Monday, May 20, 2013

Ngassa asaini miaka miwili na klabu anayoipenda.

 Hapa akionyesha uzi wa Yanga akiwa na katibu wa timu hiyo Lawrence Mwalusako, wakati alipomtambulisha rasmi mshambuliaji huyo kwa wanahabari leo asubuhi.



 Hapa Ngassa akisalimiana na wadau na viongozi mara baada ya kuzungumza mawili matatu na kuvalishwa rasmi uzi wa Yanga.
 Akikumbatiana na mmoja wa viongozi wa kamati ya udhamini Abdallah Binkleb ambaye ndiye aliyeshiriki kudaka saini ya mshambuliaji huyo.

 Hapa anasaini daftari la wageni, kwa mujibu wa katibu Ngassa alisaini ikimaanisha anakaribishwa nyumbani.

                                             Binkleb akishangilia ushindi wa kudaka saini ya Ngassa.

Hatimaye mwanandinga Mrisho Khalfan Ngassa amerejea nyumbani katika timu ya Yanga ambao ni mabingwa wa soka msimu huu baada ya kumaliza msimu na simba ambayo hakuwa na mapenzi nayo.

Kwa maelezo ya Ngassa ambaye ametambulishwa rasmi asubuhi ya leo katika ofisi za Yanga zilizopo mtaa wa Twiga Kariakoo jijini, amesema anamshukuru Mungu amereje katika timu aliyokuwa akiipenda.

"Ninamshukuru Mungu nimerudi tena nyumbani, watu wanasema ninaipenda Yanga na ni kweli naipenda, namshukuru Rais wa Yanga na viongozi wengine, nawashukuru pia wapenzi wa Azam FC na Simba kwa kunishabikia kwa vipindi tofauti nilivyokuwa huko.

"Simba nimeisaidia sana lakini hawana shukurani, pia nashukuru timu zote nilizocheza msimu huu lakini mbali ya yote nataka watu wajue Yanga ninaipenda na sina namna nyingine ya kufanya zaidi ya kuichezea kwa moyo wote," alisema Ngassa, ambaye aliandamana na viongozi wa Yanga huku mashabiki wakiwa nje ya jengo wakimsubiri kwa hamu.

Naye mwenyekiti wa kamati ya udhamini Abdallah Binkleb, amesema Ngassa amedhihirisha yeye ni mchezaji wa uhakika na mwenye nidhamu ya hali ya juu maana mbali ya kutangaza kuhamia Yanga kwa msimu ujao lakini alicheza mechi yake ya mwisho dhidi ya Yanga akiwa kwa ufundi mkubwa.

"Kila mtu alitegemea baada ya Ngassa kutangaza kuhamia Yanga labda angecheza chini ya kiwango katika mechi ya juzi lakini kwa soka aliloonyesha amedhihirisha yeye ni mchezaji wa uhakika anafanya vizuri katika timu aliyokuwapo kwa wakati huo maana hata penati waliyopata Simba aliisababisha yeye.

"Tulianza mazungumzo na Ngassa miezi sita iliyopita na tunashukuru leo tumempata huyu ni kijana wa Yanga huko kwingine alikwenda kutafuta riziki tu lakini leo ameamua kurudi nyumbani," alisema Binkleb.

Katika hatua nyingine katibu wa klabu hiyo ya maeneo ya jangwani alishindwa kuweka wazi mkataba wa miaka miwili aliyoingia Ngassa kuichezea Yanga ni wa shilingi ngapi, na wamemalizana vipi na Azam ambao ndiwo waliokuwa na mkataba na Ngassa kabla ya kuenda Simba kwa mkopo.

Hata hivyo mkataba alioingia Ngassa na Azam unaisha mwaka huu na kwakuwa alikwenda Simba kwa mkopo hakuna vizuizi vyovyote ambavyo Yanga wanaweza kukumbana navyo kutoka Simba na inawezekana wakampata bila kutumia jasho jingi kwakuwa mkataba wake unakwisha hivyo anaweza kuwa mchezaji huru.

Itakumbukwa mzunguko wa pili katika msimu ulioisha juzi jumamosi Azam walimpeleka Ngassa katika timu ya Simba kwa mkopo ili kuwakomoa Yanga baada ya mchezaji huyo kuibusu jezi ya Yanga uwanja wa taifa wakati Azam walipokutana na Yanga.

"Ili kumshawishi Ngassa kuichezea timu asiyoipenda Simba walimpa milioni 25 na gari, lakini niwaambie kitu kimoja Ngassa anaipenda Yanga kule alikwenda tu kwakuwa hakuwa na la kufanya maana tayari alishakuwa na mkataba na Azam hivyo alipaswa kufanya walivyotaka," alisisitiza Binkleb ambaye ni miongoni mwa watu waliofanya juhudi kupata saini ya mchezaji huyo hatari kwenye ligi ya Tanzania kwa sasa. 

HAFIDH KIDO
kidojembe@gmail.com
20 May, 2013
DAR ES SALAAM, TANZANIA

No comments:

Post a Comment