Saturday, July 28, 2012

Wabunge waanza kumsafisha Lowassa...


Na Mwandishi Wetu, Dodoma .Mbunge wa Monduli,
Edward Lowassa

*Wasema Kamati ya Mwekyembe ilipotosha
 
*Lugola, Ally Kessy wamuumbua ole Sendeka
*Wazima mpango kumng’oa Muhongo, Maswi

HATIMAYE wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wameibuka na kumsafisha
Waziri Mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, huku wakidai taarifa ya Kamati
teule iliyokuwa ikiongozwa na Waziri wa sasa wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ilijaa upotoshaji.


Sakata hilo, lilibuka juzi usiku, katika kikao cha Wabunge wa CCM, ambacho
 
kilikuwa kinajadili tatizo la umeme, hali iliyomfanya Mbunge wa Simanjiro,
Christopher Ole Sendeka (CCM), kuibuka na na hoja ya kutaka viongozi wa
wizara hiyo wawajibishwe.

Hoja ya Sendeka, ilimlenga Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter
 
Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliakim Maswi, wawajibishwe kwa
kukiuka Sheria ya Manunuzi ya Umma.

Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya kikao hicho, kilisema
 
kuwa hoja hiyo ya Ole Sendeka, ilionekana ni mwiba kwake, hali iliyomfanya
Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), kunyanyuka na kumuumbua ole Sendeka.

Lugola, alisema alifuatwa na Ole Sendeka, huku akiahidi kumhonga fedha ili
 
aweze kumuunga mkono hoja yake ya kutaka Waziri wa Nishati na Madini,
Profesa Sospeter Muhongo na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Eliachim Maswi,
wawajibishwe na Bunge.

“Hoja ya Ole Sendeka, ilimfanya Kangi Lugola kunyanyuka na kuanza kutoa
 
maelezo ambayo kulikuwa na lengo la kutaka kukwamisha bajeti ya Wizara ya
Nishati na Madini. Alipinga wazi kuwawajibisha viongozi wa wizara hiyo,
huku akifananisha kinachotaka kufanywa ni sawa na lililomtokea Lowasa.

“Alisema katika ripoti ile ya kamati teule ya Bunge, ilipelekea
 
kumwajibisha Lowassa na baada ya muda iligundulika ilijaa upotoshaji mwingi
na kusisitiza katu wabunge hawapo tayari kurudia makosa ya mwaka 2008,
ambapo vilitolewa vielelezo vya mitaani,” alisema mtoa habari huyo.

Baada ya maelezo ya Lugola, naye Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango
 
(CCM), aliunga mkono hoja hiyo na kusema kuwa mwaka 2008, Bunge
liliaminishwa Lowassa, alikuwa mhusika na Richmond, kutokana na jambo hilo
kukosa ushahidi alitahadharisha kutorudiwa kwa makosa tena.

“Kilango, alisema wabunge waliamini alikula fedha kwa kulipwa na Richmond,
 
lakini hakuna ukweli, hivyo hakuna sababu ya kumwajibisha Waziri wa Nishati
wala Katibu Mkuu wake.

“Baada ya hapo aliinuka Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy Mohammed
 
(CCM), ambaye alisema katu hayuko tayari kuunga mkono hoja ya Ole Sendeka,
kwani tangu alipondolewa Lowasa katika nafasi ya uwaziri mkuu nchi imekuwa
ikiyumba.

“Mjadala ulikuwa mkali ndugu yangu, Mbunge wa Ludewa, Deo Filikunjombe
 
(CCM), alisema wabunge hawako tayari kurudia makosa ya Richmond, hatakuwa
tayari kuubariki mpango huo aliouita mchafu,” kilisema chanzo hicho.

Awali kabla ya kikao hicho, Kamati ya Nishati na Madini iliamua kuunda tume
 
maalum ya kumchunguza Maswi kwa tuhuma za kukiuka Sheria ya Manunuzi ya
Umma.

Maswi, anadaiwa kukiuka sheria hiyo, wakati akitoa zabuni ya ununuzi wa
 
mafuta ya kuzalisha umeme wa dharura katika Kampuni ya Puma, ambayo ilipewa
vibali vya kuiuzia Serikali lita milioni 9 mwaka 2011 na lita nyingine kama
hizo mwaka huu.

Habari za kuaminika zilizopatikana jana kutoka mkoani Dodoma zinasema,
 
hatua ya kuundwa kamati ndogo imetokana na kikao kilichoitishwa na Waziri
Mkuu, Mizengo Pinda, kikiwa na nia moja tu ya kumaliza mpasuko uliopo.

“Kikao cha Waziri Mkuu na wabunge wa CCM, kilikumbwa na mambo mengi mno,
 
mojawapo ni kutaka kuona Maswi anawajibishwa haraka iwezekanavyo.

“Lakini hoja hiyo, ilionekana kupingwa na Waziri Mkuu na baadaye alikubali
 
iundwe kamati ndogo ya kumchunguza Maswi na maazimio yote
yatakayowasilishwa serikalini au bungeni, yatafanyiwa kazi mara moja,

“Nakwambia kauli ya Pinda, ilionekana wazi kupoza machungu ya wabunge, yeye
 
alionekana kuwa muwazi kwa kuwaahidi kuwa kila pendekezo dhidi ya Maswi,
litafanyiwa kazi barabara.

“Unajua Kamati ya Nishati na Madini haijafurahishwa kabisa na mwenendo
 
uliopo pale kwa Maswi, inaonekana kuna mambo yanakwenda shaghala baghala
tu.”

Habari za uhakika ambazo MTANZANIA ilizipata kutoka ndani ya kikao hicho,
 
zinasema Pinda alikiri waziwazi kuwa Maswi ameteleza katika uamuzi wake
aliochukua.

“Katika kuonyesha kwamba hakuridhika na hali hiyo, Pinda alikiri kuwa Maswi
 
amefanya makosa kwa sababu wakati anaunda tume kufanya uchunguzi pale
TANESCO, Ofisi ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG),
haikujulishwa.

“Hata CAG alimwambia Pinda kwamba ripoti yoyote kuhusu TANESCO, ikipelekwa
 
kwake hataitambua na anashangaa mno kutohusishwa kwenye uchunguzi huo.

“Kulikuwa na mvutano mkubwa mno, pale Mbunge wa Simanjiro, Christopher ole
 
Sendeka (CCM) aliposimama na kutoa msimamo wake. CHANZO: Mtandao wa wanabidii

No comments:

Post a Comment