Hotuba hii ilitolewa mwaka 1995 na hayati baba wa
Taifa Mwalimu Julius Nyerere katika sikukuu ya wafanyakazi iliyofanyika kitaifa
mjini Mbeya. Hotuba hii maarufu ya ‘Tumetoka wapi, tupo wapi na tunakwenda
wapi’ ililenga kumwamsha kutoka usingizini mfanyakazi wa Tanzaniana Afrika kwa
ujumla.
Nimeamua kuirudia nusu wakuwa historia imejirudia
mwaka huu pia maadhimisho ya sikukuu hiyo kitaifa yanafanyika Mbeya, tena
katika kipengele muhimu cha historia ya vyama vya wafanyakazi duniani, lengo ni
kujikumbusha malengo na nia ya wafanyakazi wa miaka iliyopita kufikiria
kuanzisha umoja wao ili kuwasaidia wanyonge kutoa mawazo yao kwa njia za siri na dhahiri.
Mwalimu
Nyerere alianza kuelezea chimbuko la vyama vya wafanyakazi kwa kusema; Wazo la
kuwa na vyama vya wafanyakazi duniani, kwamba wawe na mshikamano na umoja wa
kutetea maslahi yao sio wazo la Tanzania
wala la nchi zilizoendelea. Kusema kweli, kwa historia, lilianza huko Marekani
na lilikubalika.
Wafanyakazi
wa wakati huo, katika nchi ambazo maendeleo yake yalikuwa mazuri, waliamua wafanye
mshikamano wa kuleta maendeleo yao
na hasa ya kupambana na waajiri wao.
Mwajiri
anaanzisha shughuli yake na anafanya kwa nguvu zake mwenyewe. Anataka kulima na
analima kwa nguvu zake mwenyewe. Kama anataka
kufungua kiwanda chake cha mbao, maana ninyi ni wafanyakazi inapasa nizungumzie
habari ya viwanda badala ya kilimo, anafungua kiwanda chake cha kutengeneza
samani. Anaweza kutumia vitu vyake mwenyewe na akawa anafanya kazi na seremala
mmoja. Atakuwa amepata randa, meza, patasi na kila kitu chake.
Anafanya
kazi yake mwenyewe, anatengeneza vitu vyake, anauza na anapata hicho
anachokipata. Hicho anachokipata kinatokana na nguvu yake mwenyewe. Anataka
mbao na anatengeneza. Mtu anamwendea na kumwambia, “mimi nataka meza bwana”,
anamtengenezea.
Inabidi
mwenyewe ashughulike na meza hii mpaka inakuwa nzuri. Anapata kile anachopata.
Nyingine anafidia zile gharama zake za meza, randa na za vyombo vingine vyote
hivyo. Halafu, kinachobaki cho chote, ndiyo maslahi yake. Lakini, kile
anachopata kinatokana na jasho lake
mwenyewe . Akitoka hapo,
anaweza kuwa mshiriki na mwenzake, washirikiane wote wawili na sio kwamba mmoja
atamwajiri mwingine. Hapana! Wote wawili watafanya kazi kwa pamoja.
Watasaidiana vizuri zaidi wakifanya pamoja. Wao, vile vile, wanaweza wakapata
maslahi kutokana na nguvu zao wenyewe.
Mwanzo
wa dhuluma ya unyonyaji:
Wakitoka
hapo nao wakajifanya ni waajiri wanaotaka kuwaajiri wengine, shughuli ile si ya
hawa walioajiriwa tena. Ni ya hawa wawili tu. Wakisha kuwaingiza wengine, hao
si yao . Wanasema.
Sasa njoo hapa tusaidie kutengeneza meza, vitanda, madirisha na milango.
Lakini, meza inapokuwa imekwisha, tunaiuza. Si mali yenu ninyi wafanyakazi. Ni mali
yetu. Ninyi chenu humu ni ule mshahara na wala sio faida itakayopatikana humu.
Faida,
‘baada ya kutoa gharama zote za ununuzi wa mbao, usafirishaji wa mbao zote zile
pamoja na gharama za kuwaajiri ninyi mwitoe meza hii - kwa kuwa mishahara yenu
ni sehemu ya gharama’ nikitoa gharama zote hizi, kinachobakia ni changu.
Sasa
ile inayobaki, baada ya kutoa gharama hizo, inaweza kuwa kubwa na inaweza kuwa
ndogo. Inategemea sana
gharama zilikuwaje. Kama gharama za kununulia
mbao zilikuwa kubwa, zinanipunguzia faida yangu. Kama gharama za wafanyakazi ni
kubwa mishahara ya wafanyakazi kama ilikuwa
mikubwa, inanipunguzia faida yangu. Kwa hiyo, sipendi vyote viwili. Sipendi
muuza mbao aniuzie aghali na sipendi mfanyakazi adai mshahara mkubwa. Napenda
wote waniuzie rahisi. Nataka mbao kiurahisi, nataka mishahara iwe chini. Hapo
ndipo ninapopata faida kiuchumi.
Hili
sijambo la ajabu la wazungu wenzetu wanaojua bali ni la kila mtu mwenye akili kama zenu kutokana na mtiririko wa mantiki wa hoja
yenyewe. Kwamba, mimi nataka mshahara wenu uwe mdogo kwa kuwa faida yangu
inatokana na mshahara wenu kuwa mdogo. Sasa ninyi mtasema: ALAA Bwana Mkubwa,
kazi tufanye sisi halafu wewe utupe mshahara mdogo. Tukufanyie kazi wewe? Basi
uone iwapo tutakufanyia.
Umoja
na mshikamano ndio silaha ya kupambana na dhuluma ya unyonyaji, Kama watakuwa wananiambia
mmoja mmoja, nitawafukuza. Unakuja peke yako na unaniambia ‘Lakini Mzee sasa
mimi nataka uniongeze mshahara.’ Nitakuambia. Unaniambia nini wewe? Unasema
nikupe mshahara wa shilingi ngapi? Utajibu. ‘Ah, kama
utakavyoona, lakini uniongeze. Mungu anaona na Mtume.’ Nikaona kidomodomo chake
huyu Nikamuambia: Unataka mshahara huo ninaokupa sasa hivi? Nyamaza na nenda
kafanye kazi huku utachagua. Kama hutaki, toka.
Kazi sikukuomba. Ulikuja mwenyewe.
Nitakutisha
hivyo. Ukifikiri mchezo, nitakufukuza. Na wenzako watajua kafukuzwa kwa nini
yule. Amedai mshahara mwingi. Mimi kimya! Wengine hawatathubutu tena maana
watafikiri. Nikisemasema hapa na mimi nitatimuliwa na watoto wana njaa.
Nikitimuliwa nitapata taabu. Wewe unaonaje?
Anaendelea
huyu kukunyanyasa. Kama anaweza kuwanyonya wauza
mbao na kukunyonya wewe mfanyakazi, atawanyonyeni wote mpaka wauza mbao
washirikiane kwa pamoja wapate bei nzuri. Mpaka wafanyakazi washirikiane kwa
pamoja wapate mishahara mizuri. Bila kushirikiana, hawapati mishahara
mizuri.
Hii
ndiyo asili ya kuanzisha Vyama vya Wafanyakazi. Nasema hamkuvianzisha ninyi
vilianzishwa zamani, tena Marekani. Lakini, Marekani havikuwa na nguvu sana . Vilikuwa na nguvu
zaidi Ulaya. Hata hivyo, havina nguvu sana
tena Ulaya. Sitaki kuingilia na kuliendeleza hili kwa kuwa viongozi wenu kama wanaelewa, watawaelezeni.
Zamani,
Vyama vya Wafanyakazi vilianzisha mshikamano wa Wafanyakazi Duniani. Kauli mbiu
yake ilikuwa ‘Wafanyakazi Duniani Unganeni. Hamna cha Kupoteza isipokuwa
minyororo yenu.’ Mantiki ya kauli mbiu hiyo ilikuwa kwamba, kwa kuwa mmefungwa
minyororo na mmenyonywa unganeni. Huo ulikuwa ndio ujumbe wa kauli mbiu hiyo
kwa Wafanyakazi Dunia nzima. Hata hivyo, sisi hatukuwapo.
TUMETOKA WAPI?
Azimio la Arusha na Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea.
Tukaweka
kitu kimoja hapa kinaitwa Azimio la Arusha. Leo narudia kusoma Azimio la Arusha
hata kama hamlitaki. Kama kuna watu Tanzania
hawajali, wachukue waanze kulisoma ili waone na waniambie wanachokiona mle
kibaya ni nini hasa. Asome tu kwa dhati tu na kisha aseme hiki ni kibaya.
Siasa
ya Ujamaa.
Linasema
Azimio la Arusha, kwa msingi kabisa, kwamba “Nchi yetu ni ya Wakulima na
WafaƱyakazi”. Sasa mnasemaje? Imeacha kuwa ni nchi ya Wakulima na Wafanyakazi?
Kwa hiyo, kama tunaijenga nchi hii, tunaijenga
kwa faida ya Wakulima na Wafanyakazi. Ndivyo Azimio Ia Arusha linavyosema.
Ukweli huo umekwisha? Umefutika? Umefutwa na nani? Nini kimefuta ukweli huo
kwamba nchi hii ni ya Wakulima na Wafanyakazi? Ninyi hapa ni Wakulima na
Wafanyakazi.
Mtaona
wafanyabiashara wadogo wadogo, siku hizi wengine wanaitwa Wamachinga. Lakini,
hasa hasa, nchi hii bado ni nchi ya Wakulima na Wafanyakazi. Kama
tutafanya jitihada za kuijenga nchi hii, tutajenga uchumi wake na huduma zake
za umma ambazo lazima ziwafae Wakulima na Wafanyakazi. Hali hiyo imebadilika
lini?
Siasa
va Kujitegemea.
Tukasema
kwamba “Hatuna budi kujenga nchi hii kwa kujitegemea”. Hatuwezi kuwa tunataka
maslahi yetu ya Watanzania ya afya bora, maisha bora na elimu nzuri lakini eti
tudhani tunaye mjomba huko nje atakuja kutuletea maslahi hayo.
HATUNA!
Tutajenga nchi hii kwa faida yetu wenyewe sisi wenyewe. Akipatikana mtu
kutusaidia, tutamshukuru. Lakini kazi ya kujenga nchi hii kwa manufaa ya
Watanzania wote ni kazi ya Watanzania, si kazi ya mtu mwingine. Msimamo huo
tukauita Siasa ya Kujitegemea.
Msingi
huo umekufa. Hivi mmeshapata mjomba? Hivi kweli mtawadanganya Wafanyakazi hawa
msiwambie “chapeni kazi kama mnataka maslahi
yenu yaboreshwe, tuchape kazi kwa faida yetu!” Tuache kuwambia wakulima kwamba
“kama tunataka maendeleo, tuchape kazi hivyo
hivyo”. Hivi mtawaambia hawa kwamba “tumeshapata mjomba msiwe na wasiwasi!”
Mjomba huyo ni nani? Mimi nitafurahi kumwona. Nitakwenda kumwona, lakini
sitamwuliza lo lote. Nitafurahi kumwona. Halafu mkinionyesha, “ndiye huyu
mjomba”, nitacheeka!! Hali ya nchi hii haijabadilika hata kidogo. Tanaweza
kujenga nchi kwa maslahi ya Watanzania kwa siasa ya kujitegemea tu, lakini kwa
manufaa ya wote. Manufaa ya wote ndicho tulichokiita ujamaa.
Nchi
ya Kijamaa.
“Nchi
ya Ujamaa”, tukasema, “ni nchi ambako kila mtu anafanya kazi. Kama ni mkulima,
anafanya kazi; kama ni mfanyakazi, anafanya
kazi”. Lililokuwa la msingi na linalotawala ni mfanyakazi: maslahi yanatokana
na kazi yake na jasho lake. Watu ambao hawana ulazima, kimsingi ya kupata
maslahi yao
kutokana na jasho lao wenyewe wapo.
Watoto
wadogo hawana jukumu hilo .
Eti chakula chao kitokane na nguvu zao wenyewe? Hao ni wanyonyaji wa haki sawa
kwani wanawanyonya mama zao. Ni haki yao .
Lakini zee na madevu yake hatulitazamii limnyonye mama yake. Watoto wadogo tu
wanayo haki hiyo. Vile vile, kuna watu ambao hawana uwezo wowote ule wa
kujifanyia kazi- sio uwezo wa kutokuwa na kazi!
Wako
watu hawawezi. Wana vilema fulani ambao hawawezi kufanya kazi wajipatie riziki
kwa kazi na kwa nguvu zao wenyewe. Hawa wana haki ya kulishwa na kutunzwa na
umma pamoja na jumuiya zote. Hali kadhalika, wako watu wazima ambao wamefanya
kazi zao. Walipofika umri wao wa kushindwa, hawawezi kufanya kazi tena. Ah,
basi tena. Hawajiwezi hawa, tuwatunze. Hawa ni haki kuwatunza. Wamo watu wa
aina hiyo wanajulikana kila mahala.
Nchi ya Kibepari
Hata
hivyo, mbali ya makundi hayo, wapo watu wengine ambao wanapata riziki yao kwa kufanya kazi na wengine wanapata riziki yao kwa kafanyiwa kazi.
Nasema
nchi ya namna hiyo inaitwa ya kibepari. Nchi inakubali wengine wafanye kazi na
kupata riziki yao kwa jasho kama inavyosema
misahafu, wengine wanafanya kazi kwa kunyonya kama watoto wadogo kama vile vilema na vizee. Ni majitu yanakaa na uwezo wao
yanatumia wengine kama vyombo. Kwa hiyo,
mfanyakazi na randa ni sawa sawa. Nasema nchi ya namna hiyo inaitwa ni nchi ya
kibepari. Sasa katika dunia ya siku hizi maneno hayo si mazuri sana kuyasema.
Na
mimi nawakumbusheni tu na wala sijayasema! Mimi sina taabu, nawakumbusheni tu.
Hili Azimio la Arusha, ambalo sasa mnalitemea mate, lilikuwa linasema hivyo na,
kutokana nalo, kuna mambo fulani tukaanza kuyapata.
Kujenga uƧhumi wa viwanda
Tukaanza
shughuli ya kujenga uchumi wetu. Natumaini nitazungumzia hili la viwanda. Nchi
zinazoendelea duniani ‘kama Marekani ya
Kaskazini, Marekani yenyewe na Kanada, Ulaya, hasa Ulaya Magharibi na Japani’
na maana moja ya kuendelea ni kwamba uchumi wake unategemea viwanda. Viwanda
ndivyo vinatengeneza vipaza sauti, kamera zetu tunazotumia sasa
nakadhalika.
Maana
ya maendeleo ya leo ya uchumi wenye nguvu ni maendeleo ya viwanda. Nchi yenye
viwanda tunasema ni nchi iliyoendelea. Hata hivyo, tuna maana nyingine ya nchi
zilizoendelea ya kuziita ni nchi zenye viwanda. Nchi haiwezi kuendelea bila
kuwa na viwanda vya kisasa.
Wakati
tunajitawala, hatukuwa na viwanda. Tulikuwa tunalima kahawa, mkonge na pamba,
lakini tunauza vyote nje. Mimi najua kidogo historia ya Uingereza, ilikuwa
ndiyo nchi ya kwanza duniani kuanza maendeleo ya kisasa ya viwanda.
Sekta
moja ya viwanda waliyoanza nayo, ambayo ilikuwa rahisi wakati huo na leo ni
rahisi zaidi, ilikuwa ya kutengeneza nguo. Waingereza wakaitumia na wakajenga
viwanda. Nguo zao zikawa zinatokana na viwanda vyao.
Vile
vile, walikuwa wana dola kubwa. Walikuwa wanatutawala sisi Afrika, wanawatawala
Asia na wanatawala sehemu nyingine za Amerika, lakini hasa Afrika na Asia . Walipoingia India , walikuta Wahindi tayari
wanatengeneza nguo zao kwa mashini. Wakawaza “hata Wahindi nao wanatengeneza
nguo! Haina maana”. Wakawazuia Wahindi kutengeneza nguo kusudi soko duniani
liwe la Waingereza: liwe huru lisizuiwe zuiwe.
Namna
moja kulifanya soko hilo
kuwa huru ilikuwa ni kwa kuvitawala vijitu hivi, halafu unauza vitu vyako.
Wenyewe ndivyo walivyoanza na viwanda vya nguo na, baadaye, wakaongeza vingine
na hatima yake, Waingereza wakawa wakubwa. Wenzao duniani wakaona “Alaa
hivi Vingereza tunaviachia vinaendelea namna hii kwa nini?”. Wakaanza mambo,
wakagombana gombana, wakapigana pigana na wakanyang’ anyana.
Tulipojitawala
mwaka sitini na moja tulikuwa tunajua mambo haya, ijapokuwa tulikuwa wachache,
kwamba nchi haiwezi kuendelea na kuwa ya kisasa bila viwanda. Mtawachumia pamba
wakubwa hawa na kukata miwa. Hiyo ilikuwa sababu moja ya kuleta utumwa ili
kuwachukua Waafrika waende Marekani wakachume pamba na wakakate miwa.
Baada
ya kupata uhuru tukajiuliza. Leo tunajitawala, tuendelee kuchuma pamba na
kukata miwa? Tukaamua: Tuanze kujenga viwanda kwa kuwa sisi tunalima pamba. Kwa
hiyo, shughuli ya kwanza kabisa tutakayoanza nayo ni ya kujenga viwanda vya
nguo.
Nikawaomba
wanaojua mambo haya ya viwanda duniani. Wakati huo sisi wenyewe hatukuwa na
watalaam. Nikawaeleza watu hawa maneno haya: Hivi tunajitawala, tuendelee kuuza
pamba ghafi nje? Nataka nianze kutengeneza nguo hapa Tanzania .
Wakanishauri
na wakaniambia Mwalimu, mnaweza kuanza kutengeneza nguo kutoka pamba yenu hapa.
Jenga uwezo ili Tanzania
iweze kutumia asilimia themanini na tano (85%) ya pamba inayolimwa Tanzania
kutengeneza nguo hapa hapa.
Walinishauri
nijenge uwezo ndani ya Tanzania
wa kutumia asilimia themanini na tano (85%) ya pamba yetu hapa hapa. Asilimia
kumi na tano (15%) ya pamba iliyobaki, ama tunaweza tuitumie wenyewe hapa hapa
au tunaweza kuiuza nje. Hiyo ilikuwa safi sana , kwamba tujenge
viwanda kwa makusudi kabisa.
Wakati
ule, hata mimi ningekuwa na sera za kibepari, ningejenga viwanda. Mabepari ndio
walioanza viwanda na viwanda vyenyewe hivyo havikuwa na sera ya ubepari au
ujamaa. Vilikuwa ni viwanda tu! Sasa tukaanza kujenga viwanda vya nguo na sasa sitaki
kusema sana juu
ya jambo hili.
HAFIDH
KIDO
DAR
ES SALAAM , TANZANIA
1st
May, 2013
No comments:
Post a Comment