Sunday, May 12, 2013

Je unamkumbuka Banza Tshikala mchezaji wa zamani wa Yanga? Soma hapa...


Ni jioni tulivu nipo maeneo ya Sinza jijini Dar es Salaam, namwona mtu ninayeamini namfahamu, lakini sikumbuki ni nani. Hata hivyo kutokana na uzoefu nilionao kwenye mambo ya mpira, nahisi ni mchezaji ingawa bado nashindwa kumkumbuka.
Natamani kumjua ni nani namfuatilia, mbele kidogo maeneo ya Sinza Legho, anaingia mtaa upande wa kulia wa barabara. Licha ya safari yangu kuwa inaishia hapo, lakini nililazimika kumfuatilia na kabla ya kukata shauri la kumsimamisha na kumuuliza namkumbuka kuwa, si mwingine bali ni aliyewahi kuwa mchezaji wa timu ya Yanga Banza Tshikala.
Nikimwangalia anaonekana ni mwenye siha njema, namkimbilia ili niseme naye mawili, matatu. Msomaji usishangae kwa nini namfuatilia, hii ni kutokana na kupenda michezo hasa kwa wachezaji wa zamani waliofanya maajabu wakiwa katika soka’.
Kwa mshangao natokea katika kanisa kubwa ambapo Banza anaingia ndani yake. Kutokana na kutokuwa na mavazi yanayoniruhusu kuwepo eneo hilo naondoka bila kutimiza lengo langu.
Nakutana na Mhariri wangu wa magazeti ya mwisho wa juma Julius Magodi na kumfahamisha kuhusu kukutana na mchezaji huyo, ananipatia usafiri na kunitaka nimfuatilie siku inayofuata ambayo ni Jumapili.
Nafanya hivyo na kwa bahati nzuri wakati nafika kanisani hapo na kumkuta Banza akimwombea binti ambaye bila shaka alikuwa na matatizo. Nasubiri hadi misa ya maombezi inaisha, nakutana rasmi na mchezaji huyo aliyewahi kuichezea Yanga kwa misimu mitano. Nasalimiana naye na mwisho wa yote najitambulisha kwake, naye bila hiyana ananikaribisha ofisini kwake.
Nakutana na mchungaji mkuu wa kanisa hilo linaloitwa The Oasis Of Hearling Minitries, Prosper Ntepa na kupewa baraka zote za kufanya mahojiano na Banza ambaye ni mchungaji wa vijana katika kanisa hilo.
Banza anaanza kuelezea historia yake ya maisha kuwa alizaliwa Julai 27 mwaka 1972, nchini Kongo.
Kwa ufupi anaeleza safari yake ya kucheza soka katika ardhi ya Tanzania kuwa iliianza mwaka 1994, alipokuja na timu ya TP Mazembe akiwa ni mchezaji kwenye timu hiyo akicheza namba nne na sita, ambapo walikuwa na mechi za kirafiki na timu za Simba ,Yanga, Pan African na Tukuyu Stars.
Anasema kuwa katika mechi hizo za kirafiki walifanikiwa kuifunga Simba bao 1-0, Tukuyu Stars bao 2-0 na Pan Afrika mabao 2-0 na kufungwa na Yanga bao 1-0.
Anabainisha kuwa katika mechi hizo za kirafiki ndipo alipoonwa na viongozi wa timu ya Tukuyu Stars wakatuma watu Kongo kwa ajili ya kumsajili.
“Viongozi wa Tukuyu ndiyo walikuja Kongo na nikafanya nao mazungumzo tukakubaliana, nikasajiliwa kwenye timu hiyo kwa mkataba wa miaka miwili huku nikipewa Dola za Marekani 500 (Sh800,000 za sasa), ili nimalizie mambo yangu. Mkataba ulikuwa ni kiasi cha Dola300 (Sh480,000) kila mwezi ambapo kocha alikuwa Juma Athumani na Mwenge Yavu, huku mfadhili akiitwa ‘kaka’ namfahamu kwa jina moja,”anasema Tshikala.
SAFARI YAKE YA KUICHEZEA YANGA KWA MIAKA MITANO
Tshikala anaeleza kuwa kabla ya kumaliza mkataba wake akiwa na timu ya Tukuyu Stars, wapenzi wa Yanga mkoani Mbeya wakataka ajiunge na klabu hiyo ya mitaa ya Twiga na Jangwani. Anafafanua kuwa mwaka 1996, Yanga walikwenda Mbeya kucheza na Tukuyu Stars katika mechi za Ligi Kuu na matokeo yakawa sare ya bao 1-1.
“Kwenye mchezo huu nilionyesha kiwango cha hali ya juu. Licha ya kuwa kwenye kiwango siku zote, Yanga sikuwahi kukutana nao kutokana na dharura mbalimbali. Lakini hapa nilikutana nao na nilimkaba Mohamed Hussein ‘Mmachinga’, hakufurukuta na wakati huo ndiyo alikuwa mchezaji hatari na mwenye chenga za maudhi. Mimi niliweza kumdhibiti hadi mashabiki wa Yanga wakanikubali,”anasema Banza.
Anasimulia kuwa mechi hiyo ilihudhuriwa na viongozi wakuu wa Yanga wakati huo akiwamo Francis Kifukwe na Frank Mtangi, ambapo baada ya kumalizika kwa msimu huo wa ligi Yanga iliibuka bingwa na Tukuyu wakashika namba nne. Wakati wakijiandaa kucheza Ligi ya Muungano, Yanga walifanya mazungumzo na Tshikala na wakakubaliana kumsajili na kwenda naye Zanzibar.
Anasema kuwa kwake kuondoka Tukuyu haikuwa kazi ngumu kwa kuwa kulikuwa na baadhi ya viongozi wa Tukuyu waliokuwa wapenzi wa Yanga, waliotamani siku moja akacheze Yanga, hivyo alipoamua kuondoka, hakuna aliyeweka pingamizi huku wengine wakimpa na fedha kidogo.
MAGUMASHI WAKATI WA KUSAINI YANGA
Tshikala anasema kuwa wakati anajiunga na Yanga mwaka 1997, hakukuwa na utaratibu wa kusaini mkataba bali kulikuwa na mapatano na walikubaliana wamlipe kiasi cha Dola za Marekani 450 kwa mwezi. Hata hivyo baada ya hapo viongozi walikuwa wagumu kutimiza wajibu wake katika malipo jambo lililofanya jukumu hilo kuwa mikononi mwa Francis Kifukwe peke yake.
“Namheshimu sana Kifukwe, ni mtu mzuri. Baada ya yeye kuwa wa kwanza kunishawishi nijiunge na timu hiyo, alibeba jukumu la kunijali mwanzo-mwisho, hata baada ya uongozi kuacha kunilipia hoteli na mambo kama hayo. Kifukwe alifanya hivyo yeye mwenyewe,”anasema Tshikala.
Anasema kuwa kwa msaada wa Kifukwe aliweza kucheza miaka yote mitano akifundishwa na makocha kama Sunday Kayuni, Rauol Shungu na Juma Pondamali.
VIONGOZI WA SIMBA WAMFUATA
Anasema kuwa mwaka 2000 akiwa bado na Yanga viongozi wa Simba walimfuata kwa lengo la kumsajili kwenye timu yao, lakini kwa heshima yake kwa Kifukwe ilibidi amhusishe.
“Walikuja Mwenyekiti wa Simba wa wakati huo Juma Salum ambaye ni marehemu na Idd Azzan wakitaka nijiunge nao kwa dau la Sh3 milioni na marupurupu kibao.
Lakini nilimwambia Kifukwe akaniambia atanipa hela kama hiyo kwa awamu, kwa bahati mbaya hakuweza na alinipa nusu yake nami kwa kumheshimu sikwenda Simba licha ya kuwepo na masilahi kibao,”anatanabaisha Tshikala.
USHINDI KOMBE LA AFRIKA MASHARIKI NA KATI
Anasema akiwa na Yanga mwaka 1999 walifanikiwa kuchukua Kombe la Afrika Mashariki na Kati katika michuano iliyofanyika mjini Kampala, Uganda.
Anaeleza kuwa katika michuano hiyo walitumia zaidi vipaji kwa kuwa hakukuwa na motisha wala fedha zaidi ya kutumia vipaji na moyo wa kupenda timu uliokuwapo wakati huo.
Anaitaja mechi ngumu kwenye michuano hiyo kuwa ni dhidi ya Lyon Sports ya Rwanda kwa kuwa mechi ya kwanza waliwafunga mabao 2-0, mchezo wa marudiano ilikuwa ni lazima washinde na ikishindikana watakuwa wametolewa kwenye michuano hiyo, lakini walifanya kweli wakashinda mabao 3-0.
Anakumbuka kuwa mwaka 1999-2000 Yanga waliingia robo fainali ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika ambapo waliingia Nane Bora baada ya kuifunga Lyon Sports ya Rwanda nyumbani na ugenini kwa mabao 3-2,kabla ya kucheza na Kofi ya Ethiopia waliyoifunga jumla ya magoli 8-3 katika mechi mbili.
Anasimulia kuwa katika Nane Bora walipangwa kundi moja na Manning Rangers ya Afrika ya Kusini, Raja Cassablanca ya Morocco na Asec Mimosas ya Ivory Coast lakini hawakufanikiwa kusonga mbele na Asec Mimosas, ikifanikiwa kuchukua ubingwa wa kombe hilo.
KIKOSI KILICHOCHUKUA KOMBE LA AFRIKA MASHARIKI NA KATI MWAKA 1999
Anawataja wachezaji aliokuwa nao pamoja wakati huo kuwa ni pamoja na magolikipa Peter Manyika, marehemu Joseph Katuba na Mfaume Athumani.
Wengine ni Mzee Abdallah, Anuary Awadh, Banza Tshikala, marehemu Saidi Mwamba ‘Kizota’, Ally Mayayi, Akida Mapunda, Salvatory Edward, Kally Ongala, Sekilojo Chambua, Mohamed Hussein,’Mmachinga’, Edibily Lunyamila, Shabani Ramadhani, Ephraim Makoye na Bakari Malima ‘Jembe Ulaya’.
“Kikosi hiki sijawahi ona maishani mwangu kilikuwa ni zaidi ya kipaji, sipati neno zuri la kukisifia,”anasema Tshikala.
ZAWADI ALIZOWAHI KUPATA KWA KUCHEZA KWA KIWANGO
Anasema mechi kati ya Yanga na Asec Mimosas, alicheza vizuri kiasi kiongozi mmoja wa Ivory Coast alimpa Dola 200 na kuahidi kufanya mipango ya kumchukua kwenda kucheza nchini humo, ingawa mipango hiyo haikuzaa matunda kutokana na kutokuwepo kwa mawasiliano kati yao.
Anataja zawadi nyingine aliyopata kuwa ni pamoja na kiwanja maeneo ya Tabata, ambacho alipewa na shabiki wa Yanga baada ya kucheza vizuri na kufanikiwa kuwafunga Simba mabao 2-0, wafungaji wakiwa Mohamed Hussein na Sekilojo Chambua, hii ilikuwa mwaka 2000.

Itaendelea Jumamosi Ijayo
Chanzo: Mwananchi, Jumamosi

No comments:

Post a Comment