Jengo hili la Nkrumah, usipofika hapa ujue hujafika chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ni nyumba maarufu ya mikutano ya kitaaluma hasa kigoda cha taaluma cha Mwalimu Nyerere.
Hizo ni picha za wakuu wa chuo hiki tangu miaka ya sitini, sikuwahi kujua kuwa hata aliekuwa Spika wa Bunge la Tanzania Pius Msekwa alikuwa makamu mkuu wa chuo hicho Katika mwaka 1970-77.
Chini ya mti huu maarufu Mdigirii (Degree) wanafunzi wote wanaosoma chuo hiki kwa taaluma yoyote lazima waliwahi kujisomea kwa wakati mmoja ama mwingine. Ndipo ukabatizwa jina la utani Mdigirii kwa maana umesaidia kupatikana shahada za wanafunzi wengi.
Ni kweli ukiingia eneo la chuo kuna ukimya wa hali ya juu na hata watu unaopishana nao wanaongea kisomi.
Kumbe Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam kuna mifugo pia?
Nilifurahi nilipofika na kuona ofisi za kigoda cha taaluma cha Mwalimu nyerere, watu wanatoka nchi mbalimbali Duniani kuja kutembelea ofisi hizi hasa katika mikutano yake iliyo chini ya Professa Issa Shivji. nami nilifurahi kuwa miongoni mwao leo.
Hivi ndivyo vitabu viwili nilivyovinunnua leo na kuongeza idadi ya vitabu katika maktaba yangu ndogo nyumbani.
Ndugu zangu,
Leo niliamua tu kutembelea
kituo cha taaluma Tanzania ,
Afrika na Dunia kwa ujumla; Chuo kikuu cha Dar es Salaam .
Safari yangu ilianzia kwa
afisa uhusiano chuoni hapo ndugu Jackson Isdory, ambae nilikuwa na ahadi ya
kukutana nae kuzungumza kuhusu mambo ya kiuanahabari. Siku za nyuma niliwahi
kutoa habari ya kisayansi inayohusiana na mazao ya nyama na chakula
yanayozalishwa kwa kutumia utaalamu wa kisasa Genetic Modified Organism (GMO).
Alivutiwa na makala yale
katika gazeti la Raia Mwema, hivyo alitaka kuiboresha zaidi na kunitaka nifike
ofisini kwake ili apate kunikutanisha na wataalamu wa sayansi ya kilimo na
chakula ndipo nikaenda leo na kufanya nae mazungumzo.
Baada ya hapo nikaamua kuenda
kumtembelea rafiki yangu wa siku nyingi, aliepata kuwa mwenyekiti wa Taasisi ya
utafiti na kukuza Kiswahili (TUKI). Profesa Mulokozi, lakini sikufanikiwa
kumkuta.
Hivyo nikaamua kununua baadhi
ya machapisho na kuondoka. Ila kwakuwa nilikwenda katika taasisi ya kitaaluma
sikubweteka bali nikaamua kutafuta baadhi ya mambo mengine ya kufanya.
Nikatembelea taasisi ya
mazingira Stockholm Environmental Institute (SEI), nikakutana na Dr Victor Kongo,
alie katika kitengo cha utafiti. Tulizungumza mambo mengi sana kuhusu mazingira. Kwa maana nataka
kutembelea vijijini kuangalia tatizo la maji na uharibifu wa mazingira.
Kama nilivyoandika katika
utambulisho wa blogu hii ya Kidojembe, nitaangazia sana matatizo ya vijijini. Hivyo nilitaka
mwanga kuhusiana na tatizo la maji na mazingira katika vijiji vyetu. Amenisaidia
sana Dr Victor,
na naahidi nitarudi kuongeza taaluma zaidi.
Kitu kingine nilichojifunza
katika ziara yangu ya leo ni mazingira tulivu na yenye kuvutia ya chuo hicho kilichoanziswa
mwanzoni mwa miaka ya sitini mara baada ya uhuru.
Kadhalika tatizo la lugha
bado linasumbua hasa kwa wanafunzi wa kike, wengi wanazungumza swanglish. Yaani
wanachanganya lugha ya kiingereza na Kiswahili, ama wanazungumza Kiswahili kwa
lafudhi ya kizungu. Hatari ni kubwa kuliko unavyofikiri watoto wa kitanzania
wanazungumza Kiswahili kwa mikogo utadhani ni wageni. Aibu kubwa hii.
Angalizo, sipingi watanzania
kujifunza lugha za kigeni bali nataka mtu anapoamua kuzungumza kichina ama
kizungu basi azungumze kwa ufasaha wake bila kuchanganya lugha nyingine. Na
anapozungumza lugha ya nyumbani iwe kichaga, kisukuma ama Kiswahili basi afanye
hivyo kwa lafudhi zilizokubalika na bila kuchanganya maneno ya lugha za kigeni.
Vitabu hivyo ni ‘Kasri ya
Mwinyi Fuad’ kilichoandikwa na Shafi Adam Shafi, pamoja na ‘Masimulizi ya
Thabit Kombo Jecha’ kilichoandikwa na Mama Minael-Hosanna O. Mdundo.
Ni vitabu ambavyo vinauzwa
kwa bei ndogo sana
ya Tsh 4500/= kila kimoja, wanapunguza bei ili kuongeza kasi ya usomaji vitabu.
Huu ni mjadala mwingine ambao nitakuja kuuzungumzia siku nyingine.
Namshukuru Mungu kwa kila
hatua ninayoipiga katika kutimiza ndoto yangu kuimarisha blogu hii ya kijamii,
jiandae kupata picha na habari zinazohusu mazingira vijijini na kuangazia
matatizo ya maji na athari za tabia nchi.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM , TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
03/09/2012
No comments:
Post a Comment