Friday, September 7, 2012

Sudan bado ina matatizo ya mipika...



Balozi wa Marekani katika umoja wa mataifa Susan Rice, amesema mzozo kuhusu mpaka kati ya Sudan na Sudan Kusini huenda ukasababisha vita kuzuka tena kati ya nchi hizo mbili.
Bi Rice ametoa matamshi yake katika mkutano wa baraza la usalama la umoja wa mataifa kuhusu mzozo wa mpaka kati ya nchi hizo nchini Marekani.
Sudan Kusini imekubali mpango wa amani uliopendekezwa na Muungano wa nchi za Afrika ingawa Sudan imeukataa.
Nchi hizo mbili nusura zipigane mapema mwaka huu sababu kuu ikiwa mzozo wa mpaka na ugawanaji wa mapato ya mafuta .
Sudan Kusini ilipata uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka jana na kumaliza miaka mingi ya mapigano kati yake na Sudan.
Akiongea mjini New York, Bi Rice alisema kuwa hatua ya serikali ya Khartoum kukataa kusaini mpango wa amani inaweka nchi hizo katika hatari ya kurejelea vita.
Alisisitiza kuwa hatua ya kujikokota ya Khartoum inazua wasiwasi kuhusu kujitolea kwake kutatua mzozo huo.
Licha ya Sudan Kusini kukubali mpango wa amani, Bi Rice amekariri kuwa Marekani ina wasiwasi kwamba nchi hizo hazichukulii kwa uzito swala hilo kama ambalo linapaswa kushughulikiwa kwa dharura.
Muda wa mwisho uliowekwa na Umoja wa mataifa wa kuafikia makubaliano mwezi Agosti tarehe mbili, haukuweza kufikiwa na nchi hizo mbili.
Hata hivyo, pande hizo mbili zinashinikizwa kutia saini mpango huo wa amani ifikapo tarehe 22 mwezi Septemba.
Mwezi jana serikali za Khartoum na Juba zilifanya mkutano wa wiki tatu mjini Addis Ababa, Ethiopia.
Kwenye mazungumzo hayo, mwafaka ulifikiwa wa kugawana mapato ya mauzo ya mafuta ingawa bado mazungumzo zaidi yanahitajika kuhusu usalama.
Mazungumzo hayo yataendelea mwishoni mwa mwezi Agosti.
Majeshi ya Sudan yamepigana mara kadhaa na yale ya Sudan kusini tangu Sudan kusini kujipatia uhuru mwaka jana.
Huenda baraza la usalama la umoja wa mataifa likaziwekea vikwazo nchi hizo iwapo zitashindwa kukubaliana kusitisha mzozo huo katika eneo la mpakani.
Chanzo: BBC Swahili.

No comments:

Post a Comment