Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)
kinapinga kauli za Serikali, Jeshi la Polisi na Chama Cha Mapinduzi (CCM) zenye kulipotosha taifa kuhusu mashambulizi na mauji yanayoelezwa kufanywa na askari Mkoani Morogoro na badala yake kinataka uchunguzi huru ufanyike haraka kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act).
Kauli zilizotolewa na
Waziri wa Mambo ya Ndani zina mwelekeo wa kulilinda Jeshi la Polisi ambalo
askari na maofisa wake ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji, badala ya kuwezesha
ukweli kuthibitika na hatua kuchukuliwa kwa wahusika.
Hivyokutokana na
kujirudiarudia kwa mauaji yanayofanywa na vyombo vya dola CHADEMA kinatoa mwito
kwa Rais Jakaya Kikwete ambaye kwa mujibu wa katiba ibara ya 33 ni mkuu wa
nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu aingilie na kuwezesha uchunguzi
wa kina.
Ikumbukwe kwamba tarehe
27 Agosti 2012 Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro lilifyatua risasi za moto na
kupiga mabomu ya machozi wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa
wamejikusanya kwa ajili ya kuelekea kwenye mkutano halali wa CHADEMA na wengine
waliokuwa wakiendelea na shughuli zao eneo la Msamvu, hivyo kusababisha kifo
cha raia mmoja asiye na hatia na kujeruhi wengine wawili.
CHADEMA kinaukumbusha
umma kwamba kwa mauaji hayo na mengine katika maeneo mbalimbali nchini serikali
inayoongozwa na CCM kupitia vyombo vya dola inaendelea kukiuka Ibara ya 14 ya
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo inatambua kwamba
uhai ni haki ya msingi kwa raia wote.
CHADEMA hakikubaliani na
hatua zilizochukuliwa na Serikali mpaka sasa kuhusu tukio husika pamoja na
maelezo yaliyotolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani tarehe 28 Agosti 2012 ambayo
kwa sehemu kubwa yametokana na taarifa zisizo za kweli kutoka kwa maofisa wa
Jeshi la Polisi ambao ni sehemu ya watuhumiwa wa mauaji husika.
CHADEMA haina imani na
timu iliyoundwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi kuchunguza tuhuma za askari kufyatua
risasi na mabomu ya machozi na kusababisha mauaji kwa kuwa tayari serikali na
Jeshi la Polisi wametoa maelezo yenye kutofautiana kwa kiwango kikubwa na
maelezo ya mashuhuda waliokuwepo na ushahidi wa picha za eneo la tukio.
Wakati Serikali na Jeshi
la Polisi wakitoa maelezo kuwa marehemu alikutwa umbali wa mita 300 na
kupelekwa hospitali na wasamaria wema, mashuhuda wameeleza wazi kuwa askari
walifika jirani na eneo lake na ofisa mmoja akaonyesha ishara na ndipo risasi
za moto na mabomu ya machozi yakafyatuliwa mojawapo kumpata marehemu na
kudondoka.
Mashuhuda wote waliohojiwa
wanaeleza kwamba bunduki ya polisi ndiyo ilielekezwa na kufyatuliwa kwa
marehemu, maelezo pekee yanayotofautiana ni kuwa baadhi wameeleza kuwa ni
bunduki ya risasi za moto na wengine wa wameeleza kuwa ni bunduki ya kufyatulia
mabomu ya machozi.
Mara baada ya kudondoka
gari hilo liliondoka na gari lingine la polisi lilifika likiongozwa na Kamanda
wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia cha Mkoa ambaye alitoa amri ya gari lingine
kumbeba Ali Hassan Singano (Zona) na kuondoka naye, hivyo si kweli kwamba matukio
hayo yalitokea mbali na eneo bali pembeni ya meza ya muuza magazeti huyo karibu
na barabara ya kwenda Iringa eneo ambalo polisi ilikuwa ikifanya mashambulizi.
Kauli zilizotolewa na
Serikali kuwa Jeshi la Polisi lilizuia maandamano ya CHADEMA yaliyopangwa
kufanyika Mkoani Morogoro kwa sababu ya sensa ya watu na makazi si za kweli kwa
kuwa sababu pekee zilizotolewa ni ufinyu wa barabara na kuwa maandamano
yalipangwa siku ya kazi. Ushahidi wa suala hili ni barua ya Jeshi la Polisi
lenyewe ya 23 Agosti 2012 yenye Kumb. Na. MOR/A.25/1/VOL. II/202.
CHADEMA kinaujulisha
umma kwamba Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro ndilo lililoacha kuheshimu utawala
wa sheria na makubaliano yaliyofikiwa baada ya mazungumzo yaliyohusisha kikosi
kutoka Makao Makuu ya Jeshi la Polisi kikiongozwa na Kamanda wa Operesheni za
Jeshi hilo
Simon Siro na hivyo kuwa chanzo cha mauaji yaliyotokea na madhara mengine kwa
wananchi waliokuwepo maeneo yaliyorushiwa mabomu ya machozi.
Ikumbukwe kwamba awali
CHADEMA kilipanga kufanya maandamano na mikutano katika Jimbo la Morogoro Mjini
tarehe 4 Agosti 2012 na kuwasilisha taarifa kwa Jeshi la Polisi kwa mujibu wa
sheria.
Hata hivyo, Polisi
wakakataa kufanyika kwa maandamano na mikutano kwa kisingizio cha Sikukuu ya
Nanenane, mgomo wa walimu na ratiba kugongana na ile ya mikutano ya CCM, sababu
ambazo zilibainika kwamba hazikuwa na msingi wowote.
Baada ya mvutano na
mazungumzo CHADEMA ilikubali kutii sheria na kuzingatia matakwa ya Jeshi la
Polisi pamoja na kuwa yalitolewa kinyume cha Sheria kwamba maandamano na
mkutano wa CHADEMA vifanyike mara baada ya siku ya kuanza kwa sensa tarehe 26
Agosti 2012 na CHADEMA ilipendekeza tarehe 27 Agosti 2012 ambayo Jeshi la
Polisi liliikubali.
Polisi walifanya hivyo
wakielewa ukubwa wa barabara za Morogoro na pia wakitambua kwamba ilikuwa ni
siku ya kazi, hata hivyo tarehe 23 Agosti 2012 Jeshi la Polisi liliandika barua
ya kueleza kwamba limetoa kibali cha mkutano (suala ambalo si mamlaka yake
kisheria) na pia limekataza maandamano.
CHADEMA kikaamua kwa
mara nyingine tena kurudi katika meza ya mazungumzo na Jeshi la Polisi Mkoa wa
Morogoro, tarehe 24 Agosti 2012 ambapo polisi ilikubali maandamano ikiwemo ya
watembea kwa miguu na kupendekeza njia mbadala na tarehe 26 Agosti 2012
mazungumzo yakaendelea kwa lengo la kukagua barabara.
Hata hivyo, kufuatia
shinikizo la Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro Faustine Shilogile kinyume
na Sheria ya Jeshi la Polisi ambayo imetoa mamlaka kwa Mkuu wa Polisi Wilaya
kuhusu taarifa za mikutano, polisi ikarejea katika msimamo wa kukataza mapokezi
ya watembea kwa miguu na badala yake tarehe 26 Agosti 2012 bila sababu za
misingi ya kisheria na zisizozingatia haki za kikatiba ikapendekeza kwamba
yafanyike mapokezi kwa kutumia magari.
Maelezo ya Waziri wa
Mambo ya Ndani kuwa iwapo vyama vya siasa visiporidhika na mazingira kama hayo yapo mamlaka ya kukata rufaa yanapotosha kwa
kuwa Sheria ya Jeshi la Polisi na Sheria ya Vyama vya Siasa hazijaweka
utaratibu wa rufaa hivyo njia pekee ya kisheria ni kutumia mahakama.
Jeshi la Polisi lingeheshimu
utawala wa sheria na mazungumzo lingeruhusu CHADEMA ifanye maandamano na kutoa
ulinzi mpaka eneo la mkutano kwa muda mfupi badala yake jeshi hilo likaamua
kutumia nguvu kubwa na kusababisha mauaji, barabara kufungwa kwa muda mrefu na
kuathiri wananchi waliokuwa wakiendelea na kazi zao.
Iwapo wanachama na
wananchi waliokuwa wamekusanyika kuwapokea viongozi na kuelekea kwenye mkutano
wangekuwa wamekiuka sheria Jeshi la Polisi lingeweza kuwakamata kwa mujibu wa
sheria, hata hivyo hakuna kiongozi yoyote wa CHADEMA aliyefunguliwa jalada
mpaka sasa katika kituo chochote cha polisi kwa kudaiwa kukiuka sheria.
Kinyume chake Jeshi la
Polisi ambalo likiwa kwenye mazungumzo lilikubali kuwa mapokezi yafanyike kwa
msafara wa vyombo vya moto, lakini tarehe 27 Agosti 2012 likaamua kupiga mabomu
ya machozi kwa wananchi na wanachama wa CHADEMA waliokuwa wamekusanyika eneo la
Msamvu wakiwasubiri viongozi bila hata ya kusubiri kuona iwapo yangefanyika
matembezi ya miguu kuelekea eneo la mkutano au maandamano ya magari na vyombo
vingine vya usafiri.
Kitendo cha Jeshi la
Polisi kutumia nguvu kubwa kinyume cha sheria na kusababisha mauaji na kufunga
barabara kwa muda mrefu kiliwafanya wanachama wa CHADEMA na wananchi kwa ujumla
kutawanyika kuelekea eneo la mkutano na wengine kuingia barabarani kutembea
kuelekea eneo la mkutano na hatimaye polisi walipoona wamesababisha hali hiyo
wakaamua kulinda misafara hiyo mpaka eneo la mkutano hali inayodhihirisha kuwa
uamuzi kama huo ungechukuliwa kutoka mwanzo yasingetokea madhara yoyote.
Kwa kuzingatia utofauti
mkubwa baina ya maelezo yanayotolewa na Serikali na Jeshi la Polisi kuhusu
matukio husika na ukweli halisi ulivyotokea, CHADEMA kinasisitiza kuwauchunguzi
huru ufanyike kwa mujibu wa Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) Sura ya
24 ya Sheria za Tanzania .
CHADEMA kwa mara
nyingine kinaitaka Serikali inayoongozwa na CCM kurejea katika kifungu cha 3
cha Sheria ya Uchunguzi wa Vifo, ambacho kinatoa mamlaka ya Waziri mwenye
dhamana na masuala ya Sheria kuanzisha Mahakama ya Kuchunguza Vifo hivyo
(Coroner’s Court) katika maeneo ya serikali za mitaa kwa kushirikiana na Jaji
Kiongozi.
CHADEMA kinaikumbusha
Serikali kuwa, kufuatia kauli ya Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na
Mawaziri Vivuli husika kueleza bungeni taarifa za mauaji yaliyofanywa na vyombo
vya dola kwa nyakati mbalimbali, Waziri Mkuu na Mawaziri wengine waliahidi
bungeni kwamba sheria hiyo itaanza kutumika kuchunguza vifo vyenye utata.
Katika muktadha huo
uchunguzi wa kifo cha Ali Zona haupaswi kufanywa na timu ya polisi bali sheria
hiyo sasa ianze kutumika.
Kwa upande mwingine,
CHADEMA imeheshimu taratibu za maziko zilizopangwa na familia ambapo mwili wa
marehemu ulisafirishwa jana tarehe 28 Agosti 2012 kwenda Mkoani Tanga kwa ajili
ya maziko na CHADEMA kuwasilisha rambirambi zake za awali, taarifa zaidi kuhusu
ushiriki kwa CHADEMA kwenye maziko zitaelezwa baada ya majadiliano
yanayoendelea na familia.
CHADEMA kwa kuheshimu
mazungumzo na utawala wa sheria kwa mara nyingine tena tarehe 28 Agosti 2012 CHADEMA
kimesitisha Operesheni za Maandamano na Mikutano yake ya Vuguvugu la Mabadiliko
(M4C) kwa rai iliyotolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) ili kupisha
kukamilika kwa zoezi la sensa ambayo imetokana pia na maelezo ya mamlaka
zingine za kiserikali.
CHADEMA inatambua kwamba
wakati maandamano ya CHADEMA yametolewa rai kuwa yasitishwe kupisha sensa,
maandamano ya wagombea wa CCM kurudisha fomu za uchaguzi wa ndani ya chama chao
yameachwa yakiendelea katika barabara kadhaa nchini bila kusitishwa kwa kisingizio
hicho.
Aidha, wakati CHADEMA
ikiheshimu mazungumzo na kusogeza ratiba yake mbele ya tarehe 26 Agosti 2012
mpaka tarehe 27 Agosti 2012 kupisha sensa hatua ambayo ilifanywa pia na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba, ambayo ilitangaza ratiba yake kuendelea baaada ya tarehe
hiyo.
Tume hiyo inaendelea na
mikutano yake ya hadhara inayokutanisha wananchi katika kata za mikoa
mbalimbali wakati huo huo zoezi la sensa likiendelea lakini kwa mikutano ya
CHADEMA inaonekana kufanyika kwake ni kuingilia sensa.
CHADEMA inataka Serikali
na Polisi kueleza iwapo matukio haya na mengine hayana mwelekeo wa ubaguzi na
uhujumu wa vuguvuvugu la mabadiliko linaloendelea nchini kwa kurejea ukweli
kuwa maisha ya wachache yanaweza kuwekwa mashakani lakini si mabadiliko kwa
maslahi ya wengi.
CHADEMA itaeleza hatua
za ziada itakazochukua baada ya kupata ripoti ya uchunguzi wa mwili wa marehemu
(post mortem) uliofanyika tarehe 28 Agosti 2012 na uamuzi wa Serikali kukubali
au kukataa mwito wa kutumia Sheria ya Uchunguzi wa Vifo (Inquest Act) kuwezesha
uchunguzi huru.
Imetolewa tarehe 29
Agosti 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi
No comments:
Post a Comment