JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA
YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
TAMKO LA SERIKALI
GAZETI LA MWANAHALISI
LAFUNGIWA
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania imelifungia kutochapishwa gazeti la MwanaHalisi kuanzia 30 Julai, 2012
kwa muda usiojulikana kutokana na mwenendo wake wa kuandika habari na makala za
uchochezi, uhasama na uzushi likiwa na nia ya kusababisha wananchi kukosa imani
na vyombo vya dola hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo
nchini.
Katika matoleo yake hivi karibuni,
gazeti la MwanaHalisi toleo Na. 302 la Jumatano Julai, 11 – 18, 2012 na toleo
Na. 303 la Jumatano Julai 18 – 24, 2012 na toleo Na. 304 la Jumatano Julai 25
hadi 01 Agosti, 2012 na mengine yaliyotangulia yamekuwa yakichapisha habari na
makala zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.
Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi,
ameitwa na kuonywa mara nyingi, lakini hataki kukiri kuwa maudhui ya makala
zake hazina tija kwa jamii, pia hazifuati weledi na maadili ya taaluma ya
uandishi wa habari.
Mhariri, mara zote katika utetezi wake
amekuwa akinukuu kifungu cha 18 cha Katiba ya nchi yetu ambacho kinatoa uhuru
wa kutoa maoni na kwa makusudi kutonukuu kifungu cha 30 cha Katiba hiyo
kinachoweka ukomo wa uhuru.
Uamuzi wa Serikali
Serikali imeamua kulifungia
kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi, kwa mujibu wa Sheria
ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu Na. (25) (i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30
Julai, 2012 kwa mujibu wa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 258
lililochapishwa katika Gazeti la Serikali na kutolewa jijini Dar Es Salaam
tarehe 27 Julai, 2012.
Serikali inawataka wamiliki,
wahariri na wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na maadili ya
taaluma ya uandishi wa habari katika kutekeleza wajibu wa kuhabarisha,
kuelimisha na kutoa burudani kwa wananchi.
Kuanzia sasa Serikali haitasita
kuchukua hatua dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa maksudi vitatoa taarifa
za uchochezi ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo nchini mwetu.
Imetolewa na
OFISI YA MSAJILI WA
MAGAZETI
WIZARA YA HABARI,
VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO
30 Julai, 2012
No comments:
Post a Comment