Saturday, July 28, 2012

Chadema wakosa Meya jijini Mwanza...

Huyu ndie bwana Manerere akitia huruma.


Meya wa Jiji la Mwanza, Josephat Manyerere ameng’olewa katika wadhifa wake huo baada ya madiwani wenzake kumpigia kura ya kutokuwa na imani naye kutokana na kile walichodai kwamba ameshindwa kutimiza majukumu yake kikamilifu.

Uamuzi wa kumng’oa meya huyo ambaye ni diwani wa Kata ya Nyakato kwa tiketi ya Chadema ulitangazwa jana na Naibu wake, Charles Chinchibela, ambaye alisema wamefikia hatua hiyo baada ya Meya Manyerere kupewa nafasi ya kujitetea mbele ya Baraza la Madiwani kuhusiana na tuhuma 11 zilizokuwa zikimkabili.

Alizitaja baadhi ya tuhuma hizo kuwa ni kushindwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa majukumu katika Halmashauri, kutoitisha vikao halali kwa madai kuwa hakuna kikao kinaweza kufanyika bila yeye (Meya) kuwepo.

Kwa mujibu wa Naibu Meya huyo, tuhuma nyingine ni pamoja na kusaini mikataba kabla ya kupitishwa na Baraza la Madiwani, kukataa kusaini mikataba halali ambayo imepitishwa na Halmashauri ya jiji, kuipendelea Kata yake katika miradi ya maendeleo, kutumia madaraka yake vibaya na  kushindwa kuwaunganisha madiwani hali ambayo imesababisha kudorora kwa mahusiano kati ya madiwani na watendaji.

Aliongeza kwamba kuwa baada ya Meya kujieleza madiwani walipata nafasi ya kupiga kura ambapo madiwani 20 walipiga kura ya kutokuwa na imani naye huku madiwani wanane tu waliopiga kura ya kutaka aendelee na wadhifa wake huo.

Chinchibela alisema kwamba jumla ya madiwani 28 kati ya 33 walihudhuria kikao hicho na kupiga kura ambapo hakuna kura iliyoharibika.

Akizungumzia hatua hiyo ya mawadiwani wenzake kumng’oa madarakani, Meya Manyerere alisema kuwa ameipokea kwa moyo mkunjufu, na kwamba anawashuruku kwa ushirikiano waliompatia kwa kipindi chote alicholiongoza Jiji la Mwanza kama meya.




 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment