Wednesday, May 29, 2013

Muziki bila madawa inawezekana.

Taifa la muziki wa kizazi kipya nchini Tanzania limeondokewa na msanii mahiri wa bongofleva hasa katika upande wa mitindo huru 'free style' Albert Mangwea.

Nimeanza kumfahamu Mangwea akiwa amejipambanua katika sanaa kwa majina mengi ambayo alijipa kutokana na kipaji chake cha uimbaji. Binafsi nimeanza kumfahamu kwa kina baada ya kuimba wimbo wa 'Ghetto langu'. Naamini hata wengine walianza kumjua kwa kina kutokana na wimbo huo.

Ingawa alianza kuimba akiwa Dodoma na kundi lake la Chamber Squad mskani ya East Zuu, akiwa na kina Dark Master na Mez B, lakini kujulikana kwake kulianza baada ya wimbo huo.

Mpaka sasa watu wakiwa na vyumba vizuri utawasikia wakijisifia 'Ghetto langu zuri kama la Mangwea', hakuna shaka katika hilo kuwa wimbo ule ulimtoa vilivyo.

Baadaye aliimba vibao vingi ambavyo mpaka sasa vikipigwa kwenye radio lazima utikise kichwa, hasa 'Mikasi' alioshirikisha wasanii wakongwe chini ya mtayarishaji mahiri P Funk wa Bongo Record.

Mara baada ya kusikia kifo chake cha ghafla kilichotokea nchini Afrika Kusini jana, sikusumbuka sana yalikuja mawazo mengi lakini kubwa lililosumbua kichwa changu ni dawa za kulevya. Ingawa hakuna taarifa rasmi za daktari juu ya kifo chake lakini watu wa karibu wa marehemu wanaeleza alitumia dawa za kulevya kwa kiwango kikubwa kabla mauti hayajamfika.

Ingawa mauti yalimkuta usingizini lakini hilo la dawa za kulevya haliepukiki kwa maana tayari alishaingia katika kundi hilo baya, lakini mara kwa mara alikuwa akipinga taarifa hizo lakini waswahili husema 'mtu atakunyima chakula lakini hawezi kukunyima maneno' rafiki wa karibu wa Mangwea walikuwa wakisema wazi kukerwa na tabia ya ndugu yao kutumia dawa za kulevya.

Naandika haya si kwa kumdhalilisha marehemu, lakini ni kuonyesha wazi kuuungana na kampeni ya wasanii wa bongofleva iliyoanzishwa mwishoni mwa mwaka jana kuhusu matumizi ya dawa za kulevya. Yaani 'muziki bila madawa inawezekana'.

Nimefurahi kusikia baadhi ya wanamuziki kusogeza mbele matamasha yao ambayo mengi yalitakiwa kufanyika siku za hivi karibuni, lengo ni kuungana na ndugu pamoja na wanafamilia ya muziki nchini kuomboleza kifo cha ndugu yao.

Ipo haja kuchukua mifano hai ya matatizo ya dawa za kulevya, tayari msanii mwingine wa bongo fleva Rehema Chalamila 'Ray C' alisaidiwa matibabu na Rais Jakaya Kikwete, kuhusiana na dawa za kulevya.

Wapo baadhi ambao wanatajwa kuendelea na madawa miongoni mwao wakiwa ni TID, Loyd Eyez, Daz Baba na wengine ambao bado hawajajibainisha, lakini mficha maradhi kifo humuumbua.

Kwa pamoja tupige vita matumizi na uuzaji wa dawa za kulevya, kwa maana hakuna haja ya kusifia utajiri wa vijana wanaouza dawa za kulevya wakati vijana wengine wanaharibikiwa na kupoteza uhai wakati taifa bado linawahitaji.

MUZIKI BILA MADAWA INAWEZEKANA

HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
DAR ES SALAAM, TANZANIA
29, May 2013

No comments:

Post a Comment