Kaimu Mkurugenzi Mamlaka ya Usafiri wa
Baharini Zanzibar Abdullah Husein Kombo wakati
alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari Afisini kwake leo Malindi Mjini Zanzibar .
Na Faki Mjaka-Maelezo Zanzibar
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar
imezifutia rasmi hati ya kufanya kazi Meli ya Mv.Kalama, Mv.Seagul na
Mv.Sepideh kutokana na meli hizo kutokukidhi hali ya usalama wa abiria katika
meli hizo.
Aidha meli hizo zimepewa muda wa mwezi
mmoja kuanzia leo kuhakikisha zimeondoka katika maeneo ya Zanzibar kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa
dhidi ya wamiliki wa Meli hizo.
Kauli hiyo imetolewa na Kaimu Mkurugenzi
Mamlaka ya Usafiri wa Baharini Zanzibar Abdullah Husein Kombo wakati alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari Afisini kwake kuhusu hali ya usafiri wa
baharini na usalama Zanzibar .
Amesema Mamlaka hiyo imefanya tathmini na
uhakiki wa kutosha na kujiridhisha kuwa Meli hizo hazifai kufanya kazi katika
maeneo ya Zanzibar
jambo ambalo limepelekea kuchukua hatua za kufuta hati za kufanyia kazi meli
hizo.
Amefahamisha kuwa sababu kuu zilizopelekea
Mamlaka kufanya maamuzi hayo ni pamoja na uchakavu,umri wa meli hizo kuwa mrefu
na kupata matatizo mara kwa mara katika safari zao.
Kombo amefahamisha kuwa Sheria ya Mamlaka
ya Usafiri na Bandari Zanzibar
ya mwaka 2006 kifungu cha 17.1 inampa mamlaka Msajili wa Meli kuifuta meli
yoyote ambayo itakuwa haikidhi usalama wa abiria.
Kufuatia sheria hiyo Kombo amesema
watawataka wamiliki wa Meli hizo kuzirudisha hati za kufanyia kazi meli hizo
ili waende kutafuta sehemu nyengine za usajili kinyume na maeneo ya Zanzibar .
Akizungumzia Meli ya Mv.Serengeti Kombo
amesema wamelazimika kuiagiza meli hiyo kupunguza idadi ya abiria kutoka watu
800 hadi 350 na tani za mizigo kutoka 100 hadi 50 hadi pale ambapo
watajiridhisha kutokana na hali ya meli hiyo ilivyo.
Aidha amegusia kuwa Kampuni ya Bakhresa
italeta Meli kubwa ya abiria itakayofanya kazi zake Zanzibar
ambapo pia Serikali ya Mapinduzi nayo iko mbioni kuhakikisha wanaleta meli
inayokidhi mahitaji ya wananchi wa Zanzibar .
No comments:
Post a Comment