Kagera Sugar inaikaribisha Ruvu Shooting ya
Pwani katika mchezo pekee wa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) utakaofanyika kesho (Mei
11 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kaitba mjini Bukoba.
Ingawa timu zote mbili hazipambani kutafuta
ubingwa ambao tayari umetwaliwa na Yanga wala kukwepa kushuka daraja, mechi
hiyo bado ni muhimu kwao katika mazingira matatu tofauti.
Kagera Sugar inayonolewa na kocha mkongwe kuliko
wote katika VPL, Abdallah Kibaden na ikiwa na pointi 40 yenyewe inasaka moja
kati ya nafasi nne za juu ambazo zina zawadi kutoka mdhamini wa ligi, lakini
pia timu zinazoshika nafasi hizo za juu zinapata tiketi ya kucheza michuano ya
BancABC Super 8.
Kwa upande wa Ruvu Shooting ya Kocha Charles
Boniface Mkwasa yenye pointi 31 inasaka moja ya nafasi sita za juu ambazo ni
fursa ya kuingia kwenye Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPL Board) ambayo
inatarajiwa kuundwa baada ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Septemba 28 mwaka
huu.
Wagombea nafasi za uenyekiti na makamu wake ni
lazima watoke katika timu zilizoshika nafasi sita la juu katika VPL msimu
uliopita. Uchaguzi wa TPL Board utafanyika siku moja kabla ya ule wa TFF
uliopangwa kufanyika Septemba 29 mwaka huu.
Raundi ya 25 ya ligi hiyo itakamilika keshokutwa
(Mei 12 mwaka huu) kwa mechi kati ya wenyeji Azam na Mgambo Shooting ya Tanga.
Mechi hiyo namba 169 itachezwa katika Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi,
nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.
Azam yenye pointi 48 inahitaji moja zaidi ili
kutetea nafasi yake ya umakamu bingwa iliyoutwaa msimu wa 2011/2013 na kupata
tiketi ya kuiwakilisha Tanzania
katika mashindano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika.
Wakati Azam ikisaka pointi hiyo moja, Mgambo
Shooting inayofundishwa na wachezaji wa zamani wa mabingwa wa Tanzania Bara
mwaka 1988, Mohamed Kampira akisaidiwa na Joseph Lazaro ni moja ya timu ziko
katika hatari ya kurudi Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu ujao.
Mgambo Shooting inahitaji pointi moja tu katika
mechi mbili ilizobakiza kukwepa kurudi FDL, ikishindwa kupata pointi hiyo huku
Polisi Morogoro na Toto Africans ya Mwanza zikishinda mechi zao za mwisho kwa
uwiano mzuri wa mabao itakuwa imekwenda na maji.
Mechi ya Azam dhidi ya Mgambo Shooting
itachezeshwa na refa Jacob Adongo kutoka Mara, na atasaidiwa na Abdallah Rashid
wa Pwani na Charles Mbilinyi wa Mwanza. Mwamuzi wa mezani atakuwa Idd Lila wa Dar es Salaam wakati
Kamishna ni Omari Walii wa Arusha.
SIMBA, MGAMBO SHOOTING ZAINGIZA MIL 16
Mechi namba 149 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya
Simba na Mgambo Shooting iliyochezwa juzi (Mei 8 mwaka huu) kwenye Uwanja wa
Taifa, Dar es Salaam
na kumalizika kwa Simba kushinda bao 1-0 imeingiza sh. 16,651,000.
Watazamaji 3,006 walikata tiketi kushuhudia
mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh.
20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 3,226,125 wakati Kodi ya Ongezeko
la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 2,539,983.05.
Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya
uwanja sh. 1,640,402.54, tiketi sh. 3,175,000, gharama za mechi sh. 984,241.53,
Kamati ya Ligi sh. 984,241.53, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh.
492,120.76 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 382,760.60.
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment