Saturday, July 28, 2012

Nilichojifunza zoezi la usajili vitambulisho..

Ndugu zangu,

Serikali inapasa kuangalia watu wa kuwaweka katika mazoezi mawili haya ya kupata vitambulisho vya Taifa na zoezi la kuhesabu watu na makazi, maana leo asubuhi nilifika katika kituo cha kujiandikisha nikiwa na vielelezo vyote vilivyotakiwa.

Nilipewa fomu ya kujaza na nikafanya hivyo bila ya kuelekezwa, ndani ya dakika mbili nikawa nimeshamaliza, wakati nilikuta watu wanasaidiwa kujaza fomu hizo na makarani ambapo iliwachukua dakika tano mpaka kumi kujaza fomu ya mtu mmoja.

Kiongozi wa kituo baada ya kuvutiwa na umahiri wangu wa kujaza fomu bila kukosea wala kuelekezwa tena ndani ya muda mdupi akataka nimsaidie, kumbuka kuna makarani ambao wanalipwa kwa kazi hiyo.

Sikufanya hiyana maana najua kufanya kazi ya jamii hasa katika mwezi huu wa mfungo ni baraka kubwa sana, nikaanza kujaza fomu, ya kwanza, ya pili, dakika tano zilinitosha kujaza fomu zote mbili tena bila kukosea hata herufi moja ya jina wala mtaa wa mtu.

Nikaona mama mmoja wa kihindi lakini anazungumza kiswahili fasaha akapendezewa na mimi kusaidia watu, nae akaanza kusaidia kuandikisha watu: kwa kujitolea. Ndani ya dakika kumi nilikuwa nimefanikiwa kuandikisha watu zaidi ya watano. Na yeye kadhalika kwa kasi ya ajabu.

Kwa bahati mbaya nilikuwa na shughuli za kufanya hivyo nikaamua kuaga, lakini walijisikia vibaya sana wale wadau niliokuwa nikiwasaidia maana ghafla watu wote pale kituoni wakawa wanataka kusaidiwa kujaza fomu zao na mimi.

Nitawaambia kitu kimoja, nilikuwa mcheshi na mtambuzi wa kusoma akili ya watu. Nikiona mtu anaweza kutabasamu kwa utani mdogo niliomwambia nitaendelea kumtania huku namjazia fomu yake, tahamaki atakuwa na amani na ataona ni zoezi linalofaa kwa faida yake.

Nimegundua watu wengi hawajapewa elimu ya kutosha juu ya zoezi la vitambulisho vya taifa, wengi wanadhani wanataka taarifa zao ziwekwe katika nyaraka ili wakamatwe kwa urahisi. Si kweli hata kidogo, lengo ni kuhakikisha unaweka taarifa zako katika kumbukumbu ili hata kama watu wakiokota kitu chochote cha kwako ama ukipoteza passi ya kusafiria kitambulisho cha taifa kitakusaidia kukutambua.

Halafu tatizo jingine makarani walioajiriwa ni wazembe, wakali na wakaidi. Hawajui kutabasamu na mtu wala kumfanya mtu aamini yupo nyumbani pale anapotoa taarifa zake muhimu. Usifikiri ni kazi ndogo kwa mtu ambae hana elimu kukupa taarifa zake muhimu bila kinyongo.

Hata hivyo nimefurahi sana leo siku yangu imeanza vizuri na kazi ya jamii.
Ahasanteni.

Hafidh Kido
Dar es Salaam, Tanzania
28/07/2012

No comments:

Post a Comment