Tuesday, July 31, 2012

CCM yamjia juu Tundu Lissu.


Na Hafidh Kido

Katibu wa itikadi na uenezi chama cha mapinduzi (CCM) Nape Nnauye, amemtaka mnadhimu mkuu wa kambi ya upinzani bungeni na mbunge wa Singida Mashariki (chadema) Tundu Lissu, kuacha kuingilia shughuli za kamati zilizoundwa kufuatilia suala la wabunge wanaohusishwa na rushwa kutoka shirika la umeme nchini TANESCO.

Akizungumza jijini Dar es Salaam leo asubuhi Nape alisema anasikitishwa na kitendo cha Lissu, kutaja majina ya wabunge wanaotuhumiwa kwa rushwa katika sakata hilo lakini cha kusikitisha ametaja majina mengi ya wabunge wa CCM wakati wapo wabunge wa vyama vya upinzani ambapo watanzania wanawatajataja kila siku.

“Si kitendo cha kizalendo hata kidogo kuanza kutaja wabunge wanaohusishwa na rushwa hii, tena cha kusikitisha wabunge wengi wametajwa kutoka chama changu. Wapo wabunge kutoka upinzani ambao wanatajwa tena wengi ni wa chadema, mbona sisi hatuwataji,” alihoji Nape.

Aidha katibu huyo wa itikadi na uenezi alifafanua kuwa ni vema kazi hiyo wakaachiwa kamati zilizopangwa na kama wapo watu aina ya kina Tundu Lissu, ambao wanazo taarifa za kutosha waende kuzisaidia kamati hizo ili kupatikana watuhumiwa hawa maana sisi tunalaani vitendo vya rushwa.

“Wakati ukifika kina Lissu wataitwa kutoa ushahidi, lakini kwa sasa tunalaani kila anaetaka kuhujumu shughuli hii ya kuwahoji watuhumiwa wa rushwa. Maana rushwa inayomgusa kiongozi wa umma hiyo inakuwa zaidi ya rushwa, ni hujuma dhidi ya uchumi wetu,” alisisitiza.

Wakati akijibu maswali ya waandisi wa habari Nape alieleza kuwa iwapo wabunge wa CCM watakutwa na hatia chama kitawafutia uanachama maana huo ndiwo utaratibu wa chama chao kawaida hakilindi wala rushwa.

“Unajua watu wanadhani sisi tunakumbatia wala rushwa, nataka kuwahakikishia kuwa CCM ndiyo chama kinachoongoza kutimua wanachama wake walihusishwa na rushwa. Nawaahidi iwapo mbunge wa chama changu atabainika kuhusika kufanya biashara na TANESCO ama kula rushwa kinyume na taratibu tutamfutia uanachama maana hiyo ipo wazi hata katika kanuni zetu tunatamka kuwa ‘rushwa ni adui wa haki sipokei wala sitoi rushwa,” alieleza.

Suala hili la shirika la umeme nchini TANESCO na wabunge lilianza wiki chache zilizopita baada ya mkurugenzi wa shirika William Mhando, hilo kusimamishwa Katibu mkuu wa wizara ya nishati na madini EliakimMaswi ili kupisha uchunguzi wa shutuma za kutumia vibaya madaraka yake katika shirika hilo.

Hata hivyo baadhi ya wabunge akiwemo mbunge wa Kigoma kusini Zitto Kabwe (chadema) walilaani hatua hiyo ya kusimamishwa  kwa William Mhando na kuanza kuibua masuala mengine kama kupatikana zabuni ya kuiuzia TANESCO mafuta ya kuendeshea mitambo ya kuzalisha umeme kutoka kampuni ya mafuta ya PUMA energy. Na ndipo pakazuka madai kuwa hata baadhi ya wabune wapo ambao walihusika kufanya biashara na shirika hilo la umeme nchini ambapo walihusishwa na rushwa.

HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
31/07/2012

No comments:

Post a Comment