Saturday, May 4, 2013

YANGA, COASTAL UNION ZAINGIZA MIL 66
Mechi namba 172 ya Ligi Kuu ya Vodacom kati ya Yanga na Coastal Union iliyochezwa juzi (Mei 1 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na kumalizika kwa timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 imeingiza sh. 66,022,000.

Watazamaji 11,478 walikata tiketi kushuhudia mechi hiyo ambayo viingilio vilikuwa sh. 5,000, sh. 8,000, sh. 15,000 na sh. 20,000 huku kila klabu ikipata mgawo wa sh. 15,378,927.45 wakati Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) iliyolipwa ni sh. 10,071,152.54.

Kiingilio cha sh. 5,000 ndicho kilichovutia watazamaji wengi ambapo waliokata tiketi hizo walikuwa 10,230 na kuingiza sh. 51,150,000 wakati idadi ndogo ya washabiki ilikuwa ya kiingilio cha sh. 20,000 kilichovutia washabiki 69 na kuingiza sh. 1,380,000.

Mgawo mwingine wa mapato hayo ni asilimia 15 ya uwanja sh. 7,819,793.62, tiketi sh. 3,818,890, gharama za mechi sh. 4,691,876.17, Kamati ya Ligi sh. 4,691,876.17, Mfuko wa Maendeleo ya Mpira wa Miguu (FDF) sh. 2,345,938.09 na Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) sh. 1,824,618.51.

wakati huohuo taarifa za TFF zinaeleza kuwa, Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) inaendelea Jumapili (Mei 5 mwaka huu) kwa mechi moja kati ya Ruvu Shooting na Simba itakayochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuanzia saa 10.15 jioni.

Hiyo itakuwa mechi ya raundi ya 24 kwa timu hizo ambapo Simba iko nafasi ya nne ikiwa na pointi 39 nyuma ya mabingwa Yanga wenye pointi 57, Azam yenye pointi 48 na Kagera Sugar ambayo ina pointi 40. Ruvu Shooting iko katika nafasi ya saba ikiwa na pointi 31.

Hadi sasa mabao 348 yameshafungwa katika ligi hiyo huku Yanga ikiongoza kwa kufunga 45. Polisi Morogoro yenye pointi 22 katika nafasi ya 12 ndiyo iliyofunga mabao machache ikiwa nayo 13 tu.

African Lyon yenye pointi 19 katika nafasi ya mwisho ndiyo inayoongoza kwa kuwa na kadi nyingi. Timu hiyo inayofundishwa na Charles Otieno ina kadi 44 ambapo kati ya hizo nne ni nyekundu. Mtibwa Sugar ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro yenyewe inaongoza kwa kuwa na kadi nyingi nyekundu ambapo hadi sasa inazo saba.


Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)

No comments:

Post a Comment