Tuesday, September 4, 2012

Waziri wa mazingira asisitiza watanzania wasilale...


Na Hafidh Kido

Tanzania inategemea kuongeza fursa za uwekezaji katika sekta za utalii, biashara na ongezeko la kodi kutokana na wageni watakaoitembelea kutazama vivutio mara baada ya kuisha mkutano wa mawaziri wa mazingira wa nchi za Afrika mjini Arusha.

Akizungumza leo katika ofisi ya makamu wa Rais juu ya mkutano huo utakaoanza tarehe 10 mpaka 14 mwezi huu mjini Arusha ambao utashirikisha mawaziri wa mazingira barani Afrika, Dk Terezya Luoga ambae ni waziri wa nchi ofisi ya makamu wa Rais Mazingira alisema Tanzania itakuwa mwenyekiti wa mkutano wa mwaka huu hivyo watanzania wote wachangamkie fursa hiyo kujipatia faida.

“Tanzania itakuwa mwenyekiti wa wa mkutano huu, ambao unatarajiwa kuwa na wajumbe  wapatao 350, idadi hiyo inahusisha washiriki kutoka nchi zote za bara la Afrika na baadhi kutoka mashirika ya umoja wa mataifa na umoja wa Afrika.

“Faida ilizopata Tanzania kutoka Baraza la Mawaziri wa Mazingira wa Nchi za Afrika (AMCEN) tangu ianzishwe ni pamoja na miradi mingi iliyohusu uhifadhi wa mazingira ya muda mfupi na muda mrefu, kwa pamoja imegharimu takriban dola za Kimarekani milioni 11.6,” alisema Dk Luoga.

Aidha aliongeza kuwa kwa nchi ya Tanzania kupata uenyekiti wa AMCEN kwa miaka miwili imechochea kasi ya kuongeza fursa za upatikanaji fedha zitakazoshughulikia changamoto za mazingira, uwezekano wa kupitisha miradi itakayoinufaisha Tanzania, kuwa na maamuzi ya juu katika baraza hilo hasa kwa mambo yanayoigusa nchi na kukuza mashirikiano na nchi nyingine za kiafrika ambazo zina uwezo kitaalamu na kifedha juu ya kuondoa tatizo la mazingira nchini.

AMCEN ilianza mwaka 1985 kwa lengo la kusimamia masuala ya hifadhi ya mazingira katika bara la Afrika na kuhakikisha mahitaji ya msingi ya binadamu yanapatikana kwa njia endelevu kwa kizazi cha sasa na kijacho.

HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
04/09/2012


No comments:

Post a Comment