Friday, July 27, 2012

Mashirika ya umma kurudi Serikalini?

Picha hii si ya leo nimeitoa maktaba wadau,mnakumbuka nimewaambia kamera ya jembe imeharibika?


Waziri wa fedha nchini Dk William Mgimwa, amesema anataka kuona kuna ofisi inayojitegemea kwa maamuzi na uendeshaji wa mashirika ya umma ili kuleta ufanisi na kuhakikisha wananchi wananufaika kwa faida za mashirika ya umma.

Akizungumza katika kikao cha kujadili mapendekezo ya sheria mpya ya usajili wa hazina kilichofanyika leo asubuhi katika ukumbi wa Blue Pearl Ubungo Plaza jijini Dar es salaam, Mgimwa alisema walituma wataalamu ili kungalia vipengele ambavyo vilikuwa vikigongana na sheria ya awali iliyoundwa kubinafsisha mashirika ya umma.

“Nimekuja hapa kwa lengo moja tu la kuhakikisha tunajadili mapendekezo ya sheria mpya ya msajili wa hazina kwa kuunganisha sheria zote nne zinazotumiwa na kutunga sheria moja ili kuifanya ofisi ya msajili wa mashirika ya umma kuwa na mamlaka kamili katika kusimamia uwajibikaji na utendaji kazi wa mashirika ya umma,” alisema.

Hata hivyo katika kikao kilichokaliwa mwaka 2007 mwezi Machi na mawaziri, makatibu wakuu, kamati ya bunge ya fedha na uchumi pamoja na watendaji wakuu wa mashirika ya umma lengo likiwa ni kuangalia changamoto zinazoikabili sheria hiyo mpya.

Kikao hicho kilichokuwa chini ya uenyekiti wa aliekuwa Waziri wa fedha Mustafa Mkulo, kikao kiliona mapungufu mengi hivyo wakaamua kuunda kamati maalum ya kufuatilia uboreshwaji wa ofisi hiyo ya msajili wa hazina ili kuipa mamlaka thabiti.

Awali akizungumza katika kikao hicho katibu mkuu wizara ya fedha Ramadhan Shija alisema, wanakusanya maoni ya kuhakikisha mswada wa sheria hiyo mpya inapitishwa kwa maslahi ya watanzania wote.

“Msajili wa hazina hawezi kusimamia mashirika yote yaliyo chini ya serikali yapatayo 270, ambayo kwa pamoja yanatumia mapato ya Serikali kupata mitaji ya kujiendesha. Hivyo tunategemea kupata faida na si hasara kwani watanzania walio chini ndiwo watakaoumia,” alisema Shija.

Aidha katibu mkuu huo wizara ya fedha alibainisha kuwa ofisi ya wizara yao kupitia hazina wataendelea kupokea maoni kwa njia ya maandishi au maneno ili kuhakikisha sheria hiyo inapitishwa kwa baraka ya watanzannia wote.

Waziri Dk Mgimwa kila alipoulizwa na wanahabari kuwa mashirika ya umma yaliyobinafsishwa na Rais Mkapa yanaweza kurudishwa serikalini, lakini majibu yake ilikuwa ni kuwaambia wanahabari wangoje kwanza sheria hiyo ipite. 

HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
0713 593894/ 0752 593894
27/07/2012

No comments:

Post a Comment