Ni kawaida katika
mahusiano kuwa na magomvi yasiyokwisha juu ya wapenzi kutoka nje ya mahusiano;
si jambo la ajabu tena kwa maisha ya sasa yaliyochanganyika tamaduni na
historia mbalimbali.
Nimekuwa nikijiuliza kwa
muda mrefu juu ya suala hili la kukosa uaminifu katika mapenzi, kwa maana
sikuona sababu ya msingi kwa mtu kutoka nje ya mahusiano.
Kipi hasa kinachomfanya
mtu akakosa uaminifu juu ya mpenzi wake. Je ni starehe za kitandani? Ni starehe
za maisha na raha za mahaba? Au ni tama tu za kimwili..
Lakini waswahili husema
utu uzima ni dawa, ingawa sijawa mtu mzima wa hivyo kusema nimeona megi; ila
maisha ya sasa hata watoto tunakutana na misukosuko inayotulazimu kukua kabla
ya umri kufika.
Nitaziainisha sababu
hizo saba kwa maelezo ya kutosheleza, ikibidi nitatoa mifano ya kusaidia
kuelewa mada kwa utaratibi mzuri na mpangilio mwema rahisi kuelewa.
Sababu ya kwanza: ni
Kupungua mapenzi; hii imekuwa ni sababu kuu ya kumfanya mtu atoke nje ya
mahusiano. Kwani kawaida kuna watu hupenda kudekezwa au kupewa mapenzi motomoto
bila kupungua hata chembe kwa kipindi chote cha mahusiano.
Kwa mfano; wakati penzi
linapokuwa changa kuna kule kupigiana simu kila dakika, mtaongea hata upuuzi na
kuchekacheka huku mkitaniana kama watoto
wadogo. Ukila chakula fulani cha tunu utamwambia mpenzi wako, wakati unapika
ukijikata na kisu kwa bahati mbaya utampigia simu mpenzi wako huku ukideka, na
mengi kama hayo .
Mara nyingine mtatoka
mandari (matembezi ya baharini au jioni), mkiwa huko baharini mtarushiana maji,
mtamwagiana michanga huku mkikimbizana kwa vicheko.
Mara nyingine mnaweza
kuwa mkahawani mkila ama mkinywa, mpenzi wako anaweza kukulisha ama
akafanya kama anakulisha halafu anakwepesha au
anakula yeye. Mradi tu mcheke ama umpige kofi kidogo la mahaba, na stihizai za
kilimbukei. Lakini hayo ndo mambo ambayo wengi huwa nayo kwa kila penzi changa.
Baada ya kupita miaka
miwili ama mitatu mambo kama hayo hupungua.
Hamtakuwa na muda tena wa kuchezacheza namna hiyo. Inawezekana kazi zinawabana
ama mwanamke anaweza kuwa amejifungua na mapenzi yote ameyahamishia kwa mtoto.
Hapo sasa mume huanza
kutafuta kibinti kidogo kitakachomrudishia ile michezo ya awali aliyoizoea
kutoka kwa mkewe. Unaweza kumkuta mzee wa miaka hamsini lakini wakati akiongea
na kimada wake wa miaka ishirini huwezi kuamini, wanataniana na kuchekacheka kama mahantobwe au mahayawani wa mapenzi.
Kadhalika mume anaweza
kubanwa na kazi, mke kila akijitahidi kupata nafasi ya kuchezacheza na mumewe
huwekwa pembeni.
Anaweza kumpigia simu
mumewe ofisini akaambiwa ana kazi nyingi wataongea nyumbani, akitoka kazini
jioni amechoka, akishawekewa maji ya kuoga na kula huhamia mezani na ‘laptop’
yake anamalizia kazi za ofisini mpaka usiku mwingi, akitoka hapo hujiagusha
kitandani na kulala, asubuhi na mapema kazini. Ikifika jumapili mama huanza
kufurahia kwa kuona atakaa nyumbani na mumewe, lakini baba atasema ana semina
Bagamoyo na atalala hukohuko.
Hivyo, hayo ndiyo
matatizo yanayomfanya mume au mke kuanza kutafuta mtu atakaempa furaha kama zamani. Na ndiyo maana utakuta mume au mke hayuko
tayari kuharibu ndoa yake, ila hutoka nje ya ndoa. Kumbuka hajachoshwa na ndoa,
bali ni vitu fulanifulani tu anavikosa na ndivyo vinavyomfanya atoke nje.
Sababu ya pili: ni
tamaa ya kupata zaidi ya akipatacho katika ndoa au penzi la kawaida tu la
uchumba.
Inaweza kuwa ni tamaa ya
fedha au utundu wa kitandani, husemwa mapenzi si fedha, lakini watu husahau
kuwa mapenzi huendeshwa kwa kutumia fedha.
Chukulia utataka kutoka
mandari na mpenzi wako, lazima mtahitaji kununua juisi, soda au chakula cha
jioni kitakachowafanya muwe pamoja usiku huo. Vilevile hata kama
mpo katika ndoa, ni vema siku mojamoja muende mkalale hotelini ili kubadilisha
mazingira ili pendo lenu lizidi kushamiri.
Tazama mambo hayo
yote yanahitaji fedha, si za kumuhonga mpenzi wako la hasha, bali ni kugharamia
hayo matumizi ya kuimarisha pendo na kulipalilia furaha.
Ndiyo ukaona watu wengi
huamua kutafuta wanaume au wanawake watu wazima wenye kipato kizuri ili wapate
fedha za kuja kufurahi na wapenzi wao wanaolingana umri.
Na mara nyingine mwanume
au mwanamke anaweza kuwa na mpenzi mwenye fedha, ila bado anatoka nje; sababu
huwa ni kutafuta ridhiko la kitandani.
Zingatia hili: wanaume
wengi hawawaridhishi wapenzi wao, huwa na pupa ya kukimbilia tendo bila
kumuandaa mpenzi wake. Matokeo ni mwanamke kukaa katika mahusiano kwa miaka
miwili lakini asiridhishwe kimahaba na mpenzi wake. Hivyo huamua kutafuta
shababi mmoja atakaemtimizia haja yake.
Kumbuka mwaamke
hajachoshwana ndoa, bali ni mambo fulani fulani huyakosa; inawezekana anampenda
mumewe kuliko hata huyu anaemridhisha, lakini huamua kutoka nje ili aendelee
kuwa na huyu mumewe wakati huohuo awe anafurahia usichana wake. Sijui
nimeeleweka hapa?
Ukitaka kugundua hili,
mwanamke anaetoka nje ya ndoa akihisi anagundulika yupo tayari kuachana na huyo
anaeiba nae na si mumewe; sasa kama ikiwa
mumeo hakuridhishi si ubaki na huyu anaekuridhisha? Na si mwanamke tu, hata
mwanaume anaesaliti ndoa yake akihisi anagundulika haraka huachana na hicho
kibinti na kubaki na mkewe.
Ndoa zina mambo mengi, hilo ndilo jibu muafaka
kwangu. Unaweza kuwauliza wanawake mia moja juu ya mahusiano katika ndoa, na
ukagundua takriban wanawake thamanini hawaridhishwi na waume zao.
Kadhalika hata wanaume
wapo ambao shughuli yao
ni kubwa, kwa wiki anaweza kumuingilia mke wake hata mara kumi. Kwa siku tendo
moja anaweza kufikia mshindo mizunguko mitatu mpaka minne. Sasa wanawake
wengine ni dhaifu huchoka haraka na mara nyingine huwakatalia waume zao.
Hivyo waume namna hiyo
huamua kutoka nje ya ndoa na kutafuta kahaba au janajike linaloweza shughuli anayoitaka
yeye.
Haya si mambo ya
kufikirika, ni vitendo ambavyo tunakutana navyo katika jamii. Na ndiyo maisha
ya kila siku ya mwanaadamu, si Afirika pekee bali dunia nzima mambo haya yapo.
Kuna wanaadamu wa
kipekee ambao hupendakufanya tendo kinyume na maumbile. Hawa hufundishwa
michezo hii na wapenzi wao wa kwanza kwa kuhofia kupata mimba au kuharibu
ubikira wao.
Sasa hufikia wakazoea
michezo namna hiyo, pindi wakishaolewa hupata bahati mbaya wakaolewa na waume
wasiopendezewa na michezo hiyo ya kuenda kinyume na maumbile. Hivyo hutafuta
watu wenye kuipenda na hapo ndipo kutoka nje ya ndoa kunapoanza.
Sababu ya tatu: ni
kukosa wa kukujali; na mara nyingi sababu hii huwahusu kina dada. Wanawake
hupenda kujaliwa, ukimjali mwanamke na kumsikiliza kilio chake hujisikia faraja
sana .
Sasa, hutokea wakaolewa
ama wakapata wanaume wakatili ambao hawana muda wa kuwafuta machozi. Ndipo
wanapotafuta wanaume wanaojua kubembeleza huku wakifanya zaidi ya
kubembelezana. Humpa mwili wake kama zawadi ya
kumjali.
Nitatoa mfano: mwanamke
anaweza kuondoka nyumbani baada ya kutaka kudekezwa halafu akagundua mumewe
hana muda nae bali amekazana kuangalia mpira au kuzungumza na marafiki zake
huku wakinywa pombe.
Mke huamua kutoka
nyumbani akatafuta mahala tulivu na kupata kinywaji kuburudisha nafsi yake, au
akaenda baharini kutuliza akili kwa upepo mwanana wa bahari huku akitazama
kupwa na kujaa kwa kurasa kuubwa nyeupe za maji.
Huko anaweza kukutana na
mwanaume ambae ni mchangamfu, atamchekesha, atamtaniatania mwisho watakuwa
marafiki na kuamua kumpa siri ya moyo wake.
Zingatia hili, wanawake
hawajui kuweka kitu moyoni, hudhani akimpa kila mtu siri yake au tafrani zake
ndiyo faraja asaa akapata msitiri wa kumliwaza. Na ndiyo maana wanawake
waliotendwa katika mahusiano niwepesi sana
kutongozeka wakati wakiwa katika kilio.
Mara nyingi wanaume
wanaojua siri hizo za kinadada kwa lugha ya kimombo huitwa ‘sharp shooters.’
Hawacheleweshi, hapohapo atampa bega lake
ili mwanamke apate pa
kuegemea na kumaliza kilio chake.
Baada ya hapo wanaweza
kupanga kukutana sehemu hiyo kila siku au kila juma, na mabadiliko ya dunia
kuna simu za viganjani, watakuwa wanatumiana jumbe fupi za kuliwazana na
kutakiana kheri ya usiku.
Mume ataona kero ya
mkewe imepungua na kila siku ana furaha, akiombwa ruhusa ya kutoka atafurahi
kwani huona atapata wasaa mzuri wa kukaa na marafiki wakitazama mpira,
kumbe vyake vinaliwa.
Kwa upande mwingine hata
mume hupenda kujaliwa na kuonewa wivu. Mke akijali sana
watoto na mashoga akamsahau mume hilo
ni kosa katika mapenzi.
Kwa mfano, mume anaweza
kuwa amerudi toka kazini amechoka, mke amejitandaza upenuni anapiga soga na
mashoga zake au ananyonyesha. Badala ya kumuandalia mume maji ya kuoga au dunia
ya sasa hakuna kuandaliana maji ya kuoga, lakini japo ampokee mumewe mizigo,
amsaidie kuvua nguo na kumkandakanda mwili kutokana na siku nzito aliyokuwa ayo
kazini, lakini hayo hayafanyiki.
Mume anapoona hapewi
huduma hizo huamua kutafuta mtu mwenye kuweza kutoa huduma hizo nae afaidi raha
za dunia. Wewe utaona mumeo anatoka kazini kila siku amechangamka, utaona
amekupunguzia mzigo kumbe mwanamke mwenzio anakusaidia.
Duniani kwa sasa huduma
hizi hutolewa kama biashara, kuna wanawake
mahsusi wanawafanyia wanaume ‘massage’ na wanalipwa fedha nyingi. Kifupi
mwanaadamu hupenda kukandwakandwa mwili wake baada ya kufanya shughuli ngumu ya
kutumia nguvu au akili.
Sasa inapofikia wakati
mwanaume anavua nguo ili akandwe na jinsia ya kike tena si mkewe, sidhani kama hapo kuna usalama. Lakini ikiwa mke atampa mumewe
huduma hiyo ni salama zaidi katika kudumisha mahusiano.
Vilevile mume au mke
anaweza kuwa na gubu au kelele kila wakati; mara amembwatukia jirani, mara
kamchapa mtoto, mara kamfokea mfanyakazi za nyumbani. Alimuradi mume hana amani
katika nyumba.
Akili yake imechoka
anahitaji kupumzika au kufanya kazi zake za ofisini nyumbani, matokeo yake
huamua kutafuta sehemu kama baa au hoteli
iliyotulia ili afanye kazi zake huku anashushia kinywaji. Na baada ya hapo
anaweza kukutana na mijanajike inayosaka waume za watu na kuanza uhusiano. Mke
hapo inakuwa huna chako tena.
Sababu ya nne: ni
mwanaume au mwanamke kutaka kutimiza ndoto yake katika ujana. Tunafahamu vijana
wanakuwa na ahadi nyingi, nyingine za kipuuzi na nyingine za maana.
Sasa msichana ama
mvulana anaweza kuweka ahadi ni lazima atatembea na mtu fulani kimapenzi.
Mfano, binti anaweza
kusoma shule moja na kijana ambae alikuwa akimpenda kwa roho yake yote, ila
alikuwa akiogopa kumwambia.
Hutokea miaka ikapita na
wote wameshakuwa watu wazima, na mara nyingine keshaolewa na kusahau hata hiyo
ahadi aliyoweka.
Inatokea bahati tu siku
anakweda kazini au sokoni akakutana na huyo kijana, bado ni mzuri vilevile na
mikogo yake ya shule na muonekano vipo vilevile au vimezidi maradufu.
Hapo tena ile ahadi
inamjia na pendo linaanza upya, husemwa mtu mzima hana maya. Yaani watu wazima
huambizana kiutu uzima. Si kama watoto mpaka wazunguke, wajing’ate vidole au
waanza kukunjakunja nguo.
Hapana, watu wazima wao
huambiana kitu kilekile kilicho moyoni. Hapo mapenzi huanza na labda kutokana
na kumtamani siku nyingi mke hugundua alikuwa akikosa vitamu kutoka kwa huyo
kaka. Hapo tena balaa linaanza la kutoka nje ya ndoa.
Hata mwanaume anaweza
kuwemo katika kundi hilo
la kuweka ahadi kuwa mwanamke fulani ni lazima nimpate, lakini labda wakati
anaweka ahadi hiyo alikuwa kijana mdogo na hana pesa za kumghilibu au hana
maneno matamu ya kumhadaa.
Hivyo anapopata kazi na
kuoa, mara nyingine nae alishamsahau msichana huyo, wakikutana maofisini au
njiani ndipo hukumbukana na kijana huamua kutimiza ahadi yake, bila ya kujijua
kuwa tayari yumo katika mkataba wa ndoa na mwanamke mwengine.
Na wanaadamu wa siku
hizi unaweza kumwambia nimeshaoa ama nimeshaolewa na pete ya ndoa unayo, lakini
bado hujisikia raha kufanya machafu na wewe.
Sababu ya tano: ni
kuficha udhaifu wako katika jamii inayokuzunguka. Na hii inawahusu sana wakina baba.
Inaweza kutokea mwanaume
ni mtanashati sana ,
awapo ofisini au nyumbani huvaa nadhifu, afanyapo kazi zake huwa makini.
Anapoijali familia yake hataki mchezo; kifupi ni mfano wa kuigwa na shujaa.
Wanawake wengi hupenda
wanaume mashujaa, wanaojali kazi na familia zao bila ya kujisahau wao wenyewe.
Maana wapo wanaume hujali kazi kiasi hawakumbuki familia zao wala miili yao .
Hivyo kwa minajili ya
kuwa shujaa katika jamii wanawake wengi hutokea kujigonga kwa baba huyo; baba
atajaribu kujiheshimu na kuamua kuwakatalia, ima kwa wazi wakitumia neno
‘sitaki, nina familia’ au kwa kutumia matendo tu; kama
kutotimiza miadi ya mualiko wa chakula cha mchana au usiku. Kukataa kahawa au maua anayoletewa ofisini
na msichana huyo au hao.
Lakini jamii
inayomzuguka baba huyo itaanza kudadisi mienendo yake na wanawake hao. Maneno
kama ‘anatupa bahati, au hana nguvu za kiume ndo mana anakataa wanawake
wazuriwazuri,’ yatakuwa mengi sana .
Na wanawake wakishasikia
minongono kama hiyo ndipo watakapozidisha vituko na kujionyesha wazi wazi kama mwanaume huyo haonyeshi kuwajali ingawa wao ni
wazuri na kila mwanaume angetamani kuwa nao.
Kadhalika hata mwanamke
inaweza kumtokea hali namna hiyo; anaweza kuwa ofisini bosi akawa anamtamani
kimahaba. Atamuongeza mshahara, atampa safari za kikazi ulaya na sehemu
nzurinzuri. Lakini ataombwa mapenzi na ahadi nyingi zaidi ya alivyopata ambavyo
wafanyakazi wenzie hawana.
Atakapokataa kwa kutaka
kulinda ndoa, wafanyakazi wenzie wa kike wataanza kumuandama kwa maneno, ‘wewe
huyo mumeo atakupa nini, unaacha bahati kama
hii, looohh shoga huna akili unaokota kopo la dhahabu mtaa wa kongo unakataa
kulichukua.’ Na maneno mengi namna hiyo.
Mwanamke ataona aibu kwa
kutazama hali mbaya ya nyumbani, mara nyingine labda ametishiwa kufutwa kazi na
bosi kwa kukataa ombi lake
ovu . Hivyo huamua
kusaliti ndoa yake si kwa kuwa hampendi mumewe, bali ni kukabiliana na mitihani
ya maisha iliyo migumu.
Sababu ya sita: ni
msukumo kutoka kwa wazazi, mara nyingi hii huwaathiri wanaume. Inafahamika sana wazazi hasa wa kike
hupenda kuwachagulia watoto wao wa kiume wake wa kuoa.
Na hii husababisha
mikanganyiko ya mawazo kwa watoto wa wa kiume mpaka kufikia kutoka nje ya ndoa
ili kuwaridhisha mama zao. Kwani hali huwa mbaya kiasi mama huamua kumtafutia
mwanae wa kiume mwanamke mwengine ili kumkomoa mkwe wake.
Sitoiongelea sana sababu hii, kwani inajulikana sana
katika jamii; kisaikolojia wazazi wa kike huwa na wivu sana kwa watoto wao wa kiume. Hutamani
wasiondoke nyumbani na ikiwa wataondoka basi waende kwa wake ambao watawachagulia
wao, na ikiwa hawajawachagulia basi wake watakaoolewa na wanaume namna hiyo
basi wajipange na mashambulizi toka kwa mama wakwe wao.
Mama anaweza kutafuta
mtoto wa shoga yake na kumtambulisha kwa mwanae wa kiume huku akijua
tayari ni mume wa mtu; kinachotokea hapo ni urafiki wa kiwizi au kihawara mradi
tu amfurahishe mama yake.
Lakini ikumbukwe ndoa si
kitu cha kukiteganisha hivihivi tu, kwa maana labda wameshazaa, ama wameshakaa
katika mahusiano kwa muda mrefu na jamii imeshawazoea kuwaona hivyo. Kutengana
na mkewe linakuwa jambo gumu lakini ataamua kumfurahisha mama yake.
Kwa upande wa mwanamke
inaweza kuwa tofauti kidogo, familia za kitajiri huwa hawapendi
kuwaozesha watoto wao kwa familia za kimaskini. Hivyo hutokea binti
akalazimisha kuolewa na mume anaemchagua, lakini katikati ya safari maisha
yakawa magumu.
Anapoamua kurudi kwao,
familia humtenga na kumwambia ‘tulikuonya usiolewe na huyo mume.’ Matokeo yake
mwanamke huamua kutaka kuwaridhisha wazazi wake kwa kutembea na mwanaume mwenye
kipato, ingawa mume wake wa awali hajaachana nae.
Maana hutokea ikawa ni
ngumu kuachana nae kwani wameshazaa na mara nyingine wameshazoeana.
Sababu ya saba: na ya
mwisho kwangu si kwa kila mtu, nasisitiza si kwa kila mtu kwa maana kila mtu
atakuwa na sababu zake za kwanini mtu anatoka nje ya ndoa. Sababu hiyo ya
saba inatoakna na kufufua penzi lililositishwa na hali ya maisha au mazingira.
Hapa nazungumzia utoto,
fedha au jamii inayowazunguka ilivyokua ikiwachukulia. Inawezekana mlipokuwa
vijana mlikuwa katika penzi motomoto, lakini kwa kuwa familia zenu zilikuwa na
ugomvi wa muda mrefu hivyo haikuwezekana kuoana, ama dini zilikinzana hivyo
ukaamua kuoa au kuolewa na mtu mwingine na kumsahau kabisa mtu Yule uliekuwa
ukimpenda sana .
Lakini kwa muda fulani
mlikosana na mwenza wako Yule wa awali, ukakaa na mume au mke wako mpya hata
kwa miaka kumi, ingawa ulikuwa humpendi mume au mke huyo mpya lakini mmeshazaa
na inawezekana umeshamsahau mweza Yule wa awali.
Bila ya kutegemea
unakuja kukutana na Yule mpenzi wako wa zamani, ambae labda ndie aliekutoa
ubikira au kama ni mwanaume ndie
aliekufungulia kitabu cha mapezi; kifupi ndie mpenzi wako wa kwanza kabisa
katika maisha yako.
Namna hiyo mara nyingi
penzi huweza kuchipua upya bila ya kujijua; ile nguvu ya penzi la dhati
mlilokuwa nayo inaweza kuwafaya mkumbushie ya zamani.
Kidogokidogo bila ya
kujijua mnaweza kujikuta mnachipua penzi lililolala siku nyingi kwani
mlitenganishwa tu na mazingira na si ridhaa yenu. Ni hatari sana kuoa au kuolewa na mtu ambae
alilazimishwa kuachana na mpenzi wake aliekuwa akimpenda kuliko chochote.
Hivyo sababu zote saba
ni vema kuziangalia kwa makini na kujiuliza wewe umeangukia wapi. Usilaumu wala
kujilaumu ikiwa unaoa mpenzi wako anatoka nje ya ndoa na kukosa uaminifu, ni
vema kukaa nae chini kwa umakini na kumuuliza sababu za kufanya hivyo; kukiwa
na sababu za kuachana nae ni vema kuachana kwa wema.
Nasema hivi kwa kuwa
wapo watu ambao huwa katika ndoa ambazo hawana furaha, bali hufanya hivyo kwa
kuwa tu wana watoto, jamii inawasukuma au familia ndiyo inayolazimisha watu hao
kuwa katika ndoa.
Hivyo unapogundua mwenza
wako amebadilisha mwenendo wake ni vema mkakaa chini na kuzungumza kuhusu
mustakabali wa ndoa yenu badala ya kugombana bila ya kujua tatizo.
Kwa maana kuna mambo
katika mahusiano huwa yanamalizwa kwa mazungumzo na si kugombana, hili
litasaidia kuepusha matatizo ya kiafya na kiakili yanayoletwa na majuto baada
ya talaka za kulazimisha.
HAFIDH KIDO
DAR ES SALAAM, TANZANIA
30/07/2012
No comments:
Post a Comment