Wanafunzi wakicheza baada ya walimu wao kugoma.
WALIMU WAGOMA KILA KONA,
WANAFUNZI NAO WACHACHAMAA, SERIKALI YAONYA, YATISHIA KUWAFUTIA MISHAHARA
NCHI imetikiswa. Mgomo
wa walimu ulioanza jana katika sehemu mbalimbali nchini, umeathiri kwa kiasi
kikubwa sekta ya elimu huku kukiwa na taarifa za matukio yasiyokuwa ya kawaida
yaliyoambatana na mgomo huo usio na ukomo.
Katika sehemu mbalimbali
nchini, walimu waliripotiwa kugoma kwa kutoingia madarasani na wengine walifika
kazini na kusaini vitabu vya mahudhurio kisha kuondoka hali iliyosababisha
wanafunzi kurandaranda ovyo katika sehemu za miji iliyo karibu na shule hizo.
Mjini Dodoma ,wabunge
jana walimbana Naibu Spika, Job Ndugai wakitaka shughuli za Bunge zisitishwe
ili kujadili mgomo wa walimu ambao umeanza rasmi jana nchi nzima, na kuziacha
shule nyingi zikiwa na walimu wakuu na wakuu wa shule pekee.
Hata hivyo, Ndugai
alisema Bunge lisingeweza kujadili suala hilo kwani tayari Serikali ilikuwa
imelifikisha mahakamani baada ya kushindwa kuafikiana na walimu katika ngazi ya
usuluhishi.Wakati hayo yakiendelea, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk
Shukuru Kawambwa amesema Serikali itafuta mishahara kwa walimu walioitikia
mwito Chama cha Walimu Tanzania (CWT) wa kushiriki mgomo ambao alisema siyo
halali.
Katika mkutano wake na
waandishi wa habari Dar es Salaam
jana, Dk Kawambwa pia aliwaonya walimu ambao alisema wamekuwa wakiwabughudhi
wenzao ambao waliamua kwenda kazini.
Kwa upande wake, Naibu
Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo akiwa Mjini Morogoro
aliwaagiza wakuu wa shule za msingi na sekondari mkoani humo kuandaa orodha ya
majina ya walimu wasiofika kazini Julai 30 na waifikishe kwa maofisa elimu wa
wilaya kabla ya saa 2:00 asubuhi ya Julai 31.
Waandishi wetu katika
sehemu mbalimbali nchini pia waliripoti kwamba katika baadhi ya shule,
wanafunzi waliruhusiwa kurejea nyumbani mapema kwa maelezo kwamba hakukuwa na
masomo.Hali hiyo ilizua kizaazaa kwani katika baadhi ya mikoa wanafunzi
walicharuka na kuitisha maandamano hadi katika ofisi za maofisa elimu wa
wilaya, wakitaka Serikali iingilie kati mgomo huo ili waendelee kusoma.
Kadhalika, baadhi ya
viongozi na watendaji wa Serikali walinukuliwa wakitoa matamko ya kuwasihi au
kuwaamuru walimu warejee madarasani, kauli ambazo hata hivyo, hazikubadili
uamuzi wa walimu hao.
Wanafunzi waandamana
Maandamano ya wanafunzi
yaliripotiwa katika Mji wa Tunduma, Mbeya ambako polisi walitumia mabomu ya
machozi kuwadhibiti wanafunzi.
Wanafunzi wa shule
mbalimbali za msingi katika Wilaya ya Mbozi mkoani humo waliandamana wakidai
haki ya kufundishwa. Hata hivyo, maandamano hayo yaliingiliwa na vibaka ambao
baadaye walivunja ofisi za Halmashauri ya Mji wa Tunduma na kuiba mali kadhaa
kisha kuchoma nyaraka zilizokuwemo.
Tukio hilo lilitokea asubuhi wakati wanafunzi wa
shule 14 za msingi zilizopo katika halmashauri ya Tunduma walipojikusanya na
kufanya maandamano hadi nyumbani kwa diwani na baada ya kumkosa walielekea
kituo cha polisi na baadaye ofisi katika hizo.
No comments:
Post a Comment