Tuesday, July 31, 2012

Tanga nao hawautaki ati....... Muungano.


Burhani Yakub, Tanga
MUUNDO wa  sasa wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,unapaswa kufanyiwa marekebisho kupitia Katiba Mpya, ili kupunguza manung’uniko na hatimaye mwafaka kuhusu Muungano.
Hayo yalisemwa juzi na wananchi wa Jiji la Tanga, walipokuwa wakitoa maoni yao kwa Tume ya Kukusanya Maoni ya Wananchi kuhusu Mabadiliko ya Katiba Mpya.

Wananchi hao, wamedai kuwa muundo wa sasa wa Muungano hauna tofauti na kuwaunganisha tembo na sungura, jambo ambalo haliletin usawa.


Akitoa mapendekezo yake, Jonathan Bahweje alisema kimsingi muundo wa sasa wa chombo hichon haufai kwa sababu hakuna fursa  sawa kati ya Zanzibar na Tanzania bara.

“Muungano wa sasa ni kama tembo na sungura, unawaweka pamoja halafu unasema umewaunganisha na wako sawa, wakati kwa uhalisia, haiwezekani,” alisema Bahweja.

Mwananchi huyo alipendekeza Katiba Mpya, ivunje muungano ili usiwepo
hatimaye Tanzania bara na Zanzibar, kila moja ijitegemee na kwamba hakuna sababu ya kuogopa kuuvunja chombo hicho.

“Mimi napendekeza Muungano uvunjwe ili kila nchi iwe na Serikali yake, kwa sababu manung’uniko ni mengi na  yanayotokana na jinsi muundo wa sasa usivyokubalika,”alisema Bahweja.

Alisema kama kuna ugumu wa kuvunja Muungano, basi ni vema kukawa na  Serikali tatu, ili kila nchi iweze kuwa na uhuru wa kuendesha mambo yake wakati kuna Serikali ya Muungano itakayosimamiwa masuala yanayohusu Muungano tu.

Kwa upande wake, Rashid Juma, ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kivumbitifu, katika Kata ya Pongwe, alitaka Muungano uvunjwe kwa madai kuwa wananchi wa Tanzania bara wanapokwenda Zanzibar na kurejea na bidhaa, wanatozwa ushuru wakati wakiwa ndani ya nchi moja.

“Huu Muungano hauna faida kwetu wananchi wa Tanzania bara,  unasemaje wamba tumeungana lakini sisi tukienda Zanzibar tukija na bidhaa tunatozwa ushuru lakini ukipeleka kutoka bara hakuna ushuru,”alihoji Jumaa.
 Chanzo:Mwananchi


No comments:

Post a Comment