KUHUSU KUFUNGIWA KWA
MWANAHALISI
Chama Cha Demokrasia na
Maendeleo (CHADEMA) kinalaani uamuzi wa Serikali inayoongozwa na Chama Cha
Mapinduzi (CCM) kulifungia kwa muda usiojulikana gazeti la MwanaHalisi kwa
kutumia mwanya wa sheria mbovu ya magazeti inayokwenda kinyume na haki za
binadamu na utawala bora.
CHADEMA kinaitaka
Serikali kulifungulia gazeti hilo
haraka iwekanavyo na kimewasiliana na Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni
inayoongozwa na CHADEMA kuchukua hatua za kibunge kuisimamia Serikali
kurekebisha udhaifu huo ikiwa inaheshimu uhuru wa habari na inazingatia maslahi
ya taifa.
CHADEMA kinatafsiri
hatua hiyo ya Serikali ya kufungia gazeti la MwanaHalisi kuwa ni sawa na
kufungia uhuru wa kusambaza habari, uhuru wa kupokea habari na uhuru wa kutoa
maoni, hivyo tunatoa mwito kwa wananchi na wadau wote wa habari kuungana pamoja
kupinga hatua hiyo, na CHADEMA kitaeleza hatua za ziada za kuchukuliwa iwapo
Serikali haitasikiliza kauli za wadau wa habari juu ya suala hili.
CHADEMA kinatambua kuwa
uamuzi wa Serikali kufungia gazeti hilo kwa mara nyingine tena ni kwenda
kinyume na haki za binadamu, kinyume na utawala bora na ni kikwazo kwa
demokrasia na maendeleo nchini.
CHADEMA kinapinga hatua
ya Serikali ambayo viongozi na watendaji wake wakiwa wametajwa kama watuhumiwa
katika habari zilizoandikwa na gazeti hilo
imetumia mamlaka haramu ya Waziri mwenye dhamana ya sekta ya habari kugeuka
mlalamikaji, mwendesha mashtaka na mfungaji huku ikipuuza taasisi za kusimamia
uwajibikaji na haki.
CHADEMA ilitarajia
badala ya kulifungia gazeti la MwanaHalisi ingewezesha kufanyika kwa uchunguzi
huru kufuatia habari za kiuchunguzi zilizoandikwa na gazeti hilo juu ya
watendaji na watumishi wa Serikali kuhusishwa na jaribio la mauji ya Dr
Ulimboka Steven, kupanga njama za mauji ya viongozi wa CHADEMA na matukio
mengine ambayo yenyewe ndiyo yenye mwelekeo wa kufanya wananchi wapoteze imani
na vyombo vya dola hali ambayo inaweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo
nchini.
CHADEMA kinalinganisha
uamuzi huo wa Serikali uliotangazwa tarehe 30 Julai 2012 na Msajili wa Magazeti
chini ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kuwa ni sawa
kujichukulia sheria mikononi kwa kuwa Serikali yenye kuheshimu misingi ya asili
ya haki ingezingatia kwamba ikiwa chombo chochote cha habari kimedaiwa kuvunja
sheria ama kukiuka maadili dhidi ya Serikali, viongozi wake ama watu binafsi
mashtaka au malalamiko yangepelekwa kwa taasisi zinazohusika mathalani Baraza
la Habari (MCT) au mahakama.
CHADEMA kinafahamu kuwa
Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda usiojulikana gazeti la
MwanaHalisi, kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976, kifungu Na. (25)
(i); hata hivyo uamuzi huo ni kinyume cha misingi ya asili ya utawala wa
sheria.
CHADEMA kinaelewa kwamba
zipo sheria nyingine katika nchi yetu ambazo Serikali ingeweza kuzitumia
kushughulikia madai iliyoyatoa kuwa Gazeti la Mwanahalisi limeandika habari na
makala za uchochezi, uhasama na uzushi kupitia mahakama lakini imeamua kwa
makusudi kuendelea kutumia sheria mbaya isiyokuwa na uhalali wa kihaki (illegitimate).
CHADEMA kinakumbusha
kuwa kwamba Sheria hiyo ni kati ya Sheria zilizotajwa na Tume ya kukusanya
maoni juu ya mfumo wa vyama vingi (Tume ya Nyalali) kuwa ni sheria mbaya miaka
20 iliyopita kuwa na Sheria mbaya na Serikali imekuwa ikikwepa kutunga sheria mpya
pamoja na wadau wa habari kuandaa miswada ya sheria ya huduma za vyombo vya
habari na uhuru wa taarifa kwa nyakati mbalimbali.
CHADEMA kinatoa mwito
kwa wananchi na taasisi zote za kitaifa na kimataifa kufuatilia kwa karibu
tukio hili la kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi na matukio mengine ya hivi
karibuni kuhusu asasi za kiraia, makundi mbalimbali katika jamii ikiwemo
madaktari na vyama vya siasa hususan CHADEMA yenye kuashiria kwamba Serikali
inayoongozwa na CCM imeanza mkakati wa kuficha ukweli na kudhibiti mabadiliko
kwa kutumia sheria kandamizi, vyombo vya dola na njia nyingine haramu.
Hivyo, ieleweke kwamba
hatua hii dhidi ya Gazeti la MwanaHalisi ni mwanzo tu wa hatua zingine zaidi
dhidi ya magazeti mengine na taasisi nyingine hali ambayo inahitaji wananchi na
wadau wote kuunganisha nguvu za pamoja katika kuchukua hatua za haraka
kuinusuru nchi na mwelekeo huo.
Imetolewa tarehe 30
Julai 2012 na:
John Mnyika (Mb)
Mkurugenzi wa Habari na
Uenezi
No comments:
Post a Comment