
No comments:
Post a Comment