Sunday, July 29, 2012

Usimtukane mamba kabla hujavuka mto....


TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya umri wa miaka 20, Ngorongoro Heroes leo imeanza vibaya kampeni za kuwania kucheza Fainali za Afrika kwa vijana wenye umri huo, zitakazofanyika nchini Algeria mwakani, baada ya kufungwa na Nigeria mabao 2-1, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hadi mapumziko, Nigeria, Flying Eagles walioonekana kutumia wachezaji waliozidi umri, walikuwa mbele kwa mbele kwa mabao 2-0 katika mchezo huo wa kwanza wa Raundi ya pili, yote yakitiwa kimiani na mshambuliaji wa Enugu Rangers, Achaji Gero katika dakika ya pili na 44.

Kipindi cha pili, Ngorongoro walibadilika na kucheza vizuri, wakiwazidi wapinzani wao kumiliki mpira na kasi ya mchezo na hatimaye wakafanikiwa kupata bao la kufutia machozi, lililofungwa na Atupele Green dakika ya 50, akimalizia krosi ya Ramadhani Singano ‘Messi’.

Ngorongoro wangeweza kupata mabao zaidi, kama wangecheza soka ya chini, lakini kutia krosi za juu kwenye lango la Nigeria ilikuwa ni kuwatesa washambuliaji wao wafupi, Atupele na Simon Msuva.

Kwa matokeo hayo sasa, Ngorongoro wanahitaji ushindi wa angalau wa mabao 2-0 katika mchezo wa marudiano Nigeria wiki mbili zijazo, ili kusonga mbele.

Baada ya mchezo huo, kocha wa Ngorongoro Heroes, Mdenmark Jakob Michelsen alisema kwamba ataongeza nguvu katika kikosi chake kwa kuwaita wachezaji wawili wanaocheza nje, kiungo Adam Nditi wa Chelsea na Thomas Ulimwengu wa Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), sambamba na nyota wengine waliokwenda Ujerumani n TSU kwenye michuano ya Fallerhof.

Katika mchezo, kikosi cha Ngorongoro kilikuwa; Barwany Khomein, Omega Seme, Jamal Mroki, Issa Rashid, Ruhana Samir, Yarouk Ramadhan, Kheri Salum/Jerome Lambele, Frank Damayo, Simon Msuva, Atupele Green na Ramadhan Singano.

Flying Eagles; Samuel Okani, Hassan Abubakar, Ahiyu Mohamed, Ikechukwu Okine, Chizoba Amaefule, Agboyi Oubokha, Moses Orkuma, Chidi Osochukwu, Yahaya Adam/Harrison Egbune, Achaji Gero na Aminu Omar/Uchw Agbo. 

Picha kwa hisani ya mdau Dina Ismail wa : http://dinaismail.blogspot.com



No comments:

Post a Comment