Tuesday, August 7, 2012

Hii habari nimeeba kutoka kwa kaka mjengwa. Nimeipenda tu maana inawiana na tukio la leo litakalotokea Saa tisa alasiri huko London dada yetu Zakia atakaposhiriki mbio ndevu za mita 5000 katika Olympic...


Ndugu zangu, 
Riadha ni kipaji, maandalizi , ufundi na mbinu. Nahofia tumeanza kupungikiwa na vyote vinne. Nakumbuka mwezi Mei mwaka 1993 nilishiriki mbio za Kimataifa za Kilomita kumi mjini Sandviken Sweden.

Kulikuwa na wakiambiaji wapatao mia moja na hamsini. Watanzania tulikuwa wawili; Julius Mtibani ( Jeshi la Magereza) na Mimi niliyeamua kujitupa mashindanoni nikiwa na jukumu pia la kumsaidia Mtibani. 
Mwingine atauliza; unamsaidiaje mwingine kushinda mashindano ya mbio?
 
Jibu: Hilo lipo, na ndivyo wanavyofanya Wakenya. Inakuwa kama hivi; Kwa mfano, kwenye mbio za hapo juu nchini Sweden. Julius Mtibani alikuwa vizuri sana na hata uwezo wa kutwaa nafasi ya kwanza , pili au tatu. Lakini,  kulikuwa na wengine wazuri zaidi. Hivyo, kwa vile mimi sikuwa na uwezo wa kushika nafasi ya kwanza, pili au tatu, mimi na Mtibani tulikubaliana,  kuwa ningeanza mbio hizo kwa kasi sana kama inavyoonekana pichani. Kwa maana hiyo, kiufundi ningekuwa nimewahadaa wapinzani wa Julius Mtibani. Wakati wapinzani wa Mtibani wakikimbizana na kasi yangu Julius Mtibani alibaki kwenye nafasi ya saba.
 
Tulipomaliza kilomita tano, kwa maana ya nusu ya mbio, basi, niligeuka nyuma na kumwona Mtibani akiwa bado kwenye nafasi ya saba kwenye umbali wa mita kama 20 hivi. Nikamtamkia; " E bwana  anza kupanda!". Hakuna aliyeelewa lugha yetu ya Kiswahili. Mtibani akaanza kupanda kwa kasi huku mimi nikirejea kwenye kasi yangu ya kawaida.  Ni kama dereva anayepunguza mwendo mteremkoni.
 
Hatimaye Mtibani akaweza kuongoza mbio hizo hadi zilipobaki kilomita tatu ndipo wapinzani wake nao walijipanga upya. Akapitwa na wawili na hivyo kumaliza akishika nafasi ya tatu! Mimi nilimaliza nikishika nafasi ya tisa katika muda wa dakika 34 na sekunde 36.

Ndio, riadha ni kipaji, maandalizi, ufundi na mbinu. Ona Wakenya, wanakimbia wakiwa kama saba au hata kumi na mbili. Wanawasiliana muda wote. Na wanajua ni kina nani wanawasaidia kuhakikisha hata nafasi ya kwanza, pili na tatu wanachukua wao.

Mwanariadha wetu Zakhia Mrisho na wengineo wanahitaji sapoti kama hizi za kiufundi ili waweze kufanya vema kwenye mashindano makubwa kama Olimpiki. Kila la kheri Zakhia Mrisho katika mbio za mita 5000 mchana huu.
Maggid Mjengwa,
Bagamoyo.
0788 111 765

No comments:

Post a Comment