Kufuatia uamuzi wa Spika wa Bunge jana jumamosi tarehe 28 Julai 2012 kukubali kuvunja Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini nimetakiwa kutoa maoni yangu kuhusu uamuzi husika kwa nafasi yangu ya Waziri Kivuli wa Nishati na Madini na mbunge:
Kwa maoni yangu uamuzi
huo ni sahihi lakini umechelewa na pekee hauwezi kurejesha heshima ya bunge kwa
ukamilifu wala hautaweza kushughulikia uzembe na udhaifu ulioko kwenye bunge na
kwenye serikali ikiwa hautaambana na hatua nyingine za ziada na za haraka.Kwa upande
mwingine, uamuzi huo umedhihirisha nilichokisema kwa nyakati mbalimbali kuhusu
uzembe wa kibunge pamoja na udhaifu wa serikali.
Ukiondoa tuhuma za
wabunge wanaodaiwa kupokea rushwa ama kuwa na maslahi ya kifedha kwenye wizara,
taasisi au mashirika wanayoyasimamia kwenye kamati mbalimbali, heshima ya bunge
imeathiriwa vile vile na maamuzi mathalani uamuzi wa kuchaguliwa kwa mtuhumiwa
wa ufisadi wa Rada Mbunge Andrew Chenge kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Fedha na
Uchumi.
Hivyo hatua zaidi
zichukuliwe ikiwa ni pamoja na kuvunja na kamati zenye wajumbe waliotuhumiwa na
pia kufanya mabadiliko makubwa kwenye wajumbe wa kamati mbalimbali za kudumu za
bunge ili kupunguza maslahi ya kifedha ama tuhuma za rushwa miongoni mwa
wajumbe wa kamati. Aidha Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge imalize
kazi yake kwa dharura ili majina ya wahusika yatajwe ndani ya bunge na bunge
lijadili kupitisha maazimio ya hatua za ziada za kuchukuliwa na vyombo huru vya
kiuchunguzi na hatimaye watakaothibitika kuvunja sheria wafikishwe mahakamani.
Pamoja na hatua hizo, Kamati za Vyama nazo zichukue hatua kwa wabunge wake
watakaotajwa ili kudumisha misingi ya uadilifu na uwajibikaji kwa maslahi ya
umma.
Hata baada ya hatua
hizo, izingatiwe kuwa Bunge litaweza kujinasua kwenye uzembe ikiwa litatimiza
kikamilifu wajibu wake wa kuisimamia serikali kwa mujibu wa ibara ya 63 kuondoa
udhaifu wa serikali kwenye sekta ya nishati na sekta nyingine muhimu za taifa
kwa kuhakikisha maazimio yote ya bunge yanatekelezwa kwa ukamilifu na kwa
haraka kama nilivyoeleza kwenye maoni ya kambi rasmi ya upinzani bungeni tarehe
15 Julai 2011 na tarehe 27 Julai 2012.
Nilisema bungeni kwamba
“Naamini iwapo maazimio ya Bunge juu ya Mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya
Richmond Development Company LLC yangetekelezwa yote na kwa wakati toka mwaka
2008, maazimio ya bunge juu ya uendeshaji wa sekta ndogo ya gesi asili ya mwaka
2011 yangezingatiwa yote na kwa haraka, maazimio kuhusu uhalali wa utaratibu wa
Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti
bungeni ya mwaka 2011 yangechukuliwa kwa uzito unaostahili; taifa lingeepushwa
kurudia mijadala ile ile kuhusu Wizara hii hii mara kwa mara”.
Mathalani, Waziri wa
Nishati na Madini ameeleza bungeni tarehe 28 Julai 2012 kuwa wapo wabunge
wanaotuhumiwa kufanya biashara zenye kulihujumu Shirika la Umeme (TANESCO) na
Spika wa Bunge akahitimisha kuwa Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge
itachunguza tuhuma husika na pia kwamba inakusudiwa kutungwa kwa Kanuni za
Maadili (Code of Conduct) ili kudhibiti hali hiyo.
Hata hivyo, Serikali na
Uongozi wa Bunge kwa pamoja wamesahau kuwa mwaka 2008 baada ya Kashfa ya Richmond
iliazimiwa katika Azimio Na. 11, kwamba “Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma
ya Mwaka 1995 (The Public Leadership Code of Ethics Act), ifanyiwe marekebisho
makubwa ili kudhibiti utaratibu unaoonekana wa kawaida sasa wa Viongozi
Waandamizi wenye dhamana ya kisiasa kuendelea na biashara zao binafsi wakiwa
madarakani, jambo ambalo lina mgongano wa kimaslahi. Serikali ianze rasmi
maandalizi ya majadiliano ya kina kuhusu suala hili ndani na nje ya Bunge kwa
kuwashirikisha wadau mbalimbali.”
Bunge lilitaarifiwa
Februari 2010 kuhusu utekelezaji wa Serikali kwamba kikundi kazi (Task Force)
kiliundwa ambacho kiliandaa waraka wenye mapendekezo ya kurekebisha Sheria ya
Maadili ya Viongozi wa Umma, (Sura 398) ambao ulikuwa katika ngazi ya
kujadiliwa na Kamati ya Makatibu Wakuu (IMTC). Aidha, Bunge lilielezwa kuwa
serikali ilitarajia kuwasilisha muswada husika katika mkutano wa kumi na tisa
wa Bunge la tisa. Muswada huo haukupitishwa katika Bunge la tisa kama
ilivyoshauriwa na kamati na mpaka kutokana na uzembe na udhaifu azimio hilo
halijatekelezwa na tuhuma nyingine zimeendelea kuibuka.
Aidha, kumetolewa madai
ya baadhi ya wabunge kupokea ama kudai rushwa suala ambalo nalo Spika wa Bunge
ametoa uamuzi kuwa litashughulikiwa na Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya
Bunge. Lakini Serikali na Uongozi wa Bunge kwa pamoja wamesahau kwamba hii si
mara ya kwanza kwa tuhuma za namna hiyo kutolewa juu ya baadhi ya wabunge wa
kamati mbalimbali za bunge.
Hata hivyo, kwa sababu
ya kutochukua hatua kwa haraka na kwa ukamilifu tuhuma kama hizo zitaendelea
kujirudia hata baada ya kuvunjwa kwa kamati ya bunge ya nishati na madini.
Izingatiwe kwamba madai ya rushwa kutolewa kwa wabunge yaliwahi kujitokeza
kuhusu Kamati ya Nishati na Madini na binafsi nilitoa ushuhuda kwa Ofisi ya
Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mwaka 2011, na nikatoa ushuhuda tena
kwa Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza uhalali wa utaratibu wa Wizara ya
Nishati na Madini kuchangisha fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni mwaka
2011 kuwa yamekuwepo matukio ya kushawishi wabunge kwa rushwa hata hivyo hatua
hazikuchukuliwa ama kuvunja kamati zilizotajwa au kuwachukulia hatua wahusika.
Suala hili likatajwa
tena na Mbunge wa Kigoma Kaskazini David Kafulila kuhusu Kamati ya Hesabu za
Serikali za Mitaa na likatajwa tena na Kiongozi wa Upinzani Freeman Mbowe na
Mbunge wa Kyela Dr Harrison Mwakyembe kuhusu uchaguzi wa Afrika Mashariki
lakini hatua hazikuchukuliwa kuchunguza wabunge husika na kuchukua hatua. Iwapo
maazimio kuhusu uhalali wa utaratibu wa Wizara ya Nishati na Madini kuchangisha
fedha kwa ajili ya kupitisha bajeti bungeni ya mwaka 2011 (Maarufu kama Sakata
la Jairo), yangetekelezwa na wahusika wangechukuliwa hatua ingejenga nidhamu
pia kwa watendaji wa wizara na mashirika ya umma kuhusu rushwa na matumizi
mabaya ya fedha za umma yenye kulenga kuwaathiri wabunge kwa rushwa na maslahi
mengine ya kifedha.
Katika hali inayoonyeha
kwamba Serikali bado haioni uharaka na ulazima wa kuchukua hatua, wakati bunge
lilipokaa kama kamati tarehe 28 Julai 2012 kupitisha bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini nilitaka ufafanuzi kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini
kuhusu utekelezaji wa maazimio hayo ambayo mpaka sasa hakuna taarifa ya
utekelezaji iliyowasilishwa bungeni toka yapitishwe mwezi Novemba mwaka 2011;
lakini Waziri akajibu tu kwamba hawezi kufanyia kazi taarifa za magazetini,
bila kujali kwamba nilichouliza hakihusu taarifa za magazetini bali maazimio ya
bunge baada ya kazi iliyofanywa na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali na
ikarudiwa tena na Kamati Teule ya Bunge ambayo ilihoji wahusika na kupata pia
vielelezo.
Kwa hiyo, ni muhimu
Serikali na Uongozi wa Bunge ukarejea kwenye Hotuba niliyowasilisha bungeni na
kuchukua hatua kwa usimamizi wa Rais, Waziri Mkuu na Spika wa Bunge juu ya
masuala yote niliyoyaeleza. Pamoja na kutaja ushawishi uliokuwa ukifanywa kwa
wabunge kuhusu suala la ununuzi wa mafuta ya IPTL, na ufisadi ndani ya TANESCO
nilieleza pia masuala mengine makubwa kwenye nishati na madini yenye kuhusu
mabilioni ya shilingi kwenye mikataba mikubwa ya umeme, madini, mafuta na gesi
asili pamoja na hatua za mabadiliko ya kimfumo zinazopaswa kuchukuliwa.
Nimetoa maoni hayaleo
jumapili tarehe 29 Julai 2012:
John Mnyika (Mb)
Waziri Kivuli wa Nishati
na Madini
Chanzo:Mjenwa blog
No comments:
Post a Comment