Ndugu zangu,
Kuomba radhi ni moja ya mambo ambayo sioni haya kabisa kutamka. Husemwa mambo matatu huwa mazito katika ulimi wa mwanadamu, moja ni kuomba radhi ama wengine huita msamaha. La pili ni kumwambia mtu kuwa unampenda na la tatu ni kukiri udhaifu ama kukubali kushindwa.
Leo nilikuwa katika kongamano la washairi pale shule ya msini kisutu, lilianza saa saba adhuhuri na kuisha saa kumi na moja alasiri. Tulijadili mambo mengi sana ikiwemo kudai haki za waandishi. Na ushauri wangu wa kutunga kitabu cha washairi waliohudhuria katika kongamano hilo ulipokewa kwa shangwe sana, hivyo subirini kitabu cha ushairi muda si mwingi.
Nimeamua kuandika haya baada ya Jembe langu Abdallah kichui, kuniuliza sababu za kuwa kimya leo. Hivyo nadhani hata ninyi mlikuwa na madukuduku ila hamkuwa na namna ya kuniuliza. Sababu ndiyo hiyo.
Mimi ni mshairi wa kawaida si wa siku nyingi sana. Nina mika ipatayo kumi katika fani ya ushairi na hujisikia raha sana mtu akinitambua kwa kupitia ushairi. Shule ilinifanya kuwa kimya kidogo katika masuala ya ushairi, mashairi yangu nilikuwa nikiandika katika magazeti kama Nipashe, Uhuru, Mzalendo na Mwananchi. Mengine yalikuwa ni magazeti ya kupita tu na sikuandikia sana.
Ila sasa baada ya kukaa kimya wadau wangu wa ushairi walinipigia simu kunialika katika kongamano hilo lililoandaliwa na gazeti la TABIBU. Naam gazeti hilo hutoa kurasa mbili kwa ajili ya washairi, ni kurasa nyingi sana kuwahi kushuhudia tangu nimeanza kutumbukia katika sanaa hii.
Ni gazeti la Uhuru pekee ndilo liliokuwa na kurasa nzima kwa ajili ya washairi tu, sasa leo TABIBU wana kurasa mbili. Si jambo la kupuuza hata kidogo.
Hata hivyo nawapa pole sana maana mmekosa picha za washairi wakongwe kama kina Mzee Sudi Andanenga (Sauti ya kiza). Kamera ya jembe imeharibika hivyo sina raha kabisa ndani ya moyo wangu... Niombeeni nipate wadhamini ili niweze kununua kamera ya kisasa jembe lenu liendelee kuwa hai.. Najisikia huzuni sana.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
29/07/2012
No comments:
Post a Comment