Monday, May 13, 2013

Hatma ya dhamana ya Lwakatare kujulikana leo mahakama ya Kisutu.


Dar es Salaam. Jopo la mawakili wanaomtetea Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare leo linaanza harakati za kumtoa mahabusu kwa dhamana.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, kumfutia Lwakatare mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakimkabili yeye na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura, ambayo hayana dhamana na kubaki na shtaka moja la kula njama ambalo linadhaminika.
Kesi hiyo namba 6 ya mwaka 2013, inayosikilizwa na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, inatajwa leo, lakini mawakili wa Lwakatare wamejipanga kumwombea dhamana Lwakatare.
Mmoja wa mawakili wa Lwakatare, Peter Kibatala aliliambia Mwananchi jana kuwa kwa kuwa kosa lililobaki linadhaminika, basi jambo moja watakalolifanya leo ni kuwasilisha maombi ya dhamana.
“Kwa kuwa shtaka lililobaki linadhaminika na kwa kuwa tayari file (jalada) la kesi limesharejeshwa (Kisutu) kutoka Mahakama Kuu, basi tutakachokifanya kesho (leo) ni kuomba dhamana tu,” alisema Wakili Kibatala na kuongeza:
Kama hapatakuwa na pingamizi lolote tunaamini kuwa leo anaweza kutoka kwani tumejiandaa kutekeleza masharti yoyote yatakayotolewa na mahakama.”
Ikiwa hapatakuwa na pingamizi lolote la kisheria kutoka upande wa mashtaka ambalo litaibua mabishano makali, huenda mahakama ikatoa uamuzi wa maombi ya dhamana leo, na kama watuhumiwa wataweza kutimiza masharti yatakayowekwa na mahakama, basi Lwakatare anaweza kurejea uraiani leo.
Hata hivyo, kama kutakuwa na pingamizi la kisheria na mabishano mahakama, inaweza kuahirisha na kupanga siku nyingine ya kutoa uamuzi wa maombi hayo ili kupata muda wa kutafakari kwa kina hoja za kisheria za pande zote zitakazokuwa zimetolewa.
Lwakatare na Rwezaura walikuwa wakikabiliwa na mashtaka manne, matatu kati ya hayo yakiwa ya ugaidi na moja la kawaida la jinai. Mashtaka hayo yalikuwa ni kula njama, kupanga kumteka Dennis Msacky na kisha kumdhuru kwa kutumia sumu na kufanya mkutano wa vitendo vya kigaidi.
Mashtaka hayo matatu yalikuwa yakiwakabili washtakiwa wote wawili wakati shtaka la nne la kuhamasisha vitendo vya ugaidi lilikuwa likimkabili Lwakatare peke yake, akidaiwa kuruhusu nyumba yake ya Kimara King’ongo kutumika kupanga mipango ya ugaidi.
Hata hivyo, Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka matatu ya ugaidi na kubakiwa na shtaka moja tu la kula njama za kutenda kosa la kumdhuru Msacky kwa kutumia sumu.
Uamuzi huo wa Mahakama Kuu ulitokana na maombi ya jopo la mawakili wa Lwakatare waliyoyawasilisha mahakamani hapo wakiiomba ipitie uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka, kuwafutia kesi ya awali na kisha kuwakamata na kuwafungulia tena kesi ya mashtaka hayohayo.
Hata hivyo, wakati wa usikilizwaji wa maombi hayo, mawakili wa Lwakatare walihoji pia uhalali wa mashtaka hayo kuitwa ya ugaidi kwa kuwa hayakuwa ana maelezo yanayoonyesha kuwepo kwa viashiria vya ugaidi.
Katika uamuzi wake, Jaji Lawrence Kaduri alikubaliana na hoja za mawakili wa Lwakatare kuwa mashtaka hayo hayana maelezo ya kutosha hivyo kuyafuta matatu.
MWANANCHI

No comments:

Post a Comment