Friday, May 10, 2013

Huyu ndiye David Moyes aliyependekezwa na Sir Alex kurithi mikoba yake.



Sir Alex akisisitiza mpira uishe siku timu yake ilipokutana na Everton, pembeni ni kocha wa Everton David Moyes ambaye ndiye kocha atakayerithi mikoba ya sir Alex.


Uongozi wa Old Trafford umetangaza rasmi na kuthibitisha kuwa David Moyes atakuwa meneja mpya wa timu hiyo kuchukua nafasi ya Sir Alex Ferguson atakayestaafu mwishoni mwa msimu huu.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Old Trafford mchana wa leo, David Moyes amepewa mkataba wa miaka sita wa kuifundisha Manchester United kuanzia msimu ujao.
David Moyes mwenye umri wa miaka 50,ametangazwa kuwa mrithi wa Ferguson ambaye alitangaza kustaafu kuifundisha Manchester United mwishoni mwa msimu huu baada ya kuifundisha United kwa karibu miaka 27.
"Tumekubaliana kwa pamoja bila kipingamizi kupitisha jina la David Moyes" alisema Ferguson.
"David ni mtu ambaye ana uadilifu wa hali ya juu na mwenye maadili makubwa ya kazi. Nimeipenda kazi yake kwa muda mrefu tangu mwaka 1998 wakati tulipomjadili kama kocha msaidizi.
"Hakuna maswali juu yake na ana viwango ambavyo tulikuwa tunavihitaji kwa meneja wa klabu hii." aliongeza Ferguson.
Naye David Moyes amesema " Najua ni vigumu kurithi na kufikia mafanikio kama ya kocha bora zaidi duniani, lakini nafasi ya kuifundisha Manchester United sio jambo ambalo linakuja mara mbili hivyo nina matumani mazuri nikiwa kocha wa klabu hii msimu ujao."
David Moyes amekaa Goodison Park kwa miaka 11 na hajawahi kushinda taji la ligi kuu lakini ameweza kuifanya Everton kuwa miongoni mwa klabu zenye mafanikio ya wastani kwenye ligi kuu soka nchini England.
Akiwa na Everton, Moyes ameifikisha fainali ya kombe la FA mwaka 2009 katika mechi waliyofungwa na Chelsea 2-1, na pia mwaka 2005 aliweza kumaliza nafasi ya nne kwenye msimamo wa ligi kuu ya England lakini waliondolewa kwenye hatua za mwanzo za kusaka nafasi ya kushiriki michuano ya klabu bingwa barani Ulaya.
Licha ya kuwa na bajeti ndogo ya usajili, Moyes aliiwezesha Everton kuonekana miongoni mwa timu zenye kiwango bora cha soka ambapo mara kadhaa amekuwa akitoa upinzani mkubwa kwa Manchester United ambapo katika mechi ya kwanza ya ligi kuu msimu huu, Everton waliifunga United kwa bao moja kwa bila.
Kibarua kikubwa ambacho anatarajia kukikabili kama meneja mpya wa United msimu ujao itakuwa ni kuhakikisha mchezaji wake wa zamani aliyemuibua Wayne Rooney anasalia kwenye klabu hiyo baada ya kutangaza kuwa anataka kuondoka.
Meneja wa Wigan, Roberto Martinez na bosi wa Swansea, Michael Laudrup wanatajwa kama warithi wa Moyes kwenye klabu ya Everton.
Mechi ya kwanza ya David Moyes kama kocha mpya wa Manchester United inatarajia kuwa ya ngao ya jamii watakapo pambana na watani zao Manchester City ama Wigan hapo tarehe 11 mwezi wa nane kwenye uwanja wa Wembley.
David Moyes kocha mpya wa Manchester United
BBC SWAHILI

No comments:

Post a Comment