Prof Baregu
Chama cha Mapinduzi (CCM), kimempongeza Mjumbe wa Kamati Kuu ya
Chadema, Profesa Mwesiga Baregu kwa uamuzi wake wa kugoma kujitoa katika Tume
ya Mabadiliko ya Katiba na kuadi kuwa kwa kitendo hicho ameonyesha uzalendo
mkubwa kwa taifa lake.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa, Itikadi na Uenezi, Nape
Nnauye alisema jana alipozungumza na waandishi wa habari ambapo alisema,
Profesa Baregu ameweka maslahi ya taifa mbele badala ya vyama.
Kauli hiyo ya CCM imekuja muda mfupi baada ya vyombo vya habari
kuandika habari zinazohusu Profesa Baregu kukataa kujitoa katika Tume ya
Mabadiliko ya Katiba hiyo licha ya Chadema kutaka afanye hivyo kwa kile
kinachodaiwa kuwa, CCM imeteka mchakato wa Katiba kwa kuingiza makada na
viongozi wake wengi katika mabaraza ya Katiba.
Baregu alikaririwa akisema hakuna tatizo katika tume hiyo na
kwamba chama chake kinahitaji kujishauri upya kuhusu kusudio lake la kutaka
kususia mchakato huo.
Baregu alifika mbali zaidi aliposema kama
angeambiwa achague nchi yake na chama basi angechagua nchi kwanza.
Jana Nape alisema,“CCM inampongeza kwa dhati Profesa Baregu kwa
uzalendo na ukomavu wa kisiasa aliouonyesha kwa kuwakatalia kujitoa kwenye tume
na kuweka mbele maslahi ya taifa lake, huyu ni mfano wa kuigwa ameweka pembeni
uchadema wake kwa kuthamini utaifa.”
Alisema kitendo cha Baregu kukataa kujitoa kwenye tume inapaswa
kuwa fundisho kwa chama hicho kuondokana na tabia za kitoto za kususa.
Alisema Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni wa Katiba na
Sheria, Tundu Lissu alitoa malalamiko bungeni kwamba CCM imeteka mchakato wa
Katiba Mpya kwa kujaza makada wengi katika mabaraza hayo.
“Wajifunze kutoka kwetu, wakati CCM inahamasisha wananchi
washiriki kwenye mchakato wa Katiba, wao Chadema wanahamasisha watu wavuruge
mchakato huo kwa maslahi wanayofahamu wenyewe,” alisema.
“Tunapongeza msimamo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwa kupuuza
hoja ya kufuta mabaraza ya Katiba, kama
wanasusa sisi tutaendelea na mchakato,” alisema Nape.
Alisema nchi nyingi hasa za kiafrika, zimekuwa zikikumbwa na
machafuko yanayosababishwa na upatikanaji wa Katiba na kwamba wananchi
wanatakiwa kuwa makini na malengo ya chama hicho.
“ Chadema wanaona Watanzania wanaendelea na mchakato bila
machafuko wanakosa majibu kwa mabeberu wanaowafadhili kuchafua nchi yetu, ndiyo
maana kila kukicha wanakuja na visa na vituko kusumbua mchakato wa Katiba,”
alisema Nape.
Aidha, chama hicho kimewalaumu baadhi ya wabunge wa Chadema
kutumia Bunge kama jukwaa la kuwashambulia
watu ambao hawana fursa ya kuingia bungeni kujibu mashambulizi hayo.
“Utamaduni huo ni wa hovyo na unakiuka haki za msingi za
binadamu ambazo zinataka mtu anayetuhumiwa kupewa fursa ya kusikilizwa,”
alisema Nape.
Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, Katibu Mkuu wa Chadema,
Wilbroad Slaa na Msemaji wa Chadema, John Mnyika walipopigiwa simu
hawakupatikana jana.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment