Monday, May 13, 2013

Mitandao ya kijamii inavyoathiri watu kisaikolojia.


Facebook, mitandao mingine ya kijamii pamoja na huduma ya ‘blackberry mesenger’ maarufu kama BBM huathiri watu kisaikolojia, husababisha ndoa kuvunjika pamoja na usaliti katika uhusiano, wanasayansi wamebaini.
Utafiti huo uliofanywa mwaka 2012 na wanasayansi wa nchini Israel umebaini kuwa kwa wastani, wanawake wanatumia dakika 81 katika mitandao ya kijamii kwa siku ukilinganisha na wanaume ambao hutumia dakika 64, huku watu wasio na elimu wakionekana kuathirika zaidi na mitandao hiyo.
Watafiti hao kutoka Chuo Kikuu cha Tel Aviv walihusisha matukio kadhaa ya kisaikolojia kati ya watu walioathirika na mtandao na udanganyifu uliosababishwa na uhusiano unayoanzishwa kupitia mitandao ya kijamii.
Utafiti huo ulibaini kuwa wote waliohusishwa walikuwa na tatizo la upweke, ingawa hakuna aliyekuwa na historia ya matumizi ya dawa za kulevya au matatizo ya kisaikolojia.
Watu wenye upweke walionekana kupendelea kutafuta uhusiano kupitia mitandao, jambo linaloelezwa kusababisha kuwaumiza watu hao na kuhisi kusalitiwa.
Kiongozi wa utafiti huo Dk Uri Nitzan kutoka Chuo Kikuu cha Sackler mchepuo wa Tiba na Afya ya Akili, Shalvata Mental Health Care Centre alisema: “Kama ilivyo matumizi ya mtandao yanazidi kuwa makubwa. Vivyo hivyo inavyozidi kuhusiana na masuala ya saikolojia. Mawasiliano ya kompyuta kama Facebook na makundi ya mawasiliano yaliyopo ndani ni sehemu muhimu ya habari hii.”
Utafiti huo awali ulihusisha wagonjwa watatu ambapo Dk Nitzan anasema kuwa utafiti wao ulibaini kuwapo na mawasiliano kati ya saikolojia za wagonjwa hao na mawasiliano ya mitandao ikiwemo Facebook. Dk Nitzan anasema kuwa wagonjwa wote watatu waliachana na maisha ya upweke na kupata furaha baada ya kupata wapenzi wapya kupitia mitandao.
Anasema: “Ingawa uhusiano wau huwa na mtazamo chanya awali, lakini huishia kuwa na mawazo ya kuumizwa, kusalitiwa na uvamizi wa faragha. Watu hawa walibadilishana mawazo, ikiwamo upweke na mazingira magumu katika hasira au kutengana na watu waliowapenda awali, kutokana na teknolojia hawakuwa na historia ya kunyanyaswa,” anasema na kuongeza:
“Katika kila kesi, kulikuwa na uhusiano baina ya kuwapo na maendeleo ya taratibu na ongezeko la dalili za kuathirika kisaikolojia, pamoja na udanganyifu, wasiwasi, kuchanganyikiwa na matumizi yaliyozidi ya mawasiliano ya kompyuta.
”Dk Nitzan anasema kuwa tatizo kubwa la mitandao ni watu kuanzisha uhusiano kabla ya kuonana ana kwa ana, tatizo ambalo husababisha mtu kumwona mwenzake anamfaa, huku hali ikiwa ni tofauti pindi wawili hao wanapokutana. Aliongeza kuwa wataalamu wa afya ya akili lazima waache ushawishi wa matumizi ya mitandao ya kijamii wanapozungumza na wagonjwa.
“Unapowauliza watu kuhusu maisha yao ya kijamii ni busara zaidi kuwauliza juu ya matumizi ya Facebook na mitandao mingine ya kijamii, kama matumizi ya mitandao,”anasema.
Anaongeza: “Utafiti wetu unaonyesha, wakati teknolojia kama Facebook ikiwa na faida nyingi, baadhi ya watu wamekuwa wakiathirika na mitandao hii ya kijamii, huku ikiwavutia walio wapweke au walio katika mazingira magumu katika maisha yao ya kila siku, wakati wengine wakilazimisha tabia zisizo zao.”
Wataalamu Dar
Mwanasaikolojia na Mkurugenzi wa Kliniki ya NEHOTA inayotoa huduma ya ushauri iliyopo Makongo Juu jijini, Dk Bonaventura Mutayoba Balige anasema kuwa tatizo kubwa linalowafanya watumiaji wa mitandao ya kijamii kuathirika kisaikolojia ni uhusiano unayoanzishwa kupitia mitandao hiyo. Uhusiano unaoanzishwa katika mitandao ya kijamii hata ukiwa na matokeo chanya na kuanzisha ndoa, mara nyingi wanandoa hao huhisi kuumizwa au kusalitiwa muda wowote, jambo linalosababisha migogoro ya mara kwa mara.
“Unapokuwa na mume au mke mliyekutana Facebook, kisha akaendelea kutumia mtandao huo, bila shaka anapokuwa bize mtandaoni muda mwingi, mwenzake huanza kuathirika kisaikolojia kwani huanza kuumia kwa kuhisi kusalitiwa na mweza wake,” anasema mwanasaikolojia huyo.
Dk Balige anasema kuwa licha ya kuwepo watu wanaoathirika kwa kuwa mitandaoni muda wote, bado idadi ya watu wanaoanzisha uhusiano kwenye mitandao hiyo wakiwa kwenye hatari ya kuathirika zaidi, hasa kutokana na udanganyifu uliopo.
“Picha hazisemi kweli; wapo watu wakipiga picha haitoki kama alivyo. Hivyo mwanamke au mwanamume akianzisha uhusiano kwa kutegemea picha aliyoiona Facebook, bila shaka anaweza asitamani kuendelea na uhusiano huo atakapokutana na mtu husika ana kwa ana,” anasema Dr Balige.
Tafiti nyingine
Machi 8, 2011 wanasheria nchini Marekani walitoa ripoti yao kuwa mtandao wa Facebook ni chanzo cha migogoro katika uhusiano. Pia husababisha ndoa nyingi kuvunjika, hali inayosababisha kuongezeka kwa kesi za kudai talaka mahakamani.
Wanasheria hao walisema chanzo cha talaka nyingi ni mtandao wa Facebook ikiwamo ‘Blackberry messenger’ (BBM), huku ‘My Space’ ikichangia kwa asilimia 15 na Twitter kwa asilimia 5.
Mwanasaikolojia na mshauri wa ndoa kutoka Chuo Kikuu cha Tiba na Afya Loyola, Chicago Dk Steven Kimmons amewahi kusema: “Nimepokea kesi nyingi, mojawapo ni mwanamume aliyekutana na mwanamke aliyesoma naye kwenye mtandao wa Facebook na kuanza uhusiano, huku akiwa ameshaoa. Ni tatizo kubwa.”
Mikasa ya Facebook
Kijana mmoja aliyejitambulisha kwa jina moja la Henry anasema kuwa aliwahi kufungua akaunti ya Facebook na barua pepe feki vyote vikiwa na jina la msichana. Aliombwa urafiki na wanaume wengi, ambao walimtongoza na baadaye aliamua kumkubali mmoja aliyemfahamu, akiwa pia mtu wake wa karibu bila mtu huyo kumgundua.
“Nilianza kuchati naye, alinipenda kupitia picha niliyoiweka kwenye ukurasa wangu. Alinitumia barua pepe pia, baada ya miezi miwili alihitaji kuniona niliamua kufunga akaunti hiyo baadaye,” anasema Henry aliyebainisha kuwa mwanaume huyo alikuwa ni mume wa mtu.
Rahel Simon (si jina lake halisi) anasema kuwa alikutana na mume wake mwaka 2009 kwenye mtandao wa Facebook. Walipendana na kwa kuwa wote waliishi jijini Dar es Salaam ilikuwa rahisi kuonana.
“Wakati huo mtandao ulikuwa hauna watu wengi kama ilivyo sasa. Tulijuana na kufunga ndoa, ila nina wasiwasi wa kusalitiwa, muda mwingi mume wangu anapokuwa akichati na marafiki zake kupitia mtandao huo. Yaani kuna wakati huwa najilaumu na kutamani kama tungekutana kanisani, huwa nahisi kama alivyokutana na mimi ipo siku ataisaliti ndoa,” anasema Rahel.
Mwingine aliyejitaja kwa jina moja la Janet anasema: “Sitaki kusikia uhusiano wa kwenye mtandao.
Nilikutana na wanaume kadhaa, nikajiingiza katika uhusiano nao, baada ya kunitumia waliniacha, sidhani kama kuna mwanamume aliye tayari na mwanamke anayekutana naye kwenye hii mitandao ni waharibifu tu,” anasema kwa jazba.
Mwathirika mwingine (Hamis) aliyekuwa akitafuta mchumba kupitia Facebook anasema kuwa alikutana na msichana mmoja kupitia mtandao huo baada ya kuona picha alizoweka binti huyo kwenye ukurasa wake, zikiwa na staili mbalimbali na kumpenda, akamtongoza na wakakubaliana kuonana. “Tulipanga kuonana Ukonga jijini Dar es Salaam. Wakati wote tuliwasiliana kupitia simu. Aliniambia angefika kwa usafiri wa daladala nilimsubiri kituoni.
Alipofika alinipigia simu, nilimuuliza umevaaje akaniambia nguo za kitenge. Nilitupa jicho ila nilipomwona sikuamini, nilizima simu kwa kuwa alikuwa mbali ili asijue kama ni mimi na kutokomea. Alikuwa ni tofauti na nilivyomwona Facebook alikuwa mbaya,” anasema Hamis.
Dondoo muhimu
Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Gothenberg uligundua kwamba watu wenye kipato cha chini na wenye elimu ndogo wanatumia muda mwingi katika mtandao wa Facebook.
Katika kundi hili, wengi wanaotumia muda wao mwingi kwenye mitandao ya kijamii hawana furaha na wametawaliwa hali ya chini katika maisha yao.
Utafiti unaonyesha zaidi ya asilimia 85 ya watumiaji wa Facebook huingia katika mitandao hiyo kila siku. Asilimia 26 ya kundi hilo huona ni jambo la kawaida kwa wao kutoingia mara kwa mara.

Imeandaliwa na Editha Majura kutoka gazeti la Mwananchi Jumapili.

No comments:

Post a Comment