SERIKALI imetangaza
kushusha gharama za kuunganisha umeme kwa wananchi wanaohitaji huduma hiyo kwa
viwango ambavyo ni kati ya asilimia 60 na 77 kwa wakazi wa vijijini na kati ya
asilimia 29 na 65 kwa wananchi waishio sehemu za mijini.
Waziri wa Nishati na
Madini, Profesa Sospeter Muhongo aliliambia Bunge jana kuwa gharama za
kuunganishiwa umeme kwa wateja walioko kwenye umbali usiozidi meta 30 (single
phase) ambao hawahitaji nguzo sasa zitakuwa Sh177,000 kwa wateja wa vijijini na
mijini itakuwa Sh320,960 badala ya Sh455,108 ambazo zilikuwa zikilipwa awali
bila kujali mteja aliko.
Akiwasilisha hotuba ya
makadirio ya matumizi ya wizara yake ya 2012/2013 bungeni Dodoma
jana, waziri huyo alisema punguzo hilo
ni sawa na asilimia 61.11 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 29.48 kwa
wateja waishio mijini.
Profesa Muhongo alisema
pia Serikali imeshusha gharama za uunganishaji wa umeme kwa wateja
watakaojengewa njia moja (single phase) na kuwekewa nguzo moja katika maeneo ya
vijijini ambao sasa watalipa Sh337,740 na mijini Sh515,618 badala ya
Sh1,351,884 zilizokuwa zikilipwa awali.
“Punguzo hilo la pili ni sawa na
asilimia 75.02 kwa wateja wa vijijini na asilimia 61.86 kwa wateja waishio
mijini,” alisema Profesa Muhongo.
Alisema kwa wateja
watakaojengewa njia moja na kuwekewa nguzo mbili katika maeneo ya vijijini
watalipa Sh454,654 na mijini watalipa Sh696,670 badala ya Sh2.001 milioni
zilizokuwa zikilipwa awali.
“Punguzo hili ni sawa na
asilimia 77.28 kwa wateja waishio vijijini na asilimia 65.19 kwa wateja waishio
mijini,” alisema Profesa Muhongo na kuongeza. “Viwango hivyo vya gharama
vitaanza kutumika Januari mwakani bila kisingizio.”
Chimbuko la Punguzo
Hatua ya kushushwa kwa
gharama za kuunganishiwa umeme zimekuja zaidi ya mwaka mmoja tangu Rais Jakaya
Kikwete alipolilekeza Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kupunguza
gharama hizo ili kupata wateja wengi zaidi.
Machi 18 mwaka jana,
Rais Kikwete aliitaka Tanesco, kupunguza gharama za kuunganisha umeme kwa
wananchi ili wengi wapate huduma hiyo sambamba na kuongeza wateja wanaotumia
umeme kwa asilimia 30 ifikapo mwaka 2015.
Akizungumza na
wafanyakazi wa Wizara ya Nishati na Madini, Rais Kikwete alisema gharama hiyo
ikipunguza, itaiwezesha Tanesco kupata wateja wengi ikilinganishwa na sasa.
Kauli ya Rais ilitokana
na maelezo ya Mkurugenzi wa Shirika hilo ,
William Mhando (ambaye sasa amesimamishwa kazi) kuwa Tanesco ilikuwa ikifanya
mazungumzo na Benki za Akiba na Azania ili
zitoe mikopo kwa wateja kwa ajili ya kuunganishiwa umeme.
Chanzo. http://www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment