Sunday, July 29, 2012

Taarifa za wabunge dhidi ya Serikali zisichukuliwe kisiasa.





Na Hafidh Kido

Wiki chache zilizopita bunge la Tanzania liliwaka moto baada ya mbunge machachara wa chama cha demokrasia na maendeleo (CHADEMA), kuwasha moto kuhusiana na uteuzi wa majaji wapya watakaoongoza mahakama za Tanzania kutoa haki.

Tundu Lissu, alimshambulia Rais Jakaya Kikwete, kuwa anafanya uteuzi huo ‘kishkaji’ kwa lengo la kulipa fadhila kwani wengi wa majaji hao hawana sifa wala uwezo wa kuongoza kesi hapa nchini. Kauli hiyo ilitolewa wakati Lissu akiwasilisha maoni ya kambi rasmi ya upinzani katika hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi wizara ya katiba na sheria; ambapo alieleza kuwa katika historia ya nchi hii Rais Kikwete ndie Rais pekee alieteua majaji wengi kuliko marais waliomtangulia.

Lakini suala hilo lilipokewa kwa malalamiko kutoka kwa wadau wa sheria wakiwemo majaji waandamizi na baadhi ya viongozi wa juu wa Serikali wakimshutumu mbunge huyo kuwa hajui anachosema na ni mropokaji tu. Badala ya kukaa chini na kufanya upembuzi yakinifu juu ya tuhuma hizo wengi waliishia kulaumu badala ya kupinga ama kutoa muelekeo mbadala juu ya madai hayo.

Yote hii inaonyesha ni namna gani viongozi wa Serikali iliyo madarakani ni wazuri sana wa kukosoa kuliko kusikiliza hoja na kuzitolea majibu yanayofaa. Haisaidii chochote zaidi ya kuendelea kudumaza akili za watanzania na kuwaaminisha kuwa kila kinachosemwa na mbunge wa upinzani ni ujinga na uchochezi.

Kwa upande wangu madai ya Tundu Lissu, yalikuwa ni ya msingi na alikuwa na ushahidi wa kutosha kuweza kufanyiwa kazi ili kuondoa matatizo ambayo yanaweza kuikumba nchi katika siku za usoni. Maana lazima tuache kushabikia maamuzi ama uteuzi unaofanywa kwa faida za kisiasa; Rais ni mtu wa kupita tu na baadae anatuachia balaa sisi watu wa chini.

Kwa kutumia ibara ya 109 (6) katiba ya Tanzania ambayo inaeleza kuwa mtu anaweza kuteuliwa jaji wa mahakama kuu ikiwa ana sifa maalum ama amekuwa na mojawapo ya sifa maalum kwa muda usiopungua miaka kumi.

Lissu hakufanya hiyana bali alizitaja sifa hizo kuwa ni mtu aliye na shahada ya sheria kutoka chuo kikuu kinachotambulika na mamlaka ya ithibati nchini na amewahi kuwa hakimu, amefanya kazi katika utumishi wa umma akiwa na sifa za kufanya kazi ya uwakili au ni wakili wa kujitegemea.

Kimsingi si marais wote wanakuwa na taaluma ya sheria, hivyo hawana ufahamu wa sheria na katika uteuzi wa majaji taratibu zinamruhusu kukaa na mwanasheria mkuu wa Serikali  na viongozi wakuu waandamizi wa mahakama kuu ya Tanzania ili kupata ushauri wa namna ya kuteua majaji.

Mbunge huyo alilibainishia bunge kuwa anao ushahidi kuwa utaratibu huo haufuatwi kuteua majaji na kudai watu wengi wanateuliwa kuwa majaji wakati hawajawahi kupendekezwa na tume ya utumishi wa mahakama hivyo kukosa nafasi ya kufanyiwa ‘vetting’ yoyote na mamlaka hiyo ya kikatiba juu ya uwezo na kupimwa akili.

Mbali na hayo Lissu alilibainishia bunge kuwa anao ushahidi juu ya athari za majaji wanaoteuliwa bila ya kufuata taratibu, lakini majibu ya Serikali ni kukaa kimya na kumuona Tundu Lissu, ni mropokaji anaetafuta umaarufu wa kisiasa. Badala yake ilitakiwa mahakama ambayo ni muhimili unaojitegemea kuyachukulia hatua maneno hayo na kuona kama ushauri unaofaa badala ya kuendelea kuendekeza chuki za kisiasa katika mambo ya msingi.

Kama hiyo haitoshi, katika bunge hilihili la bajeti mbunge wa jimbo la Ubungo John Myinka, alipata kusema kuwa Rais Kikwete ni dhaifu na bunge limetawaliwa na uzembe na ndiyo maana nchi imefika hapa tulipo.

Kwa haraka utaona ni matusi ama maneno yaliyokosa busara, nilichofurahishwa na mbunge huyo kijana ni kupinga kufuta kauli yake hata baada ya kuambiwa na naibu Spika wa Bunge Job Ndugai, kuwa kauli yake hiyo itamgharimu kutolewa nje ya ukumbi wa bunge kama adhabu.

Lakini Mnyika alisimama na kuomba apewe nafasi ya kufafanua kauli yake lakini naibu Spika aliendelea kumtaka kufuta kauli yake kitu ambacho mbunge huyo alipinga na kuamua kukubali kutoka nje.

Lakini siku za nyuma mbunge wa chama cha mapinduzi Iramba magharibi Mwigulu Nchemba, alipata kutoa kauli tata bungeni lakini hakuchukuliwa hatua yoyote zaidi ya kupongezwa na wabunge wa chama chake.

Mwigulu wakati akichangia bajeti aliwaambia wabunge wa upinzani ni wanafiki, waongo, wana mapepo na wanapaswa kuombewa na kupimwa akili. Utaona ni namna gani bunge letu limekuwa likifumbia macho baadhi ya kauli na kuzitilia mkazo baadhi ya kauli, hii ni hatari.

Mambo ya kudharau taarifa zinazotolewa na wabunge machachari zimepata kuigharimu nchi yetu mpaka kufikia baadhi ya mawaziri kujiuzulu. Itakumbukwa katibu mkuu wa sasa chama cha chadema Dk Wilbord Slaa, alipata kulieleza bunge juu ya sakata la akaunti ya malipo ya nje (EPA), rushwa ya ujenzi wa majengo pacha ya benki kuu ya Tanzania, na sakata la Richmond.

Lakini mbunge huyo alionekana ni mropokaji na anatafuta umaarufu, Serikali ililifumbia macho suala hilo mpaka maji yalipowafika shingoni matokeo yake zikaundwa tume ambazo ziliigharimu serikali mamilioni ya fedha mpaka watuhumiwa walipotiwa mikononi.

Matokeo ya tume yakaiyumbisha Serikali na kumsababishia usumbufu mkubwa ndugu Rais baada ya waziri wake mkuu kujiuzulu kutokana na kashfa ya Richmond na kuamua kulivunja baraza. Hakika kulivunja baraza la mawaziri ni usumbufu mkubwa sana, maana inakupasa kuwaondoa hata wale ambao walikuwa ni wachapa kazi hodari katika kulinda maslahi ya umma.

Kimsingi bunge la sasa limebadilika sana limekuwa ni bunge la vurugu, visasi na kulinda maslahi ya vyama. Makundi yanajengwa ili kulinda maslahi binafsi, haiingii akilini kuona mbunge anaitetea Serikali kana kwamba yeye ni miongoni mwa mhimili huo wa dola.

Labda niwakumbushe tu kuwa bunge ni mhimili kamili wa dola unaojitegemea katika maamuzi yake ambayo Rais hapaswi kuyatilia shaka hata kama wabunge hao humuita mwenyekiti pindi wanapokutana katika vikao vya chama. Mihimili mitatu ya dola ni Serikali, Mahakama na Bunge, sasa inakuwaje kimoja kinasimamia kazi ya kingine?

Mawaziri wao hawana neno, maana kazi yao kubwa ni kumsimamia bosi wao, na kadiri waziri anavyokuwa na vituko katika kupinga hoja za wabunge ndivyo anavyoonekana ni mzuri na anaijua kazi yake. Kifupi hii ni dunia ya propaganda na kutetea hata pasipofaa kutetea.

Tazama waziri wa sera uratibu na bunge William lukuvi, anavyotetea hata uozo, mimi sipingani nae hata kidogo. Kwa wakati ule anapaswa kuonekana hashindwi na Serikali haikosei, lakini si wakati wote hasa anapoondoka bungeni na kurudi ofisini anapaswa kufanya majumuisho ya yale aliyoyapata kutoka kwa wabunge na kuyafuatilia kwa karibu. Hata anapotoa ripoti zake kwa waziri mkuu, maana wizara hii ipo chini ya ofisi ya waziri mkuu, basi amueleze ukweli wa mambo na wajipange kuyachukulia hatua mabaya waliyoyasikia kutoka kwa wabunge.

Wabunge ni wawakilishi wa watanzania wote, kimsingi ukumbi wa bunge ni mdogo sana hautoshi watanzania milioni 40 kuingia wote kwa wakati mmoja, lakini wamechaguliwa wachache kuenda kutuwakilisha. Maana yake wanachokizungumza wabunge iwe wa upinzania ama wa chama tawala ni sauti za watanzania hazipaswi kupingwa kirahisi rahisi tu na kuzodolewa na wabunge wa chama tawala kana kwamba wao hawawakilishi sauti za watanzania.

Ipo haja wabunge kukaa chini na kupewa sema juu ya uwakilishi wao bungeni, maana inafika wakati unajiuliza hivi hawa wabunge wanaowakosoa wenzao wa upinzani hawana majimbo? Ama wao wametumwa na wananchi kuenda kuitetea Serikali ama vipi.

Tafadhali nisionekane ni mpinzani wa Serikali, hapana bali hata Serikali yenyewe inatambua umuhimu wa wapinzani na ndiyo maana wakatengeneza Serikali kivuli ambayo ina mawaziri vivuli kazi yao ikiwa ni kukosoa muenendo wa wizara husika. Kiongozi mkuu wa upinzani kazi yake ni kuangalia muenendo wa waziri mkuu na kumkosoa inapowezekana.

Hatulengi kutengeneza Serikali yenye mizozo lakini pia hatutaki kuona wabunge ambao tulitegemea watasimama upande wetu wanaanza kusigana wenyewe kwa wenyewe. Tuhakikishe wabunge wanapoingia katika ukumbi ule wanaacha itikadi zao za vyama nje ya ukumbi na kuingia mule wakiwa ndugu ambao wataishambulia Serikali ili kuweza kuleta maisha bora kwa kila mtanzania.

Katika azimio la Arusha baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, alisisitiza sana mtu kuwa na kazi moja, kama wewe ni mbunge basi ubaki na ubunge wako na si vinginevyo. Lakini Serikali ya chama cha mapinduzi inakosea sana pale inapowapa kazi zaidi ya moja wabunge wao, utaona wabunge wengi ni wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM, hivyo usitegemee kina Mwigulu Nchemba kuwa tofauti na Serikali wakati yeye ni mkurugenzi wa fedha katika chama kinachoongoza Serikali hiyo.

Ifike wakati wabunge wetu wawe na huruma na wananchi waliowatuma, na serikali nayo ihakikishe inapopewa taarifa na wabunge wasizipuuze bali wazifanyie uchunguzi na ikiwezekana kuzichukulia hatua. Wasisubiri mpaka maji yamewafika shingoni ndipo waanze kuchukua hatua wakiwa na mihemko ya kujisafisha badala ya kutenda haki.

Wajifunze katika matukio ya Richmond, EPA, na majengo pacha ya BOT namna walivyopata tabu kuchukua hatua wakati suala limefika pabaya. Ipo haja ya kuangalia mambo kwa kina kutokana na uzito wake na si kuangalia nani ameyasema bali uzito wake kwa maslahi ya taifa.
Mwisho.    

0752 593894
www.kidojembe.blogspot.com

  


No comments:

Post a Comment