MABADIKO ya Sheria ya Hifadhi za Mifuko ya Jamii ya mwaka 2012, iliyopitishwa Aprili mwaka huu, imeendelea kuzua mtafaruku sehemu mbalimbali nchini, huku wabunge wakishinikiza kuwa, sheria hiyo inapaswa kurejeshwa bungeni ili ijadiliwe upya.
Jana, wabunge waliunga
na wafanyakazi kupinga kipengele cha sheria hiyo kinachomtaka mfanyakazi kupata
mafao yake baada ya kufikisha umri wa kustaafu kwa hiari ambao ni miaka 55, au
miaka 60 kwa mujibu wa sheria.
Hoja ya kutaka suala
hilo lijadiliwe upya ilitolewa na Mbunge wa Kisarawe (CCM), Selemani Jafo
ambaye aliungwa mkono na Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu na
Mwenyekiti wa Bunge ambaye pia ni Mbunge wa Peramiho (CCM), Jenista Mhagama.
Hoja ya Jafo ilitokana
na kuwapo kwa taarifa kuwa, zaidi ya wafanyakazi 600 katika migodi minane
nchini wameacha kazi huku wengine zaidi ya 4,000 wakiwa tayari wamewasilisha
barua za kuacha kazi kutokana na sheria hiyo.
Hata hivyo, Mbunge wa
Mwibara (CCM), Kangi Lugola alitofautiana na wenzake pale aliposema kuwa sheria
inayolalamikiwa ilishapitishwa na Bunge, hivyo angependa kujua uhalali wa
kujadiliwa tena bungeni.
Jijini Dar es Salaam , mjadala mzito uliendelea huku
baadhi ya wanasheria waliozungumza na gazeti hili wakisema: “Marekebisho hayo ni
kandimizi na yanalenga kuwanyima haki wanachama ambao wanaweza kupata matatizo
mbalimbali wakiwa kazini”.
Kwa upande wake Mamlaka
ya Usimamizi na Udhibiti wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), jana ilitoa
taarifa iliyoweka bayana kuwa, fao la kujitoa kazini limefutwa na kwamba jambo
lolote linalohusu mafao ya aina hiyo linapaswa kusubiri kutolewa kwa miongozo
husika.
Chanzo:www.mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment