Mtuhumiwa wa kurusha Bomu kwenye Kanisa Katoliki la Mtakatifu
Joseph,Parokia ya Olasiti ,Jimbo Kuu la Arusha,Victor Ambrose Calist akiwa
kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha baada ya kusomewa mashtaka 21 ya kuua na
kujaribu kuua.Picha Filbert Rweyemamu.
Polisi imewaachia huru raia wanne wa kigeni waliokuwa
wakishikiliwa kuhusiana na tukio la bomu katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Parokia ya Olasiti.
Kamanda Sabas aliwaambia waandishi wa habari ofisini kwake jana
kuwa raia hao walikamatwa baada ya kutiliwa shaka walipoonekana wakitoka kwenye
hoteli moja karibu na Kituo Kikuu cha Mabasi Arusha, muda mfupi baada ya tukio hilo .
Raia watatu wa Falme za Kiarabu(UAE), walioshikiliwa na kuachiwa
wamegundulika kuwa ni watumishi wa Serikali.
Kamanda Sabas aliwataja kuwa ni Abdul Azziz Mubarak (30),
(Mamlaka ya Mapato), Fouad Saleem Ahmed Al Hareez Al Mahri (29), (Zimamoto) na
Daeed Abdulla Saad (28), ambaye ni Askari wa Usalama Barabarani.
Raia hao pamoja na mwenzao, Al-Mahri Saeed Mohseen (29) kutoka Saudi Arabia ,
walikabidhiwa kwa Idara ya Uhamiaji kuchunguzwa iwapo waliingia nchini kihalali.
Waliachiwa katika kipindi ambacho Serikali ya Tanzania
ilikuwa ikikabiliwa na shinikizo kutoka kwa mabalozi wa nchi wanakotoka
wakipinga kukamatwa kwao na kutangazwa kwenye vyombo vya habari. Mabalozi wa
nchi hizo za Mashariki ya Kati walifuatana na wanasheria wao kwenda kuangalia
hali za watuhumiwa kutoka nchi zao huko Arusha.
Balozi wa Saudi
Arabia , Hani Abdalla Momenah aliliambia
gazeti la Al-Hayat la nchi yake akidai watu wao alikamatwa kwa hisia tu.
“Tuna matumaini makubwa kuwa watu wetu wataachiwa huru na
tutaendelea kufuatilia suala lao hadi tuone mwisho wake,” alieleza Balozi huyo,
ambaye akisisitiza asingeondoka Arusha hadi kieleweke.
Kaimu Kamanda wa Uhamiaji Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi,
Vitalis Mlay alisema tayari wageni hao wameondoka nchini kupitia Uwanja wa
Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es
Salaam .
Raia hao waliingia nchini Mei 4, mwaka huu, siku moja kabla ya
tukio hilo la
bomu na walifika Arusha alfajiri ya siku ya tukio na kwamba wangekaa nchini kwa
shughuli za kitalii kwa siku tatu.
Hata hivyo mtuhumiwa mmoja kati ya tisa waliotiwa mbaroni kuhusiana
mlipuko huo wa bomu amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu kazi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Wilaya ya Arusha
na kusomewa mashtaka 21 yakiwamo ya mauaji na kujaribu kuua.
Mbele ya Hakimu Mkazi, Devotha Kamuzora, mtuhumiwa huyo, Victor
Ambrose (20), dereva wa Bodaboda na mkazi wa eneo la Kwa Mromboo, Arusha
alisomewa mashtaka hayo yakiwamo matatu ya mauaji ya watu watatu waliofariki
katika tukio hilo
lililotokea Mei 5, mwaka huu.
Wakisoma kwa kupokezana hati ya mashtaka, Mawakili wa Serikali,
Zachariah Elisaria na Haruna Matagane walidai Calist pia anatuhumiwa kwa makosa
18 ya kujaribu kuua.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mahakamani hapo kimyakimya akiwa chini
ya ulinzi wa maofisa wa polisi na hakutakiwa kujibu lolote kwa sababu mashtaka
yanayomkabili yanapaswa kusikilizwa na Mahakama Kuu.
Kesi hiyo imeahirishwa hadi Mei 27, mwaka huu itakapotajwa tena
na mtuhumiwa amerudishwa mahabusu.
Saa moja kabla ya Ambroce kupandishwa kizimbani saa nne asubuhi,
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas aliitisha mkutano na
waandishi wa habari kitendo ambacho kiliwafanya baadhi yao
kushindwa kufuatilia vyema tukio hilo .
Mtaalamu mwingine alichambua bomu
Ofisa Usalama Mwandamizi katika Shirika la Umoja wa Mataifa (UN)
ameunga mkono kauli Polisi mkoani Arusha kwamba uchunguzi wa awali umeonyesha
kwamba bomu lililolipuliwa halikutengenezwa kienyeji akisema maelezo aliyopata
huenda limetengenezwa kiwandani.
Kapteni huyo wa zamani wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania
(JWTZ), aliyekataa kutaja jina lake, alisema msingi wa maelezo yake ni kutokana
na vyuma vilivyotawanyika na kuumiza zaidi ya watu 20.
“Mabomu ya aina hii nayafahamu kwani yanatumika vitani zaidi na
ni mahsusi kwa kutupa kwa mkono,”
MWANANCHI
No comments:
Post a Comment