Wapenzi wa mpira wa miguu duniani hasa wale wanaoshabikia
ligi ya Uingereza jana walishikwa na butwaa baada ya kocha mkuu wa klabu kongwe
ya Mnachester United, Sir Alex Ferguson kutangaza kujiuzulu kuifundisha klabu
hiyo iliyotangaza ubingwa wa ligi hiyo mapema mwezi huu.
Kwa wale wanaofuatilia maisha ya nguli huyo habari hizi
hazijawashitua sana
kwa maana kwa kipindi kirefu amekuwa akitajataja kustaafu kuifundisha klabu
hiyo aliyojiunga nayo mwaka 1986.
Tangu aanze kuifundisha Man United, Ferguson amesimamia
michezo 1498 akiwa kocha; katika michezo hiyo ameshinda 894, suluhu 337 na
kufungwa michezo 267. Maana yake ameshinda kwa silimia 60 kitu kinachomfanya
kuwa kocha mwenye mafanikio makubwa kuliko wote Uingereza.
Aidha kwa kudhihirisha mafanikio yake Ferguson ametwaa mataji 49 tangu aanze kuwa
kocha katika vilabu tofauti, ambapo mbali ya vikombe hivyo pia ameweza
kujinyakulia tuzo zaidi ya 70 katika historia yake ya ufundishaji soka.
Akizungumza na vyombo vya habari wiki hii asubuhi Ferguson alisema kwa masikitiko kuwa, “maamuzi niliyofanya
kustaafu ni miongoni mwa mambo niliyokuwa nikiyafikiria sana , nadhani ni wakati muafaka sasa kufanya
hivyo.”
Kitu pekee ambacho kinamfanya Ferguson
kustaafu kwa amani ni kuweza kuiwacha Man United katika daraja la juu la
mafanikio hasa kwa kuvunja rekodi ya Liverpool
kwa kuchukua kikombe cha ligi ya nchi hiyo kwa mara nyingi zaidi.
Kabla ya kujiunga na Manchester United, Ferguson alipata
kuvifundisha vilabu vya East Stirling 1974, St Mirren 1975-78, Aberdeen
1978-86, baadaye akaifundisha timu ya taifa ya Scotland kwa mwaka mmoja halafu
akahamia rasmi Manchester United tangu mwaka 1986 mpaka anastaafu kufundisha
soka mwaka huu.
Ferguson ambaye amezaliwa Disemba 31, 1941 nchini Scotland
alianza kucheza mpira wa miguu mwaka 1957 katika klabu ya Queens Park, baadaye
akahamia St. Johnstone, Dunfermline Athletic, Rangers, falkrik na akamalizia na
Ayr United mwaka 1974.
Akiwa anacheza safu ya ushambuliaji Ferguson katika vilabu vyote hivyo
amefanikiwa kucheza michezo 317 na kushinda mabao 170.
Alijiunga Manchester Novemba sita baada ya kocha wa awali
Atkinson kutimuliwa, katika mechi yake ya kwanza akiwa kocha Man United
Ferguson alichapwa mabao 2-0 timu ya Oxford United Novemba 8, 1986 baadaye siku
saba zilizofiuata alityoa suluhu tasa na timu ya Norwich City
ikifuatiwa na ushindi wa kwanza wa bao 1-0 dhidi ya timu yake ya zamani QPR.
Kocha aliyekuwa akitajwatajwa kuchukua mikoba ya timu hiyo
David Moyes wa Everton ndiye aliyetangazwa rasmi jana kuifundisha Man U baada
ya Ferguson .
Aidha mechi ya mwisho ya Ferguson
akiwa kocha man U itakuwa ni dhidi ya West Brom
ambapo hiyo itakuwa ni mechi yake ya 1500 akiwa kocha katika timu hiyo, ingawa
zipo taarifa kuwa mkongwe huyo amekubaliana na ombi la kubaki Man U akiwa
mkurugenzi.
Wakati huohuo taarifa zinaeleza kuwa hisa za
timu hiyo zimeshuka mara baada ya kocha huyo kutangaza kustaafu.
Taarifa za kustaafu kwa kocha wa Manchester
United, Sir Alex Ferguson zimeifanya klabu hiyo kupoteza mapato yake.
Huku maelfu wa mashabiki wakionekana
kushtushwa na habari za kustaafu kwa Fergie maarufu kama
babu, lakini pia upande wa masoko kwa klabu ya Manchester United kumekuwa na
pigo pia.
Hii ni baada ya kushuka kwa ununuzi wa hisa za
klabu hiyo kwa zaidi ya asilimia tano kwenye soko la hisa la New York .
Wachambuzi wa masuala ya biashara wameeleza
hofu yao juu ya kushuka kwa biashara za United
kufuatia kuondoka kwa Ferguson kwa kusema
itakuwa kazi kubwa kumpata mrithi wake ambaye ataweza kuchagiza mafanikio ya
klabu hiyo yatakayovutia wadhamini mbalimbali kama
alivyofanya kwa miaka 27 aliyokaa na United.
Familia ya Malcom Glazer yenye makao yake Miami nchini Marekani ambayo ndio inayomiliki klabu ya
Manchester United bado haijatangaza mrithi wa Ferguson japo wadadisi na vyanzo vya karibu
vya United vinasema huenda kocha wa Everton, David Moyes akakabidhiwa jukumu la
kuifundisha United,taarifa ambazo hazijathibitishwa wala kukanushwa na uongozi
wa Old Trafford.
Kushuka huko kwa hisa za United kumeifanya
klabu hiyo kupoteza mapato yake kwa karibu asilimia 1.3 kwa hisa moja ambayo
hununuliwa kwa dola za kimarekani 18.52 kwa hisa.
Licha ya kushuka kwa hisa hizo kufuatia
taarifa za kustaafu kwa Ferguson
lakini zaidi ya asilimia 30 ya hisa za United ziliuzwa kwenye soko la hisa hii
leo.
BBC SWAHILI
No comments:
Post a Comment