Kwa niaba ya Baraza la
Vijana wa CHADEMA (BAVICHA) tukiwa ni sehemu ya wadau wa sekta ya habari
nchini, tunaunga mkono maandamano ya amani mliyoitisha ya kupinga hatua ya
serikali kulifungia gazeti la MwahaHALISI.
Tunawapongeza wahariri
kwa mshikamano wenu katika kipindi hiki cha majaribu; endeleeni kusimama
pamoja, ni umoja wenu ndio utakaokuwa kinga ya pamoja dhidi mtu au chombo
chombo chochote kinachoingilia uhuru wenu. Mshikamano wenu ni ishara ya
kushindwa kwa mkakati wa ‘wagawe uwatawale’ na imani kwamba umoja ni nguvu.
Wahariri wote hawapaswi kukaa kimya kuhusu kufungiwa kwa MwanaHALISI kwa kuwa
leo ni kwa gazeti hilo, kesho itakuwa kwa gazeti lingine; hivyo ni vyema
kuungana pamoja kulinda uhuru, taaluma na sekta ya habari nchini.
Kwetu sisi hatua hiyo ya
serikali tunaitafsiri zaidi ya kufungia gazeti la MwanaHALISI; ni hatua ya
kufungia uhuru wa kusambaza habari na uhuru wa kupokea habari. Hivyo hatua hiyo
ni kinyume cha haki za binadamu, kinyume cha utawala bora na ni kikwazo kwa
demokrasia na maendeleo. Hakika serikali na viongozi wake wamevuka mstari wa
kukubali kukosolewa na sasa wameamua kuanza kufungia uhuru wa fikra mbadala.
Hatua ya Waziri mwenye
dhamana na sekta ya habari kugeuka mlalamikaji, mwendesha mashtaka na mfungaji
ni mwelekeo mbovu wa kupuuza taasisi za kusimamia uwajibikaji na haki. Uamuzi
uliofanywa na serikali hauna tofauti na unaofanywa na raia wanaojichukulia
sheria mikononi(mob justice). Kwa serikali inayoheshimu misingi ya asili ya
haki, tulitarajia chombo chochote cha habari, kikivunja sheria ama kukiuka
maadili dhidi ya serikali, viongozi wake ama watu binafsi mashtaka ama
malalamiko yangepelekwa kwa taasisi zinazohusika mathalani Baraza la
Habari(MCT) ama Mahakama.
Hatua ya serikali
kufungia gazeti la MwanaHALISI pamoja na kuwa imechukuliwa kwa mujibu wa sheria
iliyopo, imekiuka misingi ya asili ya utawala wa sheria. Kwani kulikuwa na
sheria nyingine nzuri ambazo serikali ingeweza kutumia kupitia mahakama lakini
ikaamua kuchagua kutumia sheria mbaya kwa kutumia mamlaka ya Waziri.
Itakumbukwa kwamba wadau wa sekta ya habari na hata serikali yenyewe imekuwa
ikikiri kwamba Sheria hiyo iliyotumiwa ni sheria mbovu inayohitaji kufutwa ama
kufanyiwa marekebisho makubwa ikiwemo kupunguza mamlaka makubwa ya viongozi wa
serikali dhidi ya vyombo vya habari. Sheria yoyote inayotambulika kuwa mbovu
katika jamii yoyote, inapoteza uhalali wa kihaki(legitimacy) miongoni mwa umma
na hivyo kuendelea kuitumia ni kuteteresha misingi ya utawala wa sheria na
kutoa mfano mbaya kwa vijana nchini na wananchi kwa ujumla. Hivyo, tunachukua
fursa hii kuitaka serikali kuharakisha mchakato wa kupitisha sheria ya vyombo
habari na sheria ya uhuru wa taarifa.
Aidha tumeshangazwa na
uamuzi wa serikali kufanya maamuzi yake kwa ubaguzi kwa kulichukulia hatua
gazeti la MwanaHALISI na kukwepa kuyachukulia hatua magazeti mengine ambayo
yameandika habari inayoshabihiana na maudhui ya habari iliyoandikwa na gazeti hilo . Kwa muda mrefu sasa,
habari za uwepo wa viongozi ama makundi ndani ya Chama Cha Mapinduzi(CCM) yenye
kupanga ‘kumng’oa’ Rais Jakaya Kikwete miongoni mwa wanaotarajiwa kugombea
urais kupitia chama hicho mwaka 2010 zimeandikwa na magazeti mbalimbali. Hatua
hii ya kibaguzi inaibua maswali kuhusu dhamira ya serikali kulifungia gazeti hilo wakati huu ambapo mchango wa gazeti hilo na mengine yaliyo mstari wa mbele
kupinga ufisadi na kutetea rasilimali za taifa unahitajika kwa kiasi kikubwa.
Hata baada ya kulifungia gazeti la MwanaHALISI, habari za aina hiyo zimeendelea
kuandikwa ikiwemo na vyombo vya habari vya nje; mathalani tarehe 24 Oktoba,
2008 kutoka Ufaransa gazeti la Africa Intelligence inayomtaja Rostam Aziz
kukusanya fedha kwa ajili ya kufadhili kundi lake katika uchaguzi huo. Katika
muktadha huo, serikali inapaswa kulifungia gazeti la MwanaHALISI mara moja, kama imeonyesha wazi kushindwa kuyachukulia hatua
magazeti mengine.
Kadhalika kwa mtiririko
wa matukio katika taifa letu, kuna mwelekeo wa Serikali na CCM kuminya maoni
yenye kumkosoa au kumgusa Rais Kikwete. Mjadala wa Rais Kikwete ‘kung’olewa’
katika uchaguzi mwaka 2010 unaelekea kuichukiza kwa kiasi kikubwa Serikali na
CCM. Gazeti la MwanaHALISI liliandika habari ya namna hiyo, likafungiwa na Serikali.
Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe akiwa katika ‘Operesheni Sangara’, alitoa
hoja hiyo na matokeo yake CCM ikaibuka na kujibu kwa vitisho na vioja.
Vijana wa Tanzania
wangependa kupata mfano uongozi bora wenye kukubali kukosolewa na kukubali mabadiliko
badala ya uongozi legelege wenye kuendeleza udikitekta wa kimawazo na hivyo
kuminya fikra huru. Si dhambi kwa CHADEMA ama mtu yoyote kutaka kuiondoa CCM
ama kiongozi wake yoyote madarakani mwaka 2010 kupitia njia za kidemokrasia.
Mwisho, tunatoa mwito
kwa watanzania wote kusoma alama za nyakati na kuunga mkono harakati hizi za
wahariri na wadau wa sekta ya habari kutetea uhuru wa kweli katika taifa letu.
Jamii itambue kwamba kitisho cha uhuru na haki kwa mtu Fulani au mahali Fulani
ni tishio kwa watu wote na mahali pote. Yanayofanywa kwa vyombo vya habari,
yanaweza pia kufanywa kwa watetezi wengine kwani hivi karibuni taifa
limeshuhudia Asasi ya HAKIELIMU ikitishiwa kutokana na jitihada zake za
kuhamasisha mabadiliko ya fikra katika sekta ya elimu na kupiga vita ufisadi
unaoathiri sekta hiyo. Tuko katika kipindi cha majaribu; kuibuka kwa mijadala
yenye kuchochea mgawanyiko/ubaguzi, kuongezeka kwa matabaka na malalamiko juu
ya hali za maisha. Katika wakati huu ambapo misingi ya nchi yetu iliyopo katika
Ngao ya Taifa ya Uhuru na Umoja inapotikiswa ni wakati wa kuunganisha “Nguvu ya
Umma” kupinga aina zote za ufisadi na kutetea rasilimali za taifa kwa
kuhamasisha maadili, fikra mbadala na mabadiliko ya kweli. Kuunga mkono
maandamano ya wadau wa sekta ya habari ni sehemu ya azma hiyo. Mshikamano,
daima; pamoja, tutashinda!
Wasalaam,
John Mnyika
Mkurugenzi wa Vijana
Taifa.
No comments:
Post a Comment