Mkutano huo unaotajwa kuwa zao la jitihada za Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana unatarajiwa kufanyika kesho na keshokutwa mjini Dodoma, huku kukiwapo taarifa kwamba wabunge wamegawanyika katika makundi kwa lengo la kupenyeza, kisha kutetea hoja walizonazo dhidi ya wenzao.
Miongoni mwa hoja zinazotajwa ni ile ya kushughulikiwa kwa wabunge ambao wamekuwa wakitajwa kwamba ni wapinzani ndani ya CCM, wakiwamo, Alphaxard Kangi Lugora (Mwibara), Deo Filikunjombe (Ludewa), Ally Keissy Mohamed (Nkasi Kaskazini) na Luhaga Mpina (Kisesa).
Wabunge hao wanatuhumiwa na wenzao kwamba wanawasaidia wapinzani kutokana na misimamo yao ya kuikosoa hadharani Serikali katika vikao na mikutano tofauti ya Bunge.
Itakumbukwa kuwa Aprili 25 mwaka huu baada ya kukwama kwa Bajeti ya Wizara ya Maji, wabunge wa CCM walikutana katika kikao cha dharura kilichoongozwa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ambako Lugola na Filikunjombe walishambuliwa kutokana na kile kilichodaiwa kwamba wamekuwa wakiidhalilisha Serikali ya CCM bungeni.
Habari zilidai kwamba waliowashambulia wabunge hao ni wenzao, Saidi Nkumba (Sikonge) na Livingstone Lusinde (Mtera), huku wakitetewa na Beatrice Shellukindo (Kilindi) na Peter Serukamba (Kigoma Mjini) ambao walikaririwa wakisema kwa nyakati tofauti kwamba hawajakosea chochote kwani wanaeleza hali halisi ilivyo.
Baada ya mjadala huo, Pinda alikaririwa akimwelekeza Katibu wa Wabunge wa CCM, Janister Mhagama kumwandikia barua Katibu Mkuu wa CCM, Kinana kuhusu suala hilo ili liwe ajenda watakapokutana na Rais Kikwete.
Hata hivyo, kuna taarifa kwamba huenda hoja hiyo ikakosa nguvu kutokana na msimamo wa sasa wa Kinana ambaye anawaona wabunge wa CCM kama ni wapole, hali inayosababisha wale wa vyama vya upinzani hasa Chadema kupata nguvu.
Kutokana na hali hiyo, ni dhahiri kwamba Rais Kikwete atakuwa na wakati mgumu wa ama kukubaliana na hoja za wale wanaokosoa wenzao kwa kuikosoa Serikali au kuegemea upande wa Kinana ambaye kimsingi anaunga mkono ukosoaji unaofanywa na wabunge.
Harufu ya kile kinachodaiwa kuwa ni maandalizi kwa ajili ya mkutano huo ilianza kunukia jana pale Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alipomtaka Lugola kuwasilisha ushahidi wa majina ya mawaziri aliodai kwamba wanajihusisha na biashara ya dawa za kulevya, ili ayafikishe kwa Rais Kikwete kwa hatua zaidi.
“Kila mtu anatakiwa aipime kauli yake kabla hajaitamka, kama Lugola ana ushahidi aulete mbele ya Bunge na tutayapeleka kwa Rais,” alisema Pinda wakati akijibu swali la Mbunge wa Tumbe, Rashid Ally Abdallah aliyesema anaamini hakuna waziri anayejihusisha na biashara hiyo kwani mchakato wa kuwapata hufanywa kwa umakini wa hali ya juu.
Abdallah alikuwa akirejea kauli iliyotolewa na Lugola mwezi uliopita kwamba atawasilisha bungeni majina ya watendaji wa Serikali wanaopokea rushwa ili kuficha majina ya mawaziri wanaojihusisha na dawa za kulevya na kwamba kauli hiyo ni nzito inayolidhalilisha Bunge.
Pinda ambaye alikuwa akijibu maswali ya papo kwa papo alisema licha ya kwamba anaheshimu kauli ya kila mbunge, Lugola anatakiwa kuleta ushahidi kamili na majina ya mawaziri.
Kuulizwa kwa swali hilo kunatafsiriwa na wachunguzi wa mambo kwamba inaweza kuwa moja ya maandalizi ya kwenda ‘kuwashtaki’ Lugola na wenzake mbele ya Rais Kikwete kwamba wamekuwa wakiichafua CCM na Serikali yake.
Chimbuko la mkutano
Habari ambazo gazeti hili limezipata zinadai kuwa chimbuko la mkutano wa Rais na wabunge wa CCM ni madai yao ya muda mrefu ambao mara kadhaa wameeleza kutoridhishwa na mambo yanavyokwenda serikalini.
Hoja kubwa ya wabunge ni matumizi mabaya ya vikao vya wabunge wa chama hicho (party caucus) ambavyo wanadai vimekuwa vikitumiwa na Serikali kuwabeba kwa kuwasafisha na kuwatetea watendaji wabovu serikalini, wakiwamo mawaziri wasiokuwa na uwezo.
“Malalamiko haya ni ya muda mrefu, wanadai (wabunge) kwamba vikao vyao vinaitishwa tu pale kunapokuwa na mpango wa kuiokoa Serikali bungeni, lakini hakuna vikao vingine ambako wanakaa kwa ajili ya kuishauri Serikali yao,” kilisema chanzo chetu na kuongeza:
“Lakini pia wanalalamika kwamba hata hao watendaji wa Serikali wanaowatetea bungeni hawako makini na wala Serikali haiwachukulii hatua zozote wanaendelea tu kuharibu.”
Chanzo hicho kilidai kuwa wabunge wa CCM wanaona kwamba kwa kutetea uozo ulio dhahiri mbele ya umma, wamekuwa wakiyaweka majimbo yao rehani na kuonekana kama watu wasio na uwezo mbele ya wapiga kura wao.
Habari hizo zinasema kuwa ajenda nyingine ni kusuasua kwa miradi mingi ya maendeleo, ajenda ambayo imejikita katika mgawanyo wa rasilimali za nchi usiozingatia vipaumbele vya maendeleo na ufujaji wa fedha za umma.
Wabunge hao wanadaiwa kwamba wanarejea maelezo ya mawaziri katika bajeti ambayo yanaonyesha kwamba hadi robo tatu ya Mwaka wa Fedha 2012/13, wizara nyingi zilikuwa hazijapokea hata nusu ya fedha zilizoidhinishwa na Bunge ilhali takwimu za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), zikionyesha kuwa kiasi kikubwa cha fedha kimekusanywa na wakati mwingine kuvuka malengo yaliyowekwa.
“Wabunge wanahoji fedha za nchi zinakwenda wapi? Maana kama TRA wanakusanya fedha kwa asilimia 108 halafu fedha hazifiki kunakohusika maana yake kuna tatizo kubwa kwenye mfuko mkuu wa Serikali (Hazina),” kilisema chanzo kingine kutoka ndani ya CCM.
Juzi, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kikao hicho kitatoa nafasi zaidi kwa wabunge kueleza masuala yanayohusu utekelezaji wa Ilani ya CCM katika majimbo yao.
Licha ya Nape kusema kwamba kikao hicho hakitahusu yale yanayotokea katika mkutano wa sasa wa Bunge la Bajeti, ni dhahiri kwamba masuala hayo hayaepukiki hasa ikizingatiwa tofauti za wazi miongoni mwa wabunge wa CCM.
Kadhalika, suala la kutotekelezwa kwa ahadi za Rais wakati wa kampeni za 2010 linaweza kuibuka kwani ni jambo ambalo limekuwa likijitokeza katika mijadala kadhaa ya wizara zilizowasilisha bajeti zake bungeni.
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment