Saturday, July 28, 2012

JK aonya makampuni yanayomilikiwa kifamilia....


RAIS Jakaya Kikwete amesema kampuni nyingi nchini zimeshindwa kuendelea kutokana na kuendeshwa kifamilia, badala ya kuuza hisa na kumilikiwa na umma. Akizindua Karakana ya Ndege ya Kampuni ya Precision Air jana, Rais Kikwete alisema kampuni nyingi nchini zinatakiwa kubadili mfumo wa uendeshaji.

“Watanzania wanaimiliki Precision Air kwa asilimia 59, huu ni mfano wa kuigwa kwa sababu ziko kampuni nyingi zimebaki kuwa za familia tu,” alisema Kikwete. Hata hivyo, Rais Kikwete alisema suala la hisa kwenye sekta ya anga bado ni biashara ambayo watu wengi hawajaielewa vizuri tofauti na sekta zingine kama benki. Alipongeza shirika hilo kwa kutengeneza karakana hiyo na kuitaka iwe na viwango vya hali ya juu vitakavyokidhi matakwa ya kimataifa.

“Tuache viwango vya kibongobongo, tukilipua tutahatarisha ustawi wa ndege na kampuni zitakazokuwa zinatumia karakana hii,”alisema. Pia, alitaka Wizara ya Uchukuzi na ile ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kujenga chuo cha ufundi wa ndege nchini.

“Siku hizi sijui hata wanajifunzia wapi... tunaona wanaruka tu walikojifunzia wanajua wenyewe,”alisema Rais Kikwete. Naye Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa shirika hilo, Michael Shirima alisema hadi sasa wana mtaji wa dola 2 milioni za Marekani na kwamba, wana ndege 12 huku wakimiliki tisa kati ya hizo.


itakumbukwa hivi majuzi aliekuwa mkurugenzi mkuu wa Tanesco ndugu Mhando, aliingia matatani kwa kusimamishwa nafasi yake hiyo ili kupisha uchunguzi baada ya kugundulika alikuwa akiipa tenda ya kusambaza vifaa va ofisi kwa shirika hilo kampuni ya mke wake.

No comments:

Post a Comment