Mwenyekiti wa Tume ya
Kuchunguza Kushuka kwa Kiwango cha Ufaulu wa Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne
mwaka 2012 Profesa Sifuni Mchome.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mwenyekiti wa Tume hiyo, Profesa
Sifuni Mchome alisema likitaka mitalaa ya shule za msingi hadi vyuo vya ualimu
itazamwe upya.
Tume hiyo iliundwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda Februari 23,
mwaka huu kuchunguza chanzo cha asilimia 65.5 ya wanafunzi kupata daraja la
sifuri kwenye mtihani wa mwaka 2012.
Alisema mapendekezo hayo yatawasilishwa kwa Waziri Mkuu baada ya
Tume kumaliza kazi yake Juni 15 mwaka huu.
“Pendekezo la kufutwa kwa matokeo na kisha kupangwa upya ni moja
tu kati ya mengi. Mpaka sasa tumeandaa zaidi ya mapendekezo 130 na kazi bado
inaendelea,” alisema Profesa Mchome.
Alisema kwa kawaida mtalaa unabadilishwa baada ya kumaliza
mzunguko wake mmoja, hivyo tume hiyo imependekeza kupitiwa upya kwa mitalaa
yote ambayo imemaliza mzunguko. Mzunguko huu ni miaka saba kwa elimu ya msingi,
minne kwa sekondari na miwili kwa kidato cha tano na sita.
“Mtalaa wa sekondari unaweza kupitiwa upya baada ya miaka minne
tangu kuanza kutumika kwake, huu wa Sekondari wa ‘based competence’ (kuangalia
ubora) ulianza kutumika 2006, mpaka sasa tayari umemaliza mzunguko wake na haya
matokeo yametokana na mtalaa huu.
Tume imependekeza mitalaa yote itazamwe upya kuanzia ile ya
shule za msingi mpaka vyuo vya ualimu,” alisema.
Kuhusu vitabu, Tume imependekeza kuangaliwa kwa njia rahisi ya
kutumia teknolojia kuhakikisha vinapatikana badala ya kusubiri mpaka
vichapishwe na kisha kupelekwa kwa wanafunzi.
“Unaweza ukaongea na makampuni ya simu kuwa waweke vitabu kwenye
system (mfumo) yao na wakaanza mashindano kuwa
mwanafunzi atakayesoma sana
atapata zawadi,” alisema na kuongeza.
“Unaweza pia kuongea na kampuni ya magazeti kama Mwananchi
ukawaambia watoe ukurasa wachapishe kitabu fulani kwa mwezi mzima na shule
ziambiwe zinunue nakala moja ambayo kwa mwezi itakuwa Sh30,000 kwa kila shule
na tatizo la vitabu litakwisha.”
Pendekezo jingine alisema ni kuangaliwa upya kwa sheria
mbalimbali za elimu jinsi zilivyo na utekelezwaji wake pamoja na kuhakikisha
madaraka yanapelekwa kwenye ngazi za Serikali za Mitaa.
Kufutwa kwa Matokeo
Akizungumzia kufutwa kwa matokeo hayo, Profesa Mchome alisema
katika uchunguzi wake, tume hiyo haikuwa na shida yoyote juu ya utungaji na
usahihishaji wa mitihani.
“Ndiyo maana tukapendekeza kupangwa upya kwa madaraja,
kitakachofanyika ni kubadilishwa tu kwa kanuni iliyotumika mwaka jana na
kutumia ile ya miaka ya nyuma,” alisema.
Alisema kwa miaka ya nyuma upangaji wa madaraja ulikuwa
unazingatia matokeo ya mitihani jinsi yalivyo na kisha kuyafananisha na miaka
ya nyuma.
“Ukiona kuwa mwaka uliopita somo fulani matokeo yake yalikuwa
hivi, basi unaangalia na ufaulu wa mwaka huu kisha mnaamua kuwa daraja A
lianzie alama fulani, hicho ndiyo kilichopendekezwa.”
“Kilichofanyika mwaka jana, masomo yote yaliwekwa kwenye daraja
fulani bila kuzingatia jinsi ufaulu ulivyokuwa. Kwa hiyo sisi tukaona kwa kuwa
wanafunzi hawa wamesoma kwenye mazingira sawa na yale ya miaka ya nyuma, hakuna
sababu ya kuwabadilishia kanuni.”
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment