Timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri chini ya miaka 20
(Ngorongoro Heroes) imeahidi ushindi kwenye mechi yake dhidi ya Nigeria (Flying
Eagles) itakayochezwa kesho (Julai 29 mwaka huu).
Mechi hiyo ya kwanza ya
raundi ya pili kutafuta tiketi ya kucheza fainali za Afrika kwa vijana wenye
umri huo zitakazofanyika mwakani nchini Algeria
itachezwa kwenye Uwanja wa Taifa, Dar
es Salaam kuanzia saa 10 kamili jioni.
Akizungumza kwenye
mkutano na Waandishi wa Habari uliofanyika leo (Julai 28 mwaka huu) ofisi za
TFF, Kocha Mkuu wa Ngorongoro Heroes, Jakob Michelsen na nahodha wake Omega
Seme wamesema timu yao iko tayari kwa mechi hiyo itakayochezeshwa na waamuzi
kutoka Kenya.
Michelsen amesema timu
yake imepata mechi mbili za kujipima nguvu dhidi ya Rwanda ,
lakini pia aliishuhudia Flying Eagles ikicheza mechi ya kirafiki na Rwanda (Young Amavubi) uliofanyika Julai 24
mwaka huu jijini Kigali .
“Timu iko vizuri na
wachezaji kama Frank Domayo, Simon Msuva na
Ramadhan Singano ambao pia wanachezea timu A (Taifa Stars), hivyo uzoefu wao ni
muhimu kwa mechi ya kesho.
“Nigeria ni mabingwa watetezi wa michuano hii kwa
hiyo tunatarajia upinzani mkubwa, lakini tumejiandaa kwa hilo . Nigeria ni nchi yenye mfumo mzuri
wa timu za vijana, na sisi tunaelekea huko huko” amesema Michelsen.
Naye Kocha Mkuu wa
Flying Eagles, John Obuh amesema haijui vizuri Ngorongoro Heroes lakini
anaiheshimu kutokana na ukweli kuwa inacheza raundi ya pili baada ya kuitoa Sudan katika
raundi ya kwanza.
“Sina mchezaji yeyote
anayecheza mpira wa kulipwa nje ya Nigeria , lakini tumekuja kushinda
ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kucheza raundi ya mwisho na hatimaye
tucheze fainali mwakani,” amesema Obuh aliyefuatana na nahodha wake Samuel Okan
ambaye ni mlinda mlango.
Viingilio katika mechi
hiyo itakayochezeshwa na mwamuzi Moses Osano ni sh. 3,000 kwa viti vya rangi ya
chungwa, bluu na kijani wakati VIP B na C itakuwa sh. 5,000. Kiingilio kwa VIP
A ni sh. 10,000.
Osano atasaidiwa na
Peter Keireini na Elias Wamalwa wakati mwamuzi wa mezani (fourth official) ni
Thomas Onyango. Kamishna wa mechi hiyo atakuwa Charles Masembe kutoka Uganda .
CAF YAMTEUA HAFIDH ALI
KUSIMAMIA MECHI YA WASUDAN
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Afrika (CAF) limemteua mwamuzi wa zamani wa kimataifa wa Tanzania , Hafidh Ali kuwa Kamishna wa mechi kati
ya El Ahly Shandy na Al Hilal zote za Sudan .
Shandy ndiyo mwenyeji wa
mechi hiyo namba 98 ya Kombe la Shirikisho itafanyika Agosti 5 mwaka huu na
itachezwa Uwanja wa Shandy ulioko katika mji wa Shandy.
Mwamuzi wa mechi hiyo ni
Raj Seechun kutoka Mauritius
ambaye atasaidiwa na Balkrishna Bootun, Jean Daniel Telvar na Parmendra Nunkoo,
wote pia kutoka Mauritius .
Mratibu Mkuu wa mechi hiyo ni Paul Bassey wa Nigeria .
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment