Saturday, July 28, 2012

Mkutano wa kudhibiti biashara ya silaha wakosa mwafaka umoja wa mataifa...

kushoto mstari wa mbele ni Bw. Theobald Kazora kutoka Ofisi ya Rais, Brigedia Jenerali Dkt. Charles Muzanila kutoka JWTZ ambaye pia alikuwa kiongozi wa ujumbe, Kaimu Balozi, Dkt. Justin Seruhere ambaye pia alikuwa kiongozi wa ujumbe akisaidia na Brigedia Jenerali Muzanila na Bw. John Kinuno ambaye ni wakili kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Kutoka kulia mstari wa nyuma ni Bw. Peter Macomara kutoka Taasisi ya Kiraia, Brigedia Jenerali Venance Mabeyo kutoka JWTZ na Kamishna Esaka Mugasa kutoka Jeshi la Polisi na Mwambata Jeshi katika Ubalozi wa Kudumu wa Tanzania Umoja wa Mataifa, Meja Wilbert Ibuge ambaye hayupo pichani. biashara ya silaha duniani inashika nafasi ya pili baada ya biashara ya madawa ya binadamu.


Na Mwandishi Maalum
Matarajio na matumaini ya kupatikana Mkataba wa Kisheria wa Kudhibiti Biashara ya Silaha Duniani ( ATT) yameishia ukiongoni baada ya nchi wanachama kushindwa kuzikabili tofauti za kimsimamo na kimaslahi.

Kuanzia tarehe Mbili hadi 27 mwezi huu wa Julai , wajumbe kutoka mataifa karibu yote duniani ikiwamo Palestina na Holly Sea, na Vyama Kiraia walikutana hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa kwa lengo moja kuu na muhimu sana, mstakabali wa biashara ya silaha duniani.

Pamoja na kujadiliana , wakati mwingine hadi usiku wa manane kuhusu umuhimu na malengo ya kuwa na Mkataba huo, nchi hizo hazikuweza kukubaliana kuwa na mkataba ambao ungesimamia ununuzi na matumizi ya silaha za aina mbalimbali zikiwamo pia risasi.

Kutofikiwa kwa Mkataba huo licha ya kutolewa kwa rasimu ambayo ilijitahidi kukidhi matarajio na maslahi ya kila nchi kumetokana na kutokukubaliana kwa vipengele vichache ambavyo baadhi ya nchi zilitaka viingizwe.

Vipengele ambayo vilishindikana kupatiwa ufumbuzi hadi siku ya mwisho ya majadiliano ni pamoja na, Baadhi ya Nchi zinazouza na kuzalisha silaha kutokuwa tayari kuingiza kwenye mkataba huo risasi na mabomu, huku nchi nyingine zikisisitiza vipengele hivyo viingizwe na kuwa sehemu ya mkataba.

Aidha nchi zilishindwa kukubaliana pendekezo lililokuwa limetolewa na mataifa ya Kiarabu la kutaka suala la Palestina la kujiamulia mambo yake liingizwe kwenye mkataba. Pendekezo hilo lilipingwa vikali na nchi za Ulaya na Marekani.

Vipengele vingine ambavyo vimechangia kutopatikana kwa Mkataba huo, ni kuhusu pendekezo la kutaka Taasisi na Mashirika ya Kikanda yanayo jihusisha na kuangalia matumizi ya silaha kutaka yapewe nafasi katika Mkataba huku baadhi ya nchi zikipinga pendekezo hilo.

Halikadharika, suala la Haki za kijinsia lilichagizwa na baadhi ya nchi likitaka liingizwe kwa kisingizo kwamba matumizi holela ya silaha yamekuwa ya kisababisha matatizo makubwa. Baadhi ya nchi hususani za Afrika zilipinga kuingizwa kwa kipengele hicho zikitumia kigezo kwamba hadi sasa hakujawa na tafsiri sahihi ya neno usawa wa kijinsia kutoka na baadhi ya mataifa ya magharibi kulazimisha kutambua haki za mashoga.

Kipengere kingine kilihusu kuingizwa kwa risasi kwenye mkataba, jambo lilozua mvutano na mabishano makali, huku nchi kubuwa zikikataa kata kata kuingizwa kwa risasi kwenye mkataba huku zikitishia kwamba zisingekuwa tayari kusaini mkataba huo kama risasi zingeingizwa.wapo

“Ninasikitika sana kwamba tumefika hapa tulipofika, hayakuwa matarajio yangu mimi kama rais wa mkutano huu na wala hayakuiwa matarajio yenu. Yalikuwa ni majadiliano magumu, yaliyojaa hisia kali tulijitahidi tulivyoweza kujaribu kuweka sawa maslahi ya kila upande. Lakini tumeshindwa kutoka na Mkataba” akatamka Balozi Roberto Garcia Morita wa Argentina aliyekuwa Rais wa Mkutano huo.

Akiongea kwa masikitoka makubwa Balozi Roberto Morita amesema kukata tamaa. 

“ Sitaki kusema mengi nisije nikatafsiriwa vibaya, ninaomba nibebe dhamana hii ya kushindwa kufikia malengo ya kuwa na mkataba. Nawashukuruni nyote kwa hatua hii tuliyofikia ingawa tumeshindwa kukidhi hamu na matarajio ya watu”.

Ingawa majadiliano kuhusu kuanzishwa kwa mkataba wa kudhibiti biashara ya silaha yalikuwa magumu na ingawa mkataba huo haukupatikana. 

Lakini majadiliano hayo yaliwezesha kupatikana kwa Rasimu ambayo kama isingekuwa kwa vipengele vilivyotajwa hapo juu kuzua mvutano katika siku za mwisho basi Mkataba ungepatikana. hatimaye chini ya usimamizi wa raisi wa mkutano huo. 

Karibu nchi zote ambazo zilipata nafasi ya kuzungumza baada ya Rais kutamka kuhitimisha kwa mkutano huo, ziliongea kwa hisia na kuelezea namna gani zilivyosikitishwa na matokeo hasi ya mkutano huo. Lakini zikaahidi kwamba zitakuwa tayari kuendelea na majadiliano hapo baadaye na hasa kwa vile sasa wanatambuana vilivyo na wanajua misimamo ya kila nchi.

Baadhi ya nchi kama vile Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, mjumbe wake aliezea kwamba kushindwa kupatikana kwa mkataba huo ni kielelezo cha wazi kwamba wananchi wa DRC ambao hawajawaji kuonja amani na usalama kwa miaka mingi wataendelea kuathirika.

“ Sote tunajua kwa nini tumefika hapa, silaha ni biashara ya pili kwa ukubwa baada ya ile ya madawa. Ni kweli tunasikitika kwa matokeo haya lakini hatujakata tamaa, tutaendelea kujadiliana ili hatimaye tuje kuwa na mkataba wa kudhibiti silaha. katika siku za baadaye tuje kuwa na mkataba.

Mkataba huo wa Kisheria kwa Kudhibiti Biashara ya Silaha Duniani kama ungepatikana basi silaha ambazo zingeguswa na mkataba ni pamoja na Magari ya Deraya, Helkopta za kivita, ndege za kivita, vifaru, magari ya kubeba mizinga, makombora, silaha ndogo na nyepesi.


Ujumbe wa Tanzania ambao kwa mwezi mzima umeshiriki kikamilifu hadi usiku wa manane pale ilipobidi na kuhakikisha kwamba maslahi ya Tanzania katika majadiliano ya kidiplomasia ya nchi wanachama kuhusu Mkataba wa Kisheria wa Kudhibiti Bishaara ya Silaha duniani yalikuwa yamezingatiwa. Hata hivyo mkutano huo ulioanza Julai Mbili na kumalizika Julai 27 umeshindwa kutoa Mkataba kutokana na wajumbe kutokukubaliana kuhusu baadhi ya vipengere ambavyo wengine walikuwa wanataka viwe sehemu ya mkataba, huku wengine wakikataa kata kata.
 Mkataba huo kama ungepatikana ulitarajiwa kwamba ungeleta matumaini na unafuu kwa mamilioni ya watu ambao maisha yao kila siku yamo hatarini kutokana na matumizi mabaya ya silaha.

Aidha mkataba huo pia ungedhibiti suala zima la ununuzi wa silaha hizo, usambazaji ,matumizi yake na kuhakikisha kwamba haziangukii mikononi mwa wahalifu.



Chanzo: Mjengwa blog.

No comments:

Post a Comment