Wednesday, May 29, 2013

Zitto Kabwe amwandikia barua waziri mkuu wa Uingereza.

Dar/Dodoma. Waziri Kivuli wa Fedha, Zitto Kabwe ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia Chadema, amemwandikia barua Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron akimwomba kufuta sheria ya nchi yake inayowalinda watoroshaji wa fedha za umma wa nchi mbalimbali.

Zitto pia amemwomba Cameron kuzishawishi nchi nyingine tajiri kuwa na sheria za aina hiyo ili kudhibiti mafisadi wa nchi zinazoendelea.

Hatua hiyo ya Zitto, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema upande wa Tanzania Bara, ni mwendelezo wa juhudi zake za kupambana na mafisadi ndani ya Serikali wanaodaiwa kuweka katika benki za nje kiasi cha dola za Marekani milioni 196 (sawa na Sh323 bilioni).

Zitto amechukua hatua hiyo kwa kuzingatia kuwa Waziri Mkuu Cameron atakuwa mwenyeji wa Kundi la Nchi Tajiri Duniani linalojulikana kama G-8 ambalo litakutana Lough Erne, Uingereza kuanzia Juni 17–18. Cameron ndiye atakuwa Mwenyekiti wa mkutano huo.

Novemba mwaka jana, Mbunge huyo alipeleka hoja binafsi bungeni akitaka iundwe timu maalumu kwa ajili ya kufuatilia kiasi cha Sh 323 bilioni ambazo zimethibitika kufichwa Uswisi.

Zitto aliikabidhi barua hiyo Jumatatu ya wiki hii kwa Balozi wa Uingereza nchini Dianna Melrose, akimwomba aiwasilishe kwa Waziri Mkuu Cameron, kuelezea kilio cha Watanzania kuhusiana na fedha hizo.

Alisema sheria hiyo ina athari kubwa kwa maisha ya Watanzania wengi maskini na Afrika kwa ujumla, ambapo alisema anaamini sheria inayotaka uwazi itapitishwa kwenye mkutano wa mataifa manane tajiri yenye viwanda duniani, maarufu G-8, utakaofanyika mwezi ujao.

Akizungumzia suala hilo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Fredrick Werema alisema kuwa ana taarifa kuhusu barua hiyo iliyoandikwa na Zitto kwenda kwa Cameron kuhusu shinikizo la Serikali kufanya mchakato wa kurudisha fedha zilizofichwa nje ya nchi.

“Tunafanya kazi na siyo kuzungumza ovyo kila mahali au kila hatua tuliyofikia, ila tunafanya kazi masaa yote, Watanzania wasubiri tu hatua tutakayofikia na tukiona tumejiridhisha tutawaambia nini kimefanyika,” aliongeza Werema.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment