DK SLAA AONYA HAKUNA
HURUMA, MSEKWA ASEMA RUSHWA ADUI WA HAKI, MBATIA ATOA WIKI MOJA SPIKA AWATAJE
WOTE
Kizitto Noya, Dodoma na Leon Bahati,
Dar
VYAMA vya CCM na Chadema
vimetoa onyo kali kwa wabunge wanaotuhumiwa kwa kashfa ya kuhongwa na baadhi ya
kampuni za mafuta na kulihujumu Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), vikisema
havitasita kuwawajibisha pindi tuhuma hizo zitakapothibitika.
Kauli ya vyama hivyo
imekuja siku moja baada ya wabunge watano, watatu wa CCM na wawili wa upinzani
kudaiwa kuhusika na vitendo hivyo vya rushwa, ambavyo vimesababisha Spika wa
Bunge, Anne Makinda kuivunja Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na kuagiza
uchunguzi wa kina ufanyike ili majina ya wahusika yawekwe hadharani.
Wakizungumza kwa nyakati
tofauti jana, viongozi wa juu wa vyama hivyo walisema wanasubiri kwa hamu
taarifa rasmi kutoka bungeni.
CCM: Rushwa adui wa haki
Makamu Mwenyekiti wa CCM
Bara, Pius Msekwa alisema chama hicho kimewaapiza wanachama wake wote kutotoa
wala kupokea rushwa.
Alisema rushwa ni kosa
la jinai hivyo anaamini vyombo husika vya dola vitachukua hatua zinazofaa kwa
mujibu wa sheria za nchi.
Katibu wa Itikadi na
Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alikazia kauli hiyo akisema rushwa inaelezwa katika
katiba ya chama hicho kwamba ni, ‘adui wa haki’ na wanachama wote waliapishwa
kuwa hawatapokea wala kutoa rushwa.
Alisema yeyote
anayekwenda kinyume na kanuni za CCM, anajiweka katika kundi la wasaliti wa
chama.
Alisema wabunge ni kundi
maalumu nchini ambalo linalipwa vizuri ili lisimamie vyema misingi ya maendeleo
ya nchi pasipo tamaa wala vishawishi hivyo wanapotajwa miongoni mwa kundi la
wala rushwa, CCM kinalaani vikali tukio hilo .
Kuhusu tuhuma hizo
kutajwa kuwahusisha wabunge watatu wa chama hicho, Nape aligoma akisema habari
hizo siyo rasmi, hivyo hawezi kuzizungumzia.
Hata hivyo, alisema CCM
kinasubiri uchunguzi ufanyike ambao ndiyo utakaoweka bayana wahusika wa
tuhuma... “Tusubiri uchunguzi ukamilike. Idadi inawezekana ikawa hiyo au
ikapungua au kuongezeka.”
Dk Slaa: Hatufumbii
macho ufisadi
Katibu Mkuu wa Chadema,
Dk Willibrod Slaa alisema: “Nalaani kitendo cha wabunge kuhusishwa na ufisadi
hasa ikizingatiwa kwamba Chadema tumekuwa tukiupinga vikali. Tumekuwa tukipinga
rushwa kwa sababu ndiyo inayoielekeza nchi pabaya… Chadema hatufumbii macho
rushwa.”
Alisema tangu kuanza
Bunge la 10, Chadema kimekuwa kikiona baadhi ya mambo yanayoendelea katika
mhimili huo muhimu wa dola yamejaa walakini... “Ndiyo maana sisi Chadema
tumekuwa tukisema Bunge limepoteza mwelekeo.”
Alisema akiwa mtendaji
mkuu wa chama, anasubiri taarifa kamili kutoka katika kikao cha wabunge wa
chama hicho ili kuweka wazi majina ya wahusika na kisha kufuatiwa na kikao cha
Kamati Kuu (CC) ambacho kitakaa na kuchukua hatua kali.
“Tunahitaji tupate
maelezo ya kina... chama chetu hakikurupuki… Nasubiri taarifa ya kokasi ya
chama. Katiba ya Chadema inatambua uwapo wa kikao cha wabunge wetu na kwa
bahati nzuri, kiongozi wake mkuu ni Mwenyekiti wa Chadema (Freeman Mbowe) na
katibu (David) Silinde ni mbunge wetu. Tunasubiri taarifa yao .”
Alisema Chadema kina
kanuni ya kudhibiti rushwa hivyo, mbunge wake akitajwa miongoni mwa
wanaohusishwa na rushwa, atawajibishwa kupitia kikao cha CC ya chama hicho.
NCCR-Mageuzi yakoleza
moto
Katika hatua nyingine,
Chama cha NCCR- Mageuzi jana kilikoleza moto baada ya kumtaka Spika Anne
Makinda awataje wabunge hao bungeni ili wafukuzwe na kufungwa kama
Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge inavyotaka.
Chanzo: http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment