Kwangu kwa msimu huu kocha aliyeweza kuiletea mafanikio timu yake ni Mecky Mexime wa Mtibwa Sugar (wa kwanza kushoto).
Michuano ya ligi kuu Soka Tanzania bara
maarufu Vodacom, inafikia tamati Mei 18 ikiwa tayari bingwa ameshajulikana na
timu itakayoshika nafasi ya pili pia imeshajulikana.
Ugomvi mkubwa upo kwenye nafasi ya tatu, nne,
tano na timu tatu zitakazoshuka daraja msimu huu, ili kuzipa nafasi timu za zilizopanda
daraja kwa michuano ya msimu ujao.
Timu za Mgambo JKT, Toto Africa, African Lyon na
Polisi Morogoro ndizo zilizo katika ‘Danger zone’ katika msimu huu kuaga
michuano ya ligi kuu Tanzania bara.
Hata hivyo Mgambo JKT wana nafasi kubwa ya
kubaki kwenye ligi kwani wamebakisha mechi tatu ambapo katika mechi hizo
wanatakiwa kupata point moja tu ili waepukane na janga la kushuka daraja,
ingawa wakipoteza michezo yote wataangukia katika orodha ya timu tatu
zitakazoshuka daraja.
Lakini cha kusikitisha Mgambo JKT wamebakisha
mechi ngumu tupu kati ya Yanga, Azam na African Lyon ambao ni mahasimu wao
katika kushuka daraja.
Kumalizika kwa ligi ni kitu kimoja lakini
maandalizi ya msimu ujao wa 2013/14 ni kitu cha msingi sana
kwa timu zinazoshiriki hasa zile ambazo matarajio yao hayakutimia katika msimu unaoisha.
Ipo haja mashabiki kuanza kugeuka wanachama ili
kuzipa nguvu timu zao, mashabiki wasiishie tu kupiga kelele bali wawe wanachama
hai watakaonunua kadi na kuzichangia timu kiuchumi ili kutimiza malengo ya
vilabu vya soka nchini.
Nikiambiwa nitaje timu tatu zilizofanya vizuri
msimu huu nitazitaja timu za Azam FC, Mtibwa Sugar na Kagera Sugar; timu hizi
zimeongeza upinzani mkubwa katika soka la Tanzania hata katika kuitwa timu ya
Taifa, utaona ule ‘usimba’ na ‘uyanga’ umepungua lakini Mtibwa Sugar na Azam FC
ndizo timu zinazoongoza kuwa na wachezaji wengi walioitwa katika vikosi vyote
viwili vya kocha Kim Poulsen anayenoa Taifa Stars na Young Tafa Stars.
Kitu kingine nilichojifunza kwenye msimu huu ni
matumizi bora ya timu za vijana kwenye vilabu, wazo hili lilipoletwa na Rais wa
TFF Leodger Tenga, watu walilichukulia kurahisi, lakini kampuni ya Azam kupitia
maji ya Uhai ilipoanzisha michuano ya timu za vijana chini ya miaka 20 vilabu
havikuchukulia uzito michuano hiyo.
Hata hivyo michuano iliyopita mwanzoni mwa mwaka
huu imeibua vipaji lukuki ambavyo vimeleta faida kubwa kwa timu za Simba na
Coastal Union . Mpaka sasa Simba inatembea
kifua mbele kutokana na vijana wa timu B, na Coastal Union kadhalika.
Hivyo vilabu vitilie mkazo sana kuibua vipaji vya vijana ili ligi irudi
ilipotoka kwa kujivunia wachezaji wa ndani, vilabu vingi viliwika miaka ya
nyuma kwa kutumia wachezaji wazalendo na wacheaji watapatikana kwa kukuza
vipaji vya watoto.
Lakini timu kubwa nazo ziache kupora wachezaji
kutoka timu zilizo na uchumi mdogo kwa hadaa, hii itapunguza ushindani. Kwani
historia inaonyesha mara nyingi wachezaji wanapokwenda kucheza timu kubwa
hawadumu katika vipaji vyao na hii inatokana na hujuma wanazofanyiana na mara
zote mhanga wa hujuma hizi anakuwa ni mchezaji asiye na hatia.
Maana tayari timu kubwa zimeshaanza kutajataja
wachezaji watakaowasajili msimu ujao, si jambo baya lakini watumie taratibu zilizowekwa
kuzungumza na timu badala ya kuwaghilibu wachezaji kwa kuwaonyesha fedha nyingi
ili wavunje mikataba na timu zao.
DAR
ES SALAAM , TANZANIA
1st
May, 2013
No comments:
Post a Comment